30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Vinara kidato cha nne wafunguka

Na waandishi wetu –Dar/mikoani

VINARA wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne, uliofanyika Novemba mwaka jana, wamezungumzia siri ya mafanikio ya kufanya vizuri mtihani huo, huku wengi wakisema kumtanguliza Mungu, kujituma na ushirikiano wa wao, wazazi na walimu kuliwasaidia.

Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa, kutoka Shule ya St Francis Girls ya Mbeya, Joan Ritte, alisema matokeo haya yamemshtua na kufungua ukurasa mpya katika maisha yake, kwamba kila kitu kinawezekana.

Joan, mtoto wa mwisho katika familia ya watoto wanne ya William Ritte, yenye makazi yake eneo la Mnarani, Moshi, alisema kuwa alimtanguliza Mungu katika mambo yote, akijua kuwa atafanya vizuri katika matokeo yake, lakini suala la kushika namba moja kitaifa limekuja kwa kushtukiza.

“Kwa kweli nilikuwa na bidii, nilifanya juhudi sana ili kupata matokeo mazuri. Nilimtanguliza Mungu katika kila jambo. Nilijua kuwa nitafaulu, lakini ufaulu wa aina gani ndilo suala ambalo lilikuwa bado ni fumbo, hadi matokeo yalipotangazwa, ambayo kwa kweli yamenishtukiza.

“Ninawashukuru wazazi, walimu na wanafunzi wenzangu ambao kwa ushirikiano wao, kila mmoja kwa nafasi yake amechangia mafanikio haya ninayoyafurahia leo. Kwa kweli sikutegemea kwamba nitashika namba moja kitaifa, Mungu ni mwema,” alisema Joan.

Alisema matokeo hayo yamemshtua kwa sababu kulikuwa na wanafunzi aliokuwa nao darasani, ambao waliwahi kumpita kwa ufaulu darasani, japokuwa walikuwa wakichuana haswa, lakini anaona kuwa hao ndio waliosaidia kumpa nguvu ya kuongeza bidii na kuweza kufanikiwa kuweka rekodi.

Joan alisema ndoto yake ya baadaye ni kuwa mhandisi wa majengo (civil engineer) na anaamini fani hiyo itamsaidia na kumwezesha kushiriki katika ujenzi wa taifa, hasa kutekeleza kaulimbiu ya Serikali inayoelekeza ujenzi wa Tanzania ya viwanda inayoelekeza taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Ninapokwenda katika masomo ya kidato cha tano na sita, nitasoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu, ambayo yataniwezesha kufikia ndoto yangu ya kuwa mhandisi. Kwa hiyo ninaamini nitafanikiwa kufikia ndoto yangu na kuwa mtaalamu wa majengo, kwa ajili ya kuchangia kuinua uchumi wa nchi yangu,” alisema Joan.

NAMBA 2

Mwanafunzi aliyeshika namba mbili, Dennis Kinyange kutoka Nyegezi Seminari, alisema alitarajia ufaulu mzuri wa juu ya wastani, suala ambalo amekuwa akilipigania wakati wote.

Kinyange alisema matokeo ya mtihani huu yamemshangaza na kumpa furaha kwa kuwa ameingia katika 10 bora kitaifa na kushika nafasi ya pili, suala ambalo hakulitarajia.

“Nilikuwa nikifanya jitihada hasa kwa kumtanguliza Mungu. Nilijizatiti kwenye masomo, niliacha mambo mengine ili niweze kutimiza lengo langu, ninamshukuru Mungu kuwa pamoja na ushirikiano nilioupata kwa wazazi na walimu, nimefanikiwa kufanya vizuri kwa kiwango hicho,” alisema Kinyange.

Alisema ndoto zake ni kuwa daktari mtaalamu wa upasuaji hapo baadaye, suala ambalo ataendelea kuweka juhudi ili kuhakikisha anafanikiwa.

NAMBA 3

Mwanafunzi aliyeshika namba tatu, Erick Mutasingwa kutoka Sengerema Seminari, alisema kutokana na jitihada alizokuwa akifanya, alijua atafaulu, kwakuwa alisoma vitabu vingi na kufanya mazoezi mengi.

Alisema anamshukuru Mungu na amepokea matokeo kwa furaha, lakini kwa mshtuko, kwa kuwa pamoja na kuwa alitarajia kufanya vizuri, kushika nafasi ya tatu kitaifa ni suala ambalo wala hakuwa ameliwaza.

“Nimepokea matokeo kwa furaha sana, lakini kwa mshtuko, yamenishtua kwa kweli. Zaidi, ndoto yangu ya baadaye ni kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na ninamwomba Mwenyezi Mungu anisaidie kutimiza ndoto hii,” alisema.

NAMBA NNE

Akizungumza na MTANZANIA, mwanafunzi kutoka St Francis Girls aliyeshika namba nne kitaifa, Rosalia Mwidege, alisema amepokea matokeo kwa mshtuko kwa kuwa japokuwa alitarajia kufanya vizuri, suala la kung’aa katika 10 bora kitaifa ni mipango ya Mungu.

Alisema anamshukuru Mungu kwa kumsimamia na kumwonyesha njia, zaidi wazazi wake ambao wamekuwa na moyo wa kumsaidia kwa hali na mali na kuhakikisha anapata kila alichokuwa akikihitaji.

“Kwa kweli ninamshukuru Mungu kwa kunipa wazazi wenye uwezo wa kunisaidia, ambao wamekuwa tayari kujua ninahitaji nini na wako tayari kunisaidia muda wote. Lakini pia ninawashukuru walimu wangu, ambao wamenifundisha kuanzia chekechea.

“Ninakumbuka kila sehemu ambayo nimekuwa nikipita kimasomo, kuanzia chekechea kulikuwa na mwalimu anayenihimiza kuhakikisha ninafanya vizuri, suala ambalo limetokea nikiwa shule ya msingi na nikiwa sekondari pia. Mchango wao ni mkubwa kwangu katika mafanikio niliyoyafikia,” alisema.

Alisema kwa sasa ndoto yake kielimu ni kuhakikisha kuwa anaendelea na masomo bila kusimama hadi atakapopata shahada ya uzamivu (PhD) na kuwa profesa katika masuala ya uchumi, lakini kiuchumi, anapenda kuwa mjasiriamali.

“Katika ndoto zangu, ukiacha ndoto ya mafanikio ninayoyahitaji kielimu, ninataka niwe mjasiriamali, nilime mazao mbalimbali, nifuge wanyama kwa kadiri Mungu atakavyoniwezesha. Katika yote, ninashukuru ushirikiano wa hali na mali na maombi ninaoupata kwa wazazi na ndugu zangu,” alisema Rosalia.

NAMBA SITA

Kwa upande wake, mwanafunzi Mvano Cobangoh wa Feza Boys Dar es Salaam, ambaye ameshika nafasi ya sita kitaifa, alisema hakuamini kushika nafasi hiyo licha ya kwamba alikuwa na ndoto za kufanya vizuri katika mtihani wake wa mwisho.

“Baba alifariki, lakini siku zote nikiwa na baba alikuwa akinisisitiza kusoma kwa bidii na hata kumuheshimu mama pindi yeye atakapofariki, kwa kuwa alikuwa na ugonjwa ambao ilikuwa ni lazima atuandae katika maisha yote ikiwamo elimu.

“Hata hivyo, naishukuru shule yangu ya Feza kwa kuendelea kumsaidia mama yangu, hasa kumpunguzia majukumu mengine na kumfanya afanikishe mimi kumaliza kidato cha nne na kufanya vizuri,’’ alisema Cobangoh.

Aliongeza kuwa kufaulu kwake ni juhudi yake ya kusoma sana usiku hadi saa sita sambamba na kuwasikiliza walimu wanapokuwa wanafundisha.

Mama mzazi wa mwanafunzi huyo, Upendo Komba, alisema kutokana na uwezo aliokuwa nao mtoto wake, aliamini angeweza hata kuwa mwanafunzi bora kitaifa.

Cobangoh alisema alikuwa anapendelea masomo ya Sayansi, hasa Hisabati na Fizikia na anatamani kuwa rubani wa ndege katika maisha yake ya ajira hapo baadaye.

Hata hivyo, aliushukuru uongozi wa Shule ya Feza kutokana na kumpa nguvu, kumtia moyo wakati wote pindi alipokuwa kwenye changamoto ya malezi akiwa peke yake bila ya mume.

“Nashukuru Mungu nafasi hii ya leo angekuwa baba yake anazungumza na waandishi, lakini hata hivyo Mungu ana makusudi yake.

“Tangu nawalea watoto wangu alioniachia wawili, sikuwahi kukumbana na changamoto yoyote, hasa katika suala la maadili, ni kwamba wote wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao,’’ alisema Upendo.

NAMBA SABA

Kwa mwanafunzi Agatha Mlelwa kutoka Shule ya St Francis ya Mbeya aliyeshika nafasi ya saba, alisema anamshukuru Mungu kwa matokeo hayo kwa kuwa anaamini ni kutokana na maombi, kujituma, kupangilia muda na kujitambua, kwa pamoja na juhudi, aliweka kila kitu mikononi mwa Mungu.

Agatha alisema suala muhimu analoamini ni maombi, juhudi na kuhakikisha kuwa unasoma na kuelewa kile unachofundishwa, siyo kukariri.

“Lakini zaidi, ni kuwa na nidhamu na kusikiliza, kisha kufuata ushauri mzuri kutoka kwa wazazi na walimu, pamoja na kuwa tayari kushirikiana na wanafunzi wenzako,” alisema Agatha.

Alisema ndoto yake ni kuwa daktari wa viungo, hasa akilenga zaidi kuwa mtaalamu mbobezi kwenye masuala ya moyo, kwa kuwa amekuwa akiona huruma sana kwa watu wanaotaabika, hasa kwenye magonjwa ya moyo.

NAMBA 10

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Huruma iliyopo Dodoma, Lucy Magashi ambaye ameshika nafasi ya 10 kitaifa, alisema amepokea taarifa hizo kwa furaha kwa kuwa kuingia katika 10 bora ni historia ya kipekee katika maisha yake.

Lucy ambaye matarajio yake makubwa ni kuwa daktari bingwa wa watoto, alisema ni kweli kwamba alitarajia kufanya vizuri, lakini suala la kuingia katika 10 bora kitaifa limekuja kama muujiza, hivyo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpa nafasi hiyo.

“Ninawashukuru pia wazazi kwa kunisimamia vyema, ninawashukuru walimu kwa kuniongoza vyema katika masomo. Kwa kweli sina la kusema, nilitarajia kufanya vizuri sana, lakini sikujua kama nitaweza kuingia katika 10 bora kitaifa, ninamshukuru Mungu kwa kweli,” alisema Lucy.

WAKUU WA SHULE

Mkuu wa Shule ya St Francis Girls ya Mbeya, Cristevina Vas ambaye shule yake imetoa wanafunzi sita kati ya 10 walioongoza kitaifa, alisema wamepokea matokeo hayo kwa furaha kwakuwa wanaona ni sehemu ya kuunga mkono juhudi ambazo wamekuwa wakizifanya ili kuhakikisha wanatoa wanafunzi bora.

Vas alisema juhudi miongoni mwa walimu, wanafunzi na ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka kwa wazazi katika kuimarisha nidhamu ya wanafunzi na wafanyakazi, ni imani iliyoijenga shule hiyo kuwa na matokeo mazuri katika mtihani wa kidato cha nne.

“Lakini zaidi, ni ushirikiano wa dhati baina ya wanafunzi, ambapo hata wanafunzi wachache ambao walikuwa wakifanya juhudi zao binafsi na kugundua mambo au kupata maarifa ya nyongeza, walikuwa tayari kushirikiana na wenzao katika maarifa hayo,” alisema.

Mwalimu wa Mipango (coordinator) wa Huruma Sekondari iliyopo Dodoma, Aloyce Martin alisema wamepokea vizuri matokeo hayo kwa kuwa yanawaelekeza kutimiza ndoto yao ya kuondoa kabisa daraja la pili katika shule hiyo.

Alisema katika matokeo hayo ya mwaka jana yaliyotangazwa rasmi jana, katika wanafunzi 49 waliomaliza kidato cha nne, 42 wamepata daraja la kwanza na saba pekee ndio waliopata daraja la pili.

“Kwa hiyo kwa matokeo haya, tunafarijika kwa kuwa tunaelekea kutimiza ndoto yetu ya kufuta madaraja yote, kwa sasa tukiwa tunaelekea kufuta daraja la pili na kubaki na daraja la kwanza pekee.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Sengerema, Fr Francis Mganyizi alisema amefarijika kwa kuwa unapompokea mtoto na kisha akawa na matokeo mazuri, ni suala la kujivunia.

Alisema ni kweli kwamba walikuwa wakitarajia mwanafunzi wao, Erick kufanya vizuri kwa kupata A saba na kuendelea, lakini wastani alioupata wa zaidi ya A 10 na kushika nafasi ya tatu katika 10 bora kitaifa ni jambo ambalo hawakulitarajia moja kwa moja, hivyo limewapa heshima kubwa.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyegezi Seminari, Fr. Theophil Kumalija alisema mwanafunzi wake Dennis Kenyagi aliyeshika nafasi ya pili kitaifa, alikuwa na uwezo mkubwa kiasi cha kutumiwa na walimu kufundisha wenzake.

Alisema matokeo hayo ambayo shule yake imeshika nafasi ya 16 kitaifa katika darasa lenye wanafunzi 54, wanafunzi 52 wamepata daraja la kwanza huku wengine wawili wakipata daraja la pili.

“Haya ni mafanikio makubwa kwetu kwani hatukutarajia ingawa tumekuwa tukifanya vizuri kila mwaka, lakini kwa miaka kumi haya ndiyo matokeo makubwa kwa shule hii na hakika juhudi zetu zimezaa matunda na ndiyo maana hata kwa mkoa tumefanya vizuri na tumeshika nafasi ya pili.

“Mimi nilikuwa mwalimu wake wa somo la Kemia toka kidato cha kwanza hadi kidato cha tatu, kwa kweli alikuwa ni mtu ambaye hataki umfundishe kila kitu, alitaka umfundishe kidogo halafu vitu vingine anavifanyia kazi mwenyewe na hata baada ya kuhitimu, shule ilimpatia vyeti.

“Siri kubwa ya mafanikio ni nidhamu kwa wanafunzi ambapo Dennis mwenyewe pia alikuwa na nidhamu kubwa ya muda na ndiyo maana leo tunaona amevuna matokeo haya ambayo yameiletea sifa sana shule yetu.

“Pia suala la kutimiza majukumu kwa walimu na watumishi wote wa shule imekuwa na mchango mkubwa katika kufikia mafanikio haya, hivyo niwashauri wakuu wenzangu wa shule wazingatie nidhamu na matumizi ya muda mashuleni kwani vitu hivyo vina mchango mkubwa katika kufikia mafanikio ya kielimu.

“Pia nitoe wito kwa shule zote zijifunze kuheshimu walimu na kuwawezesha waweze kutimiza majukumu yao kwa ufasaha kwa kuwa iko wazi kuwa walimu ndio wanajenga taifa,” alisema Fr. Kumalija.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles