23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Vikwazo kwa wanawake, vijana kuwania nafasi za uongozi

Janeth Mushi -Arusha

“DEMOKRASIA ya usawa itasaidia kuongeza idadi ya wanawake na vijana katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, japo sasa hivi hali ni tofauti kidogo na kipindi cha nyuma.

“Mwamko wa makundi ya wanawake na vijana umeongezeka katika kuwania nafasi za uongozi na hata waliofanikiwa kupata wameonyesha njia hasa kuwatetea wenzao.”

Hiyo ni kauli ya kijana aliyejulikana kwa jina la Danstan Panga, mkazi wa Karatu, mkoani Arusha, aliyoitoa hivi majuzi katika moja ya mafunzo ya viongozi wa vyama vya siasa katika ngazi za kata na wilaya zilizopo mkoani hapa.

Anasema demokrasia ya usawa ndani ya vyama vya siasa hapa nchini itakuza ushiriki wa wanawake na vijana katika kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Anasema kumekuwa na uteuzi wa kimaslahi katika vyama vingi vya siasa hapa nchini, hali inayochangia makundi hayo kukutana na vikwazo vya uteuzi.

“Tunafahamu vijana lazima waandaliwe katika siasa ila tukiangalia zuio la mikutano kwa vyama vya siasa, muda wa kuwaandaa vijana unakosekana. Hii nayo ni changamoto na ukiangalia chaguzi za mwaka huu na mwakani hazina hamasa, fursa za mikutano ingekuwapo tungeweza kuandaa vijana watakaokuwa viongozi bora,” anasema.

Naye Edwin Johnson, mkazi wa eneo la Ngaramtoni, anasema baadhi ya mila na desturi potofu miongoni mwa jamii zikiwekwa pembeni zitachangia ongezeko la wanawake na vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini.

Anasema hayo wakati wa ‘road show’ ya uhamasishaji wa wanawake na vijana kuwania nafasi za uongozi iliyotolewa hivi karibuni kwa wakazi wa eneo hilo kupitia mradi wa kukuza ushiriki wa wanawake na vijana katika kuwania nafasi za uongozi katika chaguzi za 2019/2020 (Wypre), unaofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) na kutekelezwa na Tawla, tawi la Arusha.

Anasema elimu kwa jamii ni muhimu kutolewa ili kupunguza na kumaliza baadhi ya mila na desturi zinazochangia wanawake kushindwa kuwania nafasi za uongozi.

“Uhamasishaji huu utasaidia wanawake kuwa majasiri na kujitokeza kwa wingi, tukianzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, itakuwa fursa nzuri kwao na elimu na taarifa sahihi zikipatikana kila mtu atajihusisha vema na suala alilopatia taarifa,” anasema.

Anaongeza: “Baadhi ya mila na desturi mbaya zinaathiri mno maendeleo ya kina mama, suala la uongozi mila na desturi zikiwekwa pembeni, kila mtu atakuwa na imani juu ya mwenzake, kila mtu atamheshimu mwenzake hasa utu, utu ukiheshimika kila mtu atatumia kipawa chake.”

WANAWAKE KUKABILIANA NA RUSHWA YA NGONO

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji wanawake Mkoa wa Arusha, Anna Msuya, anawataka vijana na wanawake wanaojipanga kuwania Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani mkoani hapa, kujipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoyakabili makundi hayo ikiwamo rushwa ya ngono na kutojiamini.

Anasema iwapo makundi hayo yamejipanga kuwania nafasi mbalimbali katika chaguzi hizo, wanapaswa kuacha woga, kuwa wajasiri na kujipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kipindi cha mchakato wa uchaguzi.

“Wanawake wana changamoto zaidi nyakati za uchaguzi ukilinganisha na vijana hivyo, ni wajibu wao pamoja na vijana kwa ujumla kuzingatia maadili na kuepuka tabia zisizokubalika katika jamii ili wasikumbane na vikwazo pindi wanapowania nafasi hizo,” anasema na kuongeza:

“Ni lazima mpange mikakati na mbinu za kuhakikisha mnaweza kukabiliana na changamoto hizo bila kujali kukatishwa tamaa ila kwa wanawake ni muhimu pia kuandaa familia zenu kabla ya kuwania nafasi hizo kwani tuna mifano mingi, baadhi ya wanawake waliojiingiza kwenye siasa baadaye ndoa zao huvunjika na familia kugawanyika,” anasema.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Arusha, Firmin Nnko, anasema kupitia mafunzo hayo anaamini vijana na wanawake wataiva na katika maeneo wanayotoka kutapatikana viongozi bora watakaoitumikia vyema jamii.

“Kwa kutambua kuwa jamiii haiangalii vyama bali utendaji, makundi haya yakiandaliwa bila kujali itikadi za vyama vya siasa itasaidia kubeba makundi makubwa ya kuwaongoza na wengi watajitokeza zaidi kushiriki katika chaguzi hizo,” anasema. 

Naye Tumaini Naimani, ambaye ni mkazi wa Wilaya ya Arumeru, anasema elimu hiyo itasaidia hasa wanawake kupata wawakilishi katika ngazi za uamuzi na kwamba elimu zaidi ya uhamasishaji inapaswa kutolewa hasa kwa maeneo ya pembezoni.

Anasema wanatarajia kupatikana elimu zaidi kuyajengea makundi hayo uwezo wa  kuzungumza kwa kujiamini na kujenga ushawishi kwa wapiga kura, ili waweze kuchaguliwa kutegemeana na mchango wao katika jamii.

Anazitaja changamoto kubwa walizobaini kwa wanawake kuwa ni pamoja na kutokujiamini, rushwa ya ngono na familia zao kutokupendezwa na wao kujitosa katika siasa, pamoja na vita iliyopo miongoni mwa wanawake wenyewe.

“Kwa upande wa vijana, changamoto kubwa inayowakabili ni baadhi yao kukosa maadili ya uongozi, kutumika zaidi kama wapiga kampeni na siyo wawania nafasi za uongozi, pamoja na jamii kutowaamini kutokana na kutokuwa na  maisha ya kudumu kwa kukosa familia na makazi.

“Tunaamini kupitia elimu ya mpiga kura idadi ya wagombea itaongezeka,” anasema.

Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambayo ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kusimamia uchaguzi huo, imeandaa mwongozo, kanuni  mbalimbali za kusimamia uchaguzi huu ukiwemo Mwongozo wa Elimu ya Mpiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019.

Ikizingatiwa kuwa wizara hiyo itashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu hiyo, mwongozo unaainisha kuwa elimu ya mpiga kura itatolewa kwa kuzingatia uwapo wa makundi maalum ambayo ni muhimu kupatiwa elimu hiyo. 

Baadhi ya makundi hayo kwa mujibu wa mwongozo huo ni vijana, ambao wameainishwa kuwa ni kundi maalum kwa sababu uelewa wao kuhusu umuhimu wa uchaguzi ni mdogo hivyo, kunahitajika kutumia njia ambazo zitawavutia vijana wengi kushiriki katika uchaguzi zikiwamo mitandao ya kijamii, matamasha ya muziki, ngoma za asili na mihadhara rasmi.

Katika mwongozo huo, kundi la wanawake linaainishwa kuwa ni maalum kutokana na kuwa na majukumu mengi ya kifamilia na mfumo dume.

Ni dhahiri kwamba kutokana na mwongozo huo kutoa wajibu wa wadau kuwa ni pamoja na kila mdau atakayepata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura, anatakiwa kuheshimu na kuzingatia sheria za nchi na kutumia kwa usahihi mwongozo huo. Aidha, wadau wana wajibu mkubwa wa kuhamasisha makundi hayo kushiriki kuwania nafasi za  uchaguzi.

Wanawake na vijana wengi hasa wa maeneo ya pembezoni wakifikiwa na elimu hiyo, watajitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali na kuweza kupata wawakilishi katika ngazi za uamuzi na kuondoa dhana ya kukimbilia kuwania nafasi za juu hasa kwa vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles