VIJANA WANAVYOTUMIA TAKA KUJIPATIA MAMILIONI

0
668

NA VERONICA ROMWALD–DAR ES SALAAM

KILIO cha ukosefu wa ajira si tu cha Tanzania bali ni kwa dunia nzima, kundi kubwa linaloathirika likiwa ni la vijana.

Tunashuhudia wengi wakikata tamaa huku baadhi yao wakiamua kujiingiza katika shughuli ambazo si halali.

Wengine kutokana na hali hiyo wamekata tamaa na wamekuwa wakitumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya na hili ni janga la Taifa.

Vijana ni nguvu kazi muhimu inayohitajika kutumika kwa Taifa lolote duniani katika shughuli za uzalishaji kukuza uchumi wake.

Kila kukicha kilio cha ukosefu wa ajira kinazidi kuongezeka, huku Serikali katika kila nchi zikijitahidi kutafuta mbinu za kukimaliza.

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imedhamiria kufufua viwanda kupitia kaulimbiu yake ya Tanzania ya viwanda ili kukabiliana na hali hiyo.

Jambo hilo linaungwa mkono na wadau wengi hasa vijana wenyewe, lakini bado kuna changamoto nyingi kufikia lengo hilo hasa sera nzuri za kuhamasisha uwekezaji wa kutosha nchini.

Miaka ya nyuma vijana wengi walisoma wakitarajia kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo yao, lakini si wote waliokuwa wakiajiriwa na hivyo kujikuta wengi wakiishia mitaani, huku wakiwa hawana ajira ya kuwaingizia kipato.

Leo hii ingawa bado wapo ambao wamebaki na mawazo mgando (wanasubiri kuajiriwa), wengi wameamka na kuamua kujiajiri wenyewe na sasa wanafurahia matunda ya maamuzi yao.

Sabore Mussa ni Meneja wa Kampuni ya Africraft, anasema yeye na wenzake zaidi ya 10 waliamua kutumia mikono yao kujitengenezea ajira.

“Tulitafakari namna gani tunaweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, tukaona ni vema tutumie ufahamu tulionao kubuni bidhaa mbalimbali na kutumia mikono yetu kuzitengeneza bidhaa hizo,” anasema.

Mussa anasema walianzisha kampuni yao mwaka 2006 na kwamba huwa wanatengeneza bidhaa zao kwa kutumia malighafi ambazo wengi huzitupa baada ya kumalizika muda wake.

“Wazo letu ni la tofauti kidogo na wengi wanavyodhani, tunatumia makopo yaliyokwishatumika hasa yale ya soda za kopo, vifuu, chupa, mifuko ya plastiki, viroba vya unga wa ngano na sembe na ile ya saruji.

“Utaona malighafi hizi wengi huzitupa baada ya kuzitumia na kutokana na hali hiyo, taka hizo zimekuwa zikichangia mno uharibifu wa mazingira yetu,” anasema.

Anasema tangu wakati huo hadi sasa kampuni yao imekuwa na wameweza kufundisha vijana wenzao ambao wamejiajiri kwa kazi hiyo.

“Sasa hivi tupo vijana zaidi ya 30 ambao tumejiajiri kwa kazi hii, tumesambaa katika maeneo mbalimbali nchini,” anasema.

Kuhusu soko

Anasema wamefanikiwa kupata soko kubwa la bidhaa zao wanazotengeneza hasa nchini Ujerumani na Marekani.

“Soko la ndani (Tanzania) si kubwa sana kama tunavyoona Ujerumani na Marekani, kwa mfano kuna bidhaa ambayo katika soko la ndani tutauza kwa Sh 2,000, bidhaa hiyo hiyo tukiipeleka nje hasa nchi hizi mbili tunaweza kuiuza kuanzia Sh 10,000 na kuendelea,” anasema.

Mussa anasema hiyo ni kwa sababu mwamko wa Watanzania kupenda bidhaa zinazotengenezwa ndani kwa malighafi za Kitanzania ni mdogo.

“Wengi wanapenda kutumia bidhaa zinazotoka nje ya nchi lakini ili tukuze uchumi wetu, wakati umefika sasa tuanze kupenda bidhaa zetu za ndani zilizotengenezwa na Watanzania wazalendo,” anasema.

Anasema Serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri kwa wabunifu, wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani ili vijana wengi zaidi wavutiwe kujiajiri.

Amabilis Batamula ni Mkurugenzi wa Habari wa Jarida la Fema, anasema vijana wengi bado hawajui kwamba wanaweza kujipatia mamilioni ya fedha katika taka.

“Vijana hawana elimu ya kutosha kwamba taka wanazoziona zikizagaa huko mitaani wanaweza kuzitumia kujipatia fedha na kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira, zinabaki na kuchafua mazingira,” anasema.

Anasema leo hii dunia inashuhudia mabadiliko ya hali ya nchi ambayo yamechochewa zaidi na uharibifu wa mazingira.

Anasema Juni 5, mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, waliungana na wadau mbalimbali kusherehekea siku hiyo kwa njia ya kipekee.

“Tulikutana na vijana na kuwapa elimu namna wanavyoweza kutumia taka kupata fedha, tunaamini watatumia elimu hiyo kujiajiri, tunahimiza wajiajiri na walinde mazingira, kwa sababu dunia inatuhitaji tuitunze, tusipoitunza na yenyewe itashindwa kututunza,” anasisitiza Batamula.

Anaongeza: “Utaona matairi ambayo yamekwishatumika kwenye magari mengi hutupwa, kandambili hutupwa pia, lakini zipo ambazo vijana wamefanya usafi huko baharini zikizagaa zimetumika kutengeneza mapambo mazuri mno, utashangaa.

“Kwa hiyo wamesafisha kulinda mazalia ya samaki lakini pia wamejipatia fedha, ndiyo maana tumeamua kuhamasisha vijana watumie fursa hii kwani licha ya kupata kipato tutalinda mazingira yetu ikiwamo kuzuia mmonyoko wa udongo.

Mhifadhi Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira, Alhaji Seleman Kisimbo, anasema ili kuendana pia na dhamira ya Serikali ya Tanzania ya viwanda, ni wakati mwafaka Watanzania kutumia elimu hiyo.

“Elimu ya kubadili taka kuwa bidhaa imekuja wakati mwafaka, nawasihi vijana watumie fursa hii na watafute taarifa zaidi ili kwa pamoja tufikie lengo kufikia Tanzania ya viwanda, lakini pia kulinda mazingira, jambo ambalo ni wajibu wa kila mmoja wetu,” anasema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here