VILIO VYAIBUKA UPYA AJALI LUCKY VINCENT

0
924
Wazazi na walezi wa wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliofariki kwa ajali ya basi iliyotokea Mei, mwaka huu wakiweka mashada ya maua kwenye eneo la ajali wakati wa ibada maalumu iliyofanyika eneo la Mlima Rhotia,Karatu mkoani Manyara jana.PICHA: JANETH MUSHI

Na Janeth Mushi – Karatu

VILIO, simanzi na majonzi viliibuka upya jana eneo la Mlima Rhotia, wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha, wakati wazazi na walezi wa wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi Lucky Vincent waliofariki kwa ajali ya gari, walipotembelea eneo hilo kufanya ibada maalumu.

Wazazi na walezi walifika hapo ili kuwaombea watoto  hao, walimu wawili na dereva waliofariki Mei 6, mwaka huu.

Wanafunzi watatu pekee walinusurika na hadi sasa wanaendelea na matibabu nchini Marekani.

Hali ya simanzi ilianza mara wazazi hao walipofika eneo hilo wakiwa katika mabasi mawili saa sita mchana.

Walipokewa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Ibada hiyo iliyoenda sambamba na uwekaji mashada ya maua pembeni mwa daraja ambalo basi hilo lilitumbukia, ilihudhuriwa pia na wananchi wa eneo jirani.

Mara baada ya ibada, DC Mahongo aliongoza msafara wa wazazi hao hadi Shule ya Msingi Tumaini Junior, ambayo wanafunzi hao walikuwa safarini kwenda kufanya mtihani wa kupimana uwezo na wenzao wa shule hiyo.

Msafara huo ulipowasili shuleni hapo, wanafunzi wa darasa la saba wa Tumaini Junior walipanga msitari na kupeana mikono na wazazi hao hali iliyoibua huzuni miongoni mwao na kuibua vilio.

Akizungumza mara baada ya ibada, Mahongo alisema kuwa siku ya ajali hiyo kulikuwa na ukungu na kwamba hivi sasa wameanza kuboresha eneo hilo kwa kuweka alama za barabarani.

Mahongo alisema wanafanya mazungumzo na wadau mbalimbali ili waweke mabango na kwamba suala la ukingo linashughulikiwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) ambao wameshaanza katika baadhi ya maeneo wilayani humo.

Naye Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alitumia fursa hiyo kukabidhi rambirambi zaidi ya Sh milioni 2.9 kwa Mahongo zilizochangwa na wabunge wa Chadema ili azikabidhi kwa wafiwa.

Naye Mwenyekiti wa Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Kanda ya Kaskazini Magharibi, Mchungaji Ezekiel Dangalo alikabidhi hundi ya Sh milioni 19.5 zilizochangwa na wanachama wake.

Mahongo alikiri kusitishwa kwa rambirambi, lakini alisema haizuii wananchi kuendelea kujitokeza kuwapa pole wazazi hao waliofiwa.

“Ili isionekane na Mkuu wa Wilaya ya Karatu alipewa rambirambi akatumia vinginevyo, niombe wananchi waendelee kuwafariji wafiwa maadam sasa wana uongozi wao na mimi namkabidhi hundi hizi mwenyekiti wa wazazi,” alisema Mahongo huku  akimkabidhi hundi hizo mwenyekiti huyo wa wazazi waliofiwa na watoto, Peniel ole Ndemno.

Itakumbukwa kuwa fedha hizo zilishindwa kukabidhiwa tangu Mei, mwaka huu baada ya Mkuu wa Mkoa, Gambo kudaiwa kutoa maelekezo kwa polisi kuwakamata waliokuwa kwenye hafla ya kuwakadhi wazazi fedha za rambirambi ambayo ilihudhuriwa na Lazaro, viongozi wa dini, waandishi wa habari na wamiliki wa shule.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shule ya Tumaini Junior, Modest Bayo, alipozungumza alisema kuwa walianza mahusiano na Shule ya Lucky Vicent miaka minne iliyopita wakati wanafunzi hao walipokwenda kufanya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Ngorongoro na kulala shuleni hapo.

Watoto watatu majeruhi wa ajali hiyo ambao wanatibiwa nchini Marekani wanatarajiwa kurudi nchini Mwezi ujao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here