27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana 46 kupata mafunzo ya stadi za kazi

Na Mwandishi wetu-Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema zaidi ya vijana 46,000 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya uanagenzi kupitia taasisi ya Don Bosco Net Tanzania katika mwaka huu wa fedha.

Majaliwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mafunzo na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO), katika viwanja vya Donbosco jijini Dodoma.

 “Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli, imeandaa programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kuanzia wahitimu wa darasa la saba hadi vyuo vikuu.”

Alisema katika mafunzo yalianza 2017 na 2018 walihitimu vijana 32,786.

Majaliwa alisema katika awamu ya pili ya mafunzo hayo iliyozinduliwa jana, yanahusisha vijana 5,875 kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 ya ILO.

Alisema licha ya mafanikio yaliyoonekana katika sekta ya Kazi na Ajira kwa miaka 100 iliyopita, suala la ukosefu wa ajira kwa vijana ni miongoni mwa changamoto inayoikabili dunia, hivyo linahitaji kuwekewa mikakati endelevu kwa miaka 100 ijayo. 

Alisema miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia ukosefu wa ajira kwa vijana ni vijana kutokuwa na ujuzi sahihi wa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema hadi kufikia Juni 2019 vijana 36,726 wamefaidika na programu ya kukuza ujuzi inayogharamiwa na Serikali wa asilimia 100.

Alisema kati yao vijana 6,455 walinufaika na mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali zikiwemo za ushonaji na nguo, useremara, uashi, terazo, uchongaji wa vipuri, ufundi magari, umeme na utengenezaji wa viatu vya ngozi.

Alisema mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo yametolewa kwa vijana 10,443 katika fani za uashi, useremara, ufundi wa magari, upishi na huduma za hoteli.

Jenista alisema kwa upande wa mafunzo ya kilimo cha kisasa vijana 18,800 walinufaika na mafunzo hayo huku vijana wengine 1,028 walipatiwa mafunzo ya vitendo pahala pa kazi.

Mratibu wa Miradi wa Taasisi ya Donbosco Tanzania, Rosemary Terry Njoki, alisema programu ya kukuza ujuzi imezingatia kuwawezesha vijana wa miaka kati 17 hadi 35 kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Awali, Mkurugenzi wa ILO Kanda ya Afrika Mashariki, Wellington Chibebe, alisema shirika hilo limedhamiria kupigania haki ya kijamii na haki za binadamu na kazi zinazotambulika kimataifa.

Alisema tangu 1919, ILO ni shirika pekee la Umoja wa Mataifa lenye mfumo wa utatu unaowaleta pamoja wafanyakazi, waajiri na Serikali katika nchi 187 wanachama wa shirika hilo katika kuweka viwango vya masuala ya kazi, kukuza sera na kupanga programu za zinazochagiza kazi zenye staha kwa watu wa jinsia zote.

 “Maadhimisho ya karne moja ya ILO ni fursa nzuri ya kujitathimini wapi lilipotoka, kusheherekea historia na mafanikio yake na pia kutafakari siku zijazo. Pia ni jukwaa la kipekee la kuihakikishia dunia umuhimu wa jukumu na mamlaka yake ya kutetea haki ya kijamii na ajenda ya kazi zenye staha”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles