NA TIMOTHY ITEMBE TARIME
JESHI la polisi mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya linawashikilia vijana watano kwa tuhuma za kumuua kwa kumuchoma na mshale shingoni mwalimu Justine Sospeter Ogo wa Shule ya sekondari Itiryo.
Kamanda mkoa wa kipolisi Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, alisema tukio hilo lilitokea Novemba 14,2019 asubuhi katika Kijiji cha Itiryo.
“Chanzo cha mauaji hayo ni vijana wapatao wanane walikuwa wanatembea barabarani wakiwa na silaha za jadi wakiwa wanajiandaa kwenda kwenye tohara Desemba, walikuwa wanasimamisha watu na kuwaomba fedha kwa nguvu kuonyesha ujasiri.
“Mwalimu aliyeuawa alikuwa anampeleka mwenzake kusimamia mitihani ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bungurere, (vijana hao) wakamsimamisha na kuanza kumdai awape fedha, mwalimu na wenzake wakawa wanaondoka bila kusimama, ndipo kijana mmoja wapo alimchoma na mshale shingoni kutoka upande wa kulia na kutokea upande wa kushoto, alifariki alipofikishwa hospitali,”alisema Mwaibambe.
Mwaibambe alisema vijana watano wamekamatwa kati ya nane wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo na jeshi la polisi linaendelea kuwasaka wengine waliobaki.
Alitaja majina ya vijana hao kuwa ni Nchore Richard, Marwa Mwita Gichome, Gisiri Simion Mhere, Makenge Hongo Chacha na Muhere Mwita Gichumu.
Alisema kwa sasa vijana hao wanashikiliwa kwa mahojiano na taratibu zikikamilika watafikishwa mahakamani.
Kamanda Mwaibambe alitumia nafasi hiyo kuwataka wazazi, walezi na wananchi kuwafunza watoto wao maadili mema vinginevyo sheria haitasita kuwachukulia hatua watoto wote wanaojihusha na vitendo vya kihalifu.
Awali akisimulia tukio hilo, Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Sekondari Itiryo, Nicku Bariki, alisema mwalimu huyo aliuawa akiendesha pikipiki wakati akiwa njiani na wenzake wawili aliokuwa amewapakia wakielekea Shule ya Sekondari Bungurere kusimamia mitihani.