Clara Matimbo -Mwanza
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuacha kusababisha migogoro katika misikiti na taasisi za dini hiyo kwa masilahi yao binafsi kwa kuwa Mtume Muhamad (SAW) alisimamia amani na alipinga dhuluma.
Pia alimpongeza Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir kwa kupunguza migogoro iliyokuwapo katika baadhi ya misikiti na taasisi za dini hiyo maeneo mbalimbali tangu alipoingia madarakani mwaka 2016.
Majaliwa aliyasema hayo juzi jioni alipomwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika Baraza la Maulid wakati wa kilele cha maadhimisho ya kuzaliwa Mtume Muhamad (SAW) yaliyofanyika kitaifa jijini Mwanza.
Aliwataka viongozi wa dini hiyo kujitathmini kwa kiasi gani wameweza kufuata misingi ya dini hiyo, kama ilivyoasisiwa na muasisi wao ambaye alikuwa mwaminifu na alitenda matendo mema kwa manufaa ya binadamu wengine.
Alisema ili kumaliza na kuzuia migogoro isitokee, ni wajibu wa kila mmoja kumthamini mwenzake bila kujali tofauti za dini, siasa wala kabila kwa kuwa Mtume Muhamad (SAW) enzi za uhai wake hakumbagua mtu, bali alikuwa na uelewa mkubwa.
“Tujiulize, tunamuenzi vipi Mtume wetu, kwanini tunagombea uongozi katika misikiti na taasisi zetu za dini, wakati mafundisho yanatufundisha Mtume alikuwa mchungaji bora, aliwachunga kondoo wake kwa amani,” alisema.
Alisema migogoro mingi ya misikiti na taasisi za dini ya Kiislamu inasababishwa na viongozi wenye kutafuta masilahi binafsi.
“Tunampongeza Mufti Zubeir maana kwa kipindi kifupi cha uongozi ameweza kushughulikia matatizo hayo na kutengeneza Bakwata mpya.
“Rai yangu kwa viongozi wenzake endeleeni kumpa ushirikiano muitunze amani na mshikamano ili kuleta maendeleo, tambueni uongozi anaoupenda Mtume ni ule wa kujitoa kwa ajili ya wengine, sio wa kutaka masilahi yako binafsi,” alisema Majaliwa.
Kuhusu uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, unaotarajia kufanyika Novemba 24, mwaka huu, aliwataka Waislamu kufuata maelekezo ya Mtume Muhamad (SAW) kwa kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi watakaowafaa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alisema licha ya maadhimisho hayo kukumbusha mema yaliyofanywa na Mtume Muhamad (SAW), wapo baadhi ya viongozi wa misikiti wamekuwa wakitengeneza migogoro kwa masilahi yao binafsi.
Alisema kutokana na hilo wameagiza viongozi wa misikiti na taasisi zote kutoa ripoti ya utendaji kazi ili kudhibiti suala hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema mkoa utaendelea kuenzi amani kwa kushirikiana na viongozi wa dini zote, wadau na wananchi.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum, alisema Mufti Zubeir ameweza kuwaunganisha Waislamu wa madhehebu mbalimbali na kuleta maendeleo.