27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

Vijana JKT waliojenga ukuta wa Mererani waitwa kwa ajira

TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

VIJANA 2,333 waliokuwa wanajitolea katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kujenga ukuta wa Mirerani, wametakiwa kuripoti kambi ya Mgulani, Dar es Salaam ili wapatiwe ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, alisema wito huo ni kutekeleza ahadi ya Rais Dk. John Magufuli kuwa watapatiwa ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Alisema vijana walioitwa ni wale wa Operesheni Kikwete na Operesheni Magufuli ambao walishiriki ujenzi wa ukuta wa Mirerani.

“Nawatangazia vijana ambao bado wanajitolea JKT na waliomaliza mikataba yao waripoti katika kambi ya jeshi ya Mgulani waweze kuandikishwa,” alisema Jenerali Mabeyo.

Alisema vijana hao wanatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti walivyotunukiwa baada ya kumaliza ujenzi wa ukuta wa Mirerani na vyeti vya kumaliza mkataba wa kujitolea jeshini kwa waliomaliza mikataba yao.

Aidha Jenerali Mabeyo aliwataka vijana wanaojiunga na JKT kuondoa matumaini ya kupata ajira jeshini kwani lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uzalendo na kujitambua kuwa ni Watanzania.

“Dhamira ya mafunzo hayo ni kujifunza stadi mbalimbali za kazi zitakazowawezesha kujiendesha kimaisha na kujitegemea na si kupata ajira moja kwa moja jeshini,” alisema Jenerali Mabeyo.

Aliongeza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine huelekezwa kuchukua vijana waliomaliza JKT na si lazima wanapomaliza mafunzo waajiriwe.

“Vijana hawa walikuwa wanawasiliana na viongozi mbalimbali wakidhani ahadi ya Rais Magufuli ni hewa, hii imeleta usumbufu, hasa kwa viongozi wa serikalini na jeshini,” alisema Jenerali Mabeyo.

Aidha aliwataka wazingatie maadili waliyofundishwa na kuacha kutumia lugha zisizostahili.

“Tuliambiwa kuwa kama kuna ajira kidogo basi tuchukue vijana wanaokidhi mahitaji kwa hofu ya watakaobaki kujiingiza katika vitendo viovu, lakini sisi tunasema hapana kwa kuwa lengo si hilo la ajira,” alisema Jenerali Mabeyo.

Alisema wamefuatilia rekodi za uhalifu na tangu kuanzishwa kwa JKT, hakuna tukio baya lililofanywa na vijana waliotoka katika mafunzo hayo.

Wakati huo huo, Jenerali Mabeyo alisema Amiri Jeshi Mkuu, Rais Magufuli amemteua Brigedia Jenerali Charles Mbuge kuwa Mkuu wa JKT.

Mbuge anachukua nafasi Meja Jenerali Martin Busungu ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Akiba.

Awali Aprili13, Rais Magufuli alimpandisha cheo Brigedia Jenerali Mbuge kutoka kuwa Luteni Kanali na kuwa Brigedia Jenerali.

Dk. Magufuli alimpandisha cheo hicho Brigedia Jenerali Mbuge baada ya kufurahishwa na utendaji wake wa kazi katika kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali ikiwamo ujenzi wa ukuta wa Mirerani.

“Ninawapongeza maofisa walioshiriki kukamilisha mradi huu na Kanali Mbuge alisimamia ujenzi wa majengo mbalimbali ya Serikali pamoja na ukuta wa Mirerani, hivyo kuanzia leo atakuwa Brigedia Jerenali, sitaki kuchelewa, hivyo ninataka CDF ukafanye utaratibu wa vile vinavyotakiwa kuwekwa kwenye mabega awekewe,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles