33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana 51,917 wanufaika na elimu ya afya ya uzazi wilaya ya Shinyanga

Na Damian Masyenene, Shinyanga

Jumla ya vijana 51,917 wamenufaika na elimu ya afya ya uzazi na huduma za kisasa za afya ya uzazi (Uzazi wa mpango) wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, ambayo imekuwa msaada kwao katika kubadili fikra juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na kukomesha ukatili na unyanyasaji kwa wanawake.

Vijana hao wamenufaika na elimu hiyo kupitia mradi wa USAID TULONGE AFYA unaotekelezwa na Shirika la Thubutu Africa Initiatives katika halmashauri mbili za Wilaya ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga, ambao ni wa kike na kiume kuanzia miaka 15 – 24 ambao siyo wanafunzi wakiwemo ambao wameshapata watoto wakiwa nyumbani kwa wazazi wao na wale ambao bado hawajapata watoto.

Kwa mujibu wa Meneja Miradi wa Shirika la Thubutu Africa Initiative, Paschalia Mbugani, kwa mwaka 2020, jumla ya wasichana 18,028 na wavulana 18,958 walinufaika na elimu hiyo katika halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, huku vijana wa kiume 6,956 na wa kike 7,975 wakinufaika katika Manispaa ya Shinyanga kwa mwaka huo.

Vile vile, kwa mwaka 2019, Vijana wa kiume 6,844 na wasichana 3,331 katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakinufaika na wavulana 1,397 na wasichana 3,323 katika Manispaa ya Shinyanga wakinufaika.

Paschalia ameeleza kuwa kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo matamasha ya kijamii na majadiliano katika vikundi wanawasaidia vijana kubadilisha fikra kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango, kujikinga na mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya ngono, matumizi sahihi ya Kondomu na kufuta dhana kwamba njia za uzazi wa mpango ni kwa wanawake walioolewa peke yake.

“Vijana wana matamanio ya kupata elimu lakini hawajui wanaipataje, kutokana na tamaduni hawawezi kumuuliza mzazi na hospitalini anaogopa, kwahiyo tunaweza kusema kwamba huenda elimu hii ilichelewa… tunashukuru kwamba mwitikio ni mkubwa hasa kwa mabinti ambao tayari wameshaanza kupata watoto.

“Wanauliza vitu vingi kwa sababu hawapati nafasi nzuri ya kuuliza mambo mengi kutokana na uchache wa rasilimali watu katika vituo vingi vya kutolea huduma za afya na hasa huduma rafiki kwa vijana hivyo kukosa taarifa sahihi.

“Vijana wengi hawana taarifa sahihi juu ya mabadiliko ya kimwili yanayotokea katika kipindi cha balehe na hawajui jinsi ya kukabiliana na changamoto ya mihemko ya kimwili, kutokuwa na maamuzi kwenye tendo la ndoa (hasa wasichana) huku wavulana wengi wakifikiri kwamba jukumu la kujikinga na mimba ni msichana peke yake, ndio inapelekea wasichana wengi kupata ujauzito usiotarajiwa,” amesema.

Akibainisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo vijana wakati wa kupata huduma za kisasa za afya ya uzazi ni upungufu wa vituo vya huduma rafiki kwa vijana na vilivyopo havina wataalam waliowezeshwa ipasavyo kuzungumza na vijana, pia mahitaji ni makubwa kwa vijana lakini huduma na wataalam havikidhi mahitaji.

Akizungumza MtanzaniaDigital ofisini kwake juu ya mimba kwa wanafunzi na ndoa za utotoni wilayani Shinyanga, Mkuu wa Wilaya hiyo, Jasinta Mboneko alieleza kuwa kila anapopata nafasi ya kutembelea shule mbalimbali amekuwa akizungumza na wanafunzi namna ya kuepuka vishawishi na kutojiingiza kwenye mambo yanayoharibu utu wao.

Amebainisha kuwa wanaendelea kutoa elimu kwenye maeneo yote kupunguza tatizo hilo na watazidi kufuatilia, huku akiwaagiza walimu wakuu, maofisa elimu na watendaji wa kata kujipanga kuhakikisha wanadhibiti mimba shuleni.

“Nitaanza ziara yangu kwenye shule kuhakikisha kwamba yale maagizo tuliyoyatoa kuhusu tatizo hili yametekelezeka, Wananchi waendelee kutoa taarifa za matukio haya na kusaidia kutoa ushahidi. Pia tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi, lakini pia watu wa afya kuendelea kutoa elimu ili tuwasaidie watoto kufikia ndoto zao na tukomeshe zile mila potofu za kuozesha watoto wa kike katika umri mdogo,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles