30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana epukeni starehe kukwepa janga wazee wa mitaani

Na HASSAN DAUDI

‘UJANA ni maji ya moto’. Nimeanza na msemo huo pamoja na kwamba ipo mingi inayosisitiza kuwa ni changamoto kubwa kwa binadamu kuvuka umri huo. Ni kipindi chenye vishawishi vingi. Ni wakati ambao kila jambo unalitamani na unataka kujaribu.

Huenda tutakubaliana kwamba ni katika umri huo ndipo vijana walio wengi hujikuta wakishindwa kuepuka matumizi ya dawa za kulevya, sigara, pombe, uzinzi na mambo mengine ambayo kwao ni sehemu ya starehe.

Huku chanzo kikubwa kikiwa ni makundi, kwa maana ya marafiki, ni kwa mazingira hayo basi, haishangazi kuona wengine wakiacha masomo na kujikita katika shughuli za vijiweni, ambazo hakika nyingi huwa na matokeo hasi ndani ya jamii, nikitolea mfano wizi.

Hata hivyo, hakuna ubishi kuwa kuna vijana wengi hujutia maisha ya starehe wanapofikia uzeeni. Hoja hapa haitofautiani na kile alichokisema mwandishi wa vitabu, Nhat Hanh, alipoonya: “Chochote unachoweza kukifanya, hakikisha unakifanya leo ili uzee wako uwe mtamu.”

Naye msomi mwingine aitwaye Fred Astaire aligongelea msumari katika kauli hiyo akisema: “Hakuna haja ya kuhofia uzee ikiwa yalikuwapo maandalizi wakati wa ujana.”  Unachoweza kujifunza hapo ni kwamba huwezi kuepuka uzee lakini utaufurahia tu endapo utakuwa umejipanga kuupokea, maandalizi ambayo unapaswa kuyafanya ukiwa kijana.

Nikijenga hoja kwa kauli ya msomi huyo, hiyo inamaanisha kuwa kijana wa leo ni mzee wa kesho, hivyo suala la msingi ni maandalizi tu. Je, ni kwa kiasi gani kijana wa leo umejipanga kukabiliana na changamoto za uzee? 

Kuliweka hilo katika muktadha, hivi sasa kumekuwapo na janga la wazee wa mitaani, ingawa bado halijaonekana kuwa tatizo kubwa kama ilivyo kwa watoto tuliozoea kuwaona katikati ya miji wakizunguka kuomba, kuosha magari kwa malipo, wakiwa hawako chini ya uangalizi makini wa wazazi.

Nikiwa silengi kuwakebehi katika andiko hili, nikiamini wanapaswa kusaidiwa pia kama watoto wa mitaani, wasiwasi wangu ni kwamba huenda walio wengi kati ya wazee hao waliponzwa na anasa za ujana.

Licha ya kwamba hakuna utafiti rasmi, sina shaka kuwa ukihoji 10, sita kati yao watakupa simulizi za kusisimua juu ya maisha yao. Watakwambia namna maisha yao ya ujana yalivyokwenda sambamba na matukio yaliyoiharibu leo yao huku uzeeni.

Huenda hapo utawakuta ‘vijana wa zamani’ waliotumia sehemu kubwa ya maisha yao kuonesha wenzao ufahari wa mavazi ya gharama, kukesha katika kumbi za starehe, kubadilisha wasichana kila uchwao.  

Lugha ya picha inayoweza kulifafanua hilo ni kwamba walisahau kwamba kama ilivyo kwa jua kuchomoza upande wa Magharibi kila ifikapo asubuhi na kisa kutokomea Mashariki jioni, basi hata leo yao ilikuwa ujana na kesho yao ingekuwa uzee. 

Hebu nikuulize kijana wa leo, ambaye asilimia zaidi ya 50 ya saa 24 umekuwa ukizitumia mitandaoni kutazama na kubishana juu ya maisha ya mastaa, hiyo inajenga kwa kiasi gani kesho yako, nikimaanisha uzeeni?

Ukiwa ndiyo kwanza una umri wa miaka 25 au chini ya hapo, umeshaanza kujipanga kuwa mzee wa mitaani, yaani kuishi kwa kuomba au kuokota makopo na kwenda kuuza kama wafanyavyo wengine kwa sasa?

Binafsi nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa simulizi za waliofanikiwa, akiwamo mfanyabiashara maarufu nchini China na ulimwenguni kote, Jack Ma. mara nyingi watu wa aina hiyo watakwambia siri ya kufanikiwa uzeeni ni kuyatoa sadaka  maisha ya ujana.

Kama nilivyoeleza hapo juu, maisha ya ujana yana vishawishi vingi, hivyo utakuwa umefanikiwa uzeeni endapo tu utafanikiwa kupambana na kisha kushinda vita hiyo. Kwa lugha nyepesi, uwe tayari kuufanya ujana uwe mchungu kwa masilahi yako ya uzeeni.

Wakati unaupa kisogo ujana, wenzako wengi watakushangaa kwa kuwa aghalabu utakuwa tofauti nao. Huenda kati ya washikaji zako watano, ni wewe tu ambaye hutakuwa mlevi, mvutaji sigara/bangi au mzinzi.

Kwa upande wako, hiyo isikufanye uachane na msimamo wako kwamba kiasi cha fedha ambacho labda ungetumia katika starehe hizo utakiwekeza katika mambo ya msingi, zikiwamo biashara ndogondogo.

Kuhitimisha ujumbe wangu huu kwa kijana wa leo, nikuache na kisa cha mmoja kati ya washahiri wa lugha ya Kiarabu aliyekuwa akilalamika kuwa anatamani siku moja awe kijana kwa mara nyingine ili ausimulie namna uzee unavyompa tabu.

Ukiwa kijana, kinachopaswa kuwa akilini mwako wakati wote ni kwamba hiki ni kipindi ambacho una nguvu na uwezo wa kufikiria kuliko kingine chochote kilichobaki katika safari yako hapa duniani. Unaweza kusema kwamba wakati mzuri wa kuuandaa uzee wako ni sasa. Jipange kijana…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles