‘Vijana 800,000 hukosa ajira kila mwaka’

0
960

Eliya Mbonea -Arusha

VIJANA wametakiwa kuongeza ujuzi na kuwa wajasiriamali ili waweze kujiajiri na kuajiri wengine kutokana na vijana 800,000 kukosa ajira kila mwaka nchini.

Kauli hiyo imetolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Asasi ya Anza, inayojishughulisha na ufundishaji vijana masuala ya ujasiriamali na kuboresha mawazo ya biashara, Joshua Silayo.

Changamoto hiyo imeisukuma Anza na Asasi ya Climate Launch pad kuendesha shindano kwa vijana 10 ili kupata mawazo bora ya biashara zinazolenga kutunza mazingira yatakayoshindanishwa kidunia.

Akizungumza wakati wa kutafuta washindi watatu kati ya 10 walioshiriki mafunzo ya masoko, fedha na wateja kwa miezi miwili,  Silayo aliyataja malengo yao kuwa ni kukuza ajira tano hadi 10 kwa kila biashara.

“Tunalenga kukuza mapato ya vijana ili wakidhi mahitaji yao na jamii inayowazunguka, kuendeleza elimu kwa vijana wengine na kukuza jamii ya kijasiriamali kwani kila mwaka vijana 800,000 hukosa ajira.

“Mwaka jana katika mashindano kama haya kidunia, tulipata biashara iliyoshinda Euro 2,500 kwa wazo la biashara kijani. Vijana washiriki mashidano haya ili kukuza biashara zao,” alisema Silayo.

Alisema washindi watatu waliopatikana watakwenda kushiriki mashindano ya kidunia nchini Amsterdam na kwamba wazo la biashara litakaloshinda litapata Euro 10,000, wa pili Euro 5,000 na wa tatu Euro 2,500.

Kwa upande wake jaji kiongozi wa shindano hilo ambaye pia ni mchumi na mtafiti, Mapolu John, alisema wameangalia ujuzi wa vijana hao na wanautumia vipi katika maisha ya kila siku, hasa biashara zinazotunza mazingira.

“Vijana wamefanya vizuri, lakini walio wengi wana elimu ya kitabuni na wanakosa utafiti mkubwa katika masuala ya takwimu, wanalinganisha takwimu zilizopitwa na wakati.

“Hawajui masoko, baadhi wameshindwa kuoanisha biashara anayofanya, masoko, sera na sheria za nchi,” alisema Mapolu.

Akifafanua kuhusu suala la mitaala mashuleni, Mapolu alisema ni wakati mwafaka kwa mitaala ya shule na vyuo vya Serikali na binafsi waanze kufundisha ujasiriamali kwani una kitu kikubwa.

“Vijana wengi hawana ajira na kuwasomesha shule ya vyeti inakuwa haina mpapaso mkubwa kwenye uchumi.

 “Lakini mitaala ikianza kubadilika na wanafunzi kufundishwa namna ya biashara, kuandika miradi, kutunza vitabu, kulipa kodi na faida zake, inaweza kuwa ukurasa mpya katika eneo la ajira,” alisema.

Naye mgeni rasmi katika shindano hilo, Meneja wa Sido Mkoa wa Arusha, Nina Nchimbi, aliwapongeza Anza kwa kubuni programu ya kuwatafuta vijana wenye mawazo ya biashara zinazotunza mazingira.

“Vijana waliopo vyuoni, waliomaliza, waliopo mitaani wakizunguka na bahasha waangalie au wachukue fursa za changamoto zinazowazunguka,” alisema Nchimbi.

Mshindi wa kwanza wa shindano hilo, Frolence Zakara kutoka Twende Initiative, aliibuka mshindi kutokana na wazo la mradi wa masuala ya hedhi kwa wanawake na mazingira.

“Shindano lilikuwa gumu, kila mtu amefanya vizuri, sisi tumewazidi wengine, pengine kutokana na wazo letu kuwa muhimu katika jamii, hasa wanawake.

“Hedhi kwa wanawake imewafanya watumie fedha nyingi, jukumu letu tunajaribu kupunguza gharama ili watumie fedha hizo kulisha watoto na kufanya kazi za majumbani badala ya kuishia kwenye vifaa vya hedhi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here