29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana Mwanza kuwezeshwa ujuzi kukabiliana na changamoto ya ajira

Na Clara Matimo, Mwanza

KATIKA jitihada za kukabiliana na tatizo la ajira jijini Mwanza, Shirika lisilo la Serikali la Teen’s Corridor Organization limeamua kuwawezesha vijana ujuzi wa kuchora, kutengeneza bidhaa za urembo, elimu ya afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia ili kuwainua kiuchumi na kuwawezesha kupata ujuzi waweze kuanzisha biashara na kujiajiri.

Baadhi ya vijana wanaotarajia kunufaika na mradi wa Ujuzi ni Mchongo(waliosimama) wakiwa na baadhi ya viongozi wa Shirika la Teens Corridor Organization, wa kwanza kutoka kulia ni Mkufunzi wa Shirika hilo Thomas Gabriel, Mkurugenzi Sophia Nshushi na Mwenyekiti wa Bodi, Esther Massawe, wa kwanza kushoto ni Emiliana Hangi kutoka Nyanza Development Organization.

Shirika hilo litawezesha ujuzi huo kupitia mradi wake wa miezi mitatu uliopewa jina la ‘Ujuzi ni Mchongo’ ambao unawalenga vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 19, uliozinduliwa Novemba 11, 2023 katika ofisi za shirika hilo zilizopo Kawekamo B wilayani Ilemela, Mwanza.

Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Mkurugenzi wa shirika hilo, Sophia Nshushi, amesema mradi huo utawasaidia vijana kujifunza uchoraji bila malipo na kupata elimu ya masuala ya afya ya uzazi na ukatili wa kijinsia huku wakiwatafutia masoko ya bidhaa watakazotengeneza.

“Tumebaini Mwanza kuna changamoto kubwa ya ajira kwa vijana hivyo ujuzi huu utawasiadia kujiajiri tunaomba tushirikiane na jamii pamoja na familia zao kuwawezesha vijana hawa ili tufanikishe tulichotarajia kufanya.

“Tunatoa wito kwa serikali iangalie namna ya kuturahisishia kufika mashuleni kuwafikia watoto kusiwe na mlolongo mrefu tunapohitaji kutoa elimu hii kwa vijana, vilevile, mashirika makubwa yatuunge mkono na kutusapoti kwa kuchangia chochote,” amesema Mkurugenzi huyo.

Mkufunzi wa elimu ya uchoraji, Thomas Gabriel, amesema alianza kuchora akiwa na umri wa miaka saba kwa sababu ni kitu alichokipenda na anafurahia kukifanya mpaka sasa kwani kinamsaidia kupata kipato kwa kuuza picha, huku akisisitiza kwamba anapenda kupata vijana wengi watakaonufaika na ujuzi huo.

Mmoja wa vijana ambao wameanza mafunzo ya uchoraji, Averina James, amesema anapenda kuchora kwa sababu ni fani ambayo mchoraji anaelezea hisia zake, hivyo anaamini baada ya miezi mitatu ya mradi huo atapata ujuzi na kuitendea kazi Sanaa ya uchoraji ambayo anaipenda sana.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kawekamo B kata ya Kawekamo, Moshi Malima, akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo na kutoa ujumbe wa serikali, amesema Serikali ya mtaa huo itawaunga mkono kufanikisha mafunzo hayo huku akiwataka vijana kuzingatia maadili na kutii sheria za mtaa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles