24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

‘VIJANA WANATUMIA KIVULI CHA UCHAWI KUWAPORA WAZEE’

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba.

Na LEONARD MANG’OHA,

MAUAJI ya kujichukulia sheria mkononi yamekuwa kama jambo la kawaida miongoni mwa Watanzania. Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia watu wasio na hatia wakiuawa katika matukio mbalimbali.

Wananchi wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa watu wanaotekeleza uhalifu kama vile wizi, ubakaji na mingineyo.

Hili ni jambo la kutisha na lisilohitaji kufumbiwa macho na kila mpenda amani katika nchi hii, kwani licha ya kuwa linakatisha maisha ya watu, pia linaitangaza vibaya nchi katika duru za kimataifa, hali inayoweza kusababisha kutajwa kama moja ya nchi zisizo salama kuishi licha ya kuwa haina vita kama nchi zingine jirani zinazokabiliwa na vita za mara kwa mara.

Ni hivi karibuni gazeti hili liliripoti habari ya kuuawa kwa watu wawili wilayani Mkuranga mkoani Pwani, katika tukio la mgogoro uliohusisha wakulima na wafugaji, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni baada ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.

Katika tukio hilo inadaiwa kuwa baada ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na wakulima kuikamata mifugo hiyo, wafugaji walikwenda nyumbani kwa mmoja wa waliouawa, Mwidini Saidi (22) kumfuata baba yake ili wamuue.

Baada ya kumkosa, walimkamata Said akiwa njiani kurejea nyumbani na kumuua, mauaji ambayo yaliyoibua hasira za wafugaji na hivyo kwenda kulipa kisasi kwa kumuua mtu aliyetajwa kwa jina la utani (Msukuma), ambaye alipigwa na kuchomwa moto.

Pamoja na jitihada kadhaa zinazochukuliwa na Serikali kukomesha mauaji haya, bado sizioni juhudi za dhati za kuyakomesha, au vyombo husika vinafurahia kuendelea kwa matukio hayo, kama si hivyo ni lini watazuia kuendelea kwa mauaji haya ya kutisha?

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, amekuwa akilaani mara kwa mara matukio ya aina hii akisema hayapaswi kufumbiwa macho.

Matukio haya ni mwendelezo wa matukio ya kikatili yanayoendelea kujitokeza siku hadi siku nchini ambayo yamekuwa yakikiuka haki za binadamu.

Pia kumekuwapo na mauaji ya wazee katika maeneo mbalimbali nchini, hasusan katika Kanda ya Ziwa, ambapo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mwaka 2015 takribani watu 500 huuawa kila mwaka.

Mwaka 2012 watu 630 waliuawa katika maeneo mbalimbali nchini, mwaka 2013 waliouawa ni 765 wakati 2014 hakuna taarifa ya mtu kuuawa iliyoripotiwa na 2015 waliouawa ni 425.

Utafiti huo unaonyesha kuwa mauaji yanayohusisha imani za kishirikina yanatekelezwa zaidi Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kati ambapo mwaka 2015 watu 300 waliripotiwa kuuawa katika Mkoa wa Tabora huku mauaji ya watu 84 yakitekelezwa katika Wilaya ya Kaliua.

“Idadi ya watu wanaouawa kutokana na imani za kishirikina inaonyesha wazi kuwa imani hizo bado zinapewa nafasi kubwa katika maisha ya Watanzania. “Mwaka 2010 katika utafiti uliofanywa na Pew Forum ulionyesha asilimia 93 wanaamini uwepo wa uchawi,” unaeleza utafiti huo.

Akizungumza na gazeti hili, Kijo- Bisimba, alisema baadhi ya Watanzania hutumia kisingizio cha ushirikina kuwapora mali wazee.

Anasema baadhi ya watekelezaji wa mauaji hayo wanapomwona mzee ana mali huwatafutia mbinu ya kuwanyang’anya, inaposhindikana huwazushia kuwa ni wachawi hivyo kutokana na jamii hizo kuamini imani hizo hushawishika kutekeleza mauaji.

Anasema mauaji hayo husababishwa na uelewa mdogo miongoni mwa wananchi sambamba na kutojiamini pale wanapopatwa na matatizo mbalimbali kama vile magonjwa.

Rai yake kwa vyombo vya dola nchini ni kuhakikisha vinakomesha mauaji hayo kwa namna yoyote ile kutokana na tatizo hilo kuongezeka siku hadi siku.

“Polisi wachukue hatua za kisheria japo wanasema inakuwa vigumu kuwatambua waliotekeleza mauaji kwa sababu wanakuwa katika ‘mob’.

“Lakini hawa watu hata kama wanatekeleza mauaji wakiwa wengi wakikamatwa hata wawili wakafikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua stahiki, itakuwa fundisho kwa wengine” anasema Kijo-Bisimba.

Aidha, wananchi wanapaswa kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha ushirikina jambo ambalo si rahisi kulithibitisha na kutokana na kuwa nadharia tu miongoni mwa watu wanaoamini katika hilo.

Kijo-Bisimba anawataka wananchi kufuata taratibu za kisheria hata kama watabaini mtu ametenda kosa walilokuwa wakimtuhumu.

Kuhusu wazee 500 kuuawa kila mwaka, anasema jamii hususan vijana wanapaswa kutambua kuwa uzee si jambo ambalo mtu hujitakia mwenyewe limfike, bali ni suala la lazima kwa mtu yeyote anayefikia umri mkubwa.

Anasema sera ya wazee inapaswa kuangaliwa na kuzingatiwa ili kuhakikisha inatoa mafao kwa wazee, ulinzi na kuhakikisha wanatibiwa bure, sera ambayo anasema kuwa licha ya kuwa serikali inasema wazee watibiwe bure bado imeendelea kuwa ni hadithi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles