RAMADHAN HASSAN-DODOMA
VIONGOZI wa umma 11,330, sawa na asilimia 83 hadi kufikia Desemba 20M mwaka huu hawajarejesha tamko la rasilimali na madeni ya viongozi wa umma kwa Kamishna wa Maadili.
Hayo yalielezwa hapa jana na Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutoa tathmini ya hali ya urejeshaji wa tamko la rasilimali na madeni ya viongozi wa umma.
Alisema hadi Desemba 20, mwaka huu, tathmini inaonesha hali ya urejeshaji mpaka sasa si nzuri.
Alisema kati ya viongozi wa umma 13,699, wanaotakiwa kuwasilisha tamko, 2,369 sawa na asilimia 17 ndio waliowasilisha matamko yao.
“Kwa maoni yangu, kama hali itabaki hivi mpaka Desemba 31, haitaleta taswira nzuri hasa ukizingatia kwamba nchi yetu inafuata misingi ya utawala bora,unaohimiza ,uwazi na uwajibikaji sambamba na kuzingatia sheria,kanuni na taratibu,”alisema.
Alisema viongozi wa umma kushindwa kuwasilisha tamko, ni kosa chini ya kifungo cha 15 (a),aliwatahadharisha viongozi ambao watashindwa kutekeleza matakwa hayo kuwa Sekretariet ya Maadili haitasita kuwachukulia hatua kali ikiwemo kupelekwa kwenye Baraza la maadili.
Alipoulizwa ni viongozi wangapi wamewapelekwa kwenye Baraza la Maadili mpaka sasa “Ukikiuka maadili sisi hatuendi kwenye mahakama za kawaida, tuna utaratibu wetu unaishia katika Baraza la Maadili,kuna hatua kama mbili hivi kabla ya kufikia kwenye baraza.
“Kuna mwingiliano, ila makosa ya kimaadili ukikiuka, tuna utaratibu wetu chini ya sheria yetu tunaweza tukakupeleka kwenye baraza la maadili na faini ni milioni moja mpaka 5.
Alisema uvunjaji wa maadili ndiyo chanzo cha makosa makubwa ambayo yanatokea.
“Hatupendelei unaweza ukaonywa tukazungumza yakaishia hapo hapo kwa sababu unapelekwa huko ili iweje,kama kurejesha fomu lazima tukupeleke baraza la maadili kama hutatoa taarifa za kuridhisha,”alisema Kamishna huyo.
Aliwahimiza viongozi ambao bado hawajawasilisha matamko yao kutumia vizuri muda uliobaki kutekeleza matakwa hayo ya kisheria na hakutakuwa na muda wa nyongeza wa kuwasilisha nje ya muda huo.
“Napenda ieleweke wazi,sheria ya maadili ya viongozi wa umma haiwataki tu viongozi wa umma kuwasilisha matamko yao ya rasilimali na madeni, bali kutoa taarifa za kweli ndani ya matamko yao,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu mafisadi waliopelekwa mahakamani pamoja na wala rushwa sheria ya maadili inasema,Nsekela alisema sheria hawairuhusu kuwashughulikia watu wa namna hiyo.
“Sasa ukikutwa kwa kosa la ufisadi humu kwetu halimo kwenye sheria hii, kwahiyo sisi hatuwezi kukushughulikia kwani suala la ulaji wa rushwa halipo huku kwetu
“Ni kweli inawezekana kunatokea kukiukwa maadili mfano kupokea zawadi kwa sisi viongozi sio kosa ila ni ukiukwaji wa maadili ukipokea zawadi zaidi ya shilingi 200,000 unatakiwa umweleze mkuu wako wa kazi kwamba nimepokea zawadi ya shilingi 200,000.