Na ABDALLAH AMIRI
MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga imewahukumu viongozi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mkusanyiko usio halali.
Waliohukumiwa kwenda jela ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Igunga ambaye kwa sasa ni Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Igunga, Vicent Kamanga (52), Mwenyekiti wa Chadema Tawi la Mwamsunga, Fea Rifa (41) na Katibu wa Chadema Tawi la Mwamsunga katika Kijiji cha Mgongoro, Luhanya Zogoma(48).
Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Igunga, Elimajid Kweyamba, alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, Ajali Milanzi kuwa watuhumiwa wote watatu wakiwa wafuasi na viongozi wa Chadema na wakiwa na nia ovu walifanya mkusanyiko usio halali wa Oktoba 30, 2016 kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni katika Kitongoji cha Mwamsunga wilayani humo.
“ Washitakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kinyume na kifungu 74 na 75 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 mapitio ya 2002 inayozuia kutenda makosa kama hayo,” alidai Kweyamba.
Watuhumiwa walikana kutenda kosa hilo na upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi watatu mahakamani ambao waliwatambua washitakiwa.
Akito hukumu hiyo, Hakimu Milanzi, alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka umewatia hatiani washitakiwa hivyo kila mmoja atatakiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela.
“Mahakama inamwachia huru mshitakiwa wa nne ambaye alikuwa ni Katibu wa zamani Chadema Wilaya ya Igunga, Idd Athumani, baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani,” alisema Hakimu Milanzi.