Vigogo wawili Lindi waingia 18 za Majaliwa

0
520

Mwandishi wetu-Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama, Warioba Gunze na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, Mhandisi Mndeme, kufika ofisini kwake Dar es Salaam leo asubuhi na taarifa ya skimu ya umwagiliaji wa Narunyu.

 Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati alipoenda kukagua skimu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa tangu mwaka juzi. 

Alichukua uamuzi huo baada ya kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko ya wanajumuiya ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi huo na alipotaka maelezo ya wataalamu, hakuna hata mmoja ambaye alikuwepo.

“Nilitaraji niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Ofisa Umwagiliaji wa Wilaya na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda.

“Nimeagiza wanikute Uwanja wa Ndege Lindi au Dar es Salaam na kesho asubuhi (leo) waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya Sh milioni 240 ziko wapi.

 “Walipaswa niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana (juzi) kwamba nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi (jana) walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa nitachukua maamuzi mengine,” alisema.

 Akielezea umuhimu wa mradi huo wakati akizungumza na baadhi ya wanaushirika waliokuwepo, Majaliwa alisema ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote.

“Huu ni mradi wa kuringia. Mradi huu unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi, tena mengi tu,” alisema Majaliwa.

 Alisema kutokana na umuhimu wa mradi huo, hivi sasa wangekuwa wanazalisha mazao ya kila aina.

 “Hapa ni mahali pa kuzalisha mazao mengi, leo unalima mahindi, ukivuna unapanda matikiti, ukitoa unapanda nyanya. Sasa nitapasimamia mwenyewe,” alisisitiza.

 Majaliwa aliwataka  wanaushirika wanaounda jumuiya ya umwagiliaji wahakikishe kila mmoja anatambua eneo lake na mara kazi ikianza wawe tayari kuanza kilimo.

“Huu mradi una manufaa kwa watu wa Ruo, Mahumbika hadi Mnazi Mmoja. Lazima tuung’ang’anie kwa sababu kuna idadi kubwa ya wakulima wanaoutegemea. Huu mradi lazima tuuvalie njuga,” alisema.

 Majaliwa alipofika Uwanja wa Ndege wa Lindi, maofisa hao walikuwa hawajafika na simu zao hazikupatikana, na akaagiza wafike Dar es Salaam leo asubuhi. 

 Mapema Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika mafaili aliyoyapitia ofisini kwake, alibaini kwamba mradi huo ulitengewa Sh milioni 788, mkandarasi wa kwanza Chest Investments Company alilipwa Sh milioni 121, lakini akashindwa kazi.

 “Mkandarasi wa pili ambaye ni D & L naye alilipwa zaidi ya Sh milioni 400, naye pia akashindwa kazi na kuondoka. Kwenye ripoti inaonyesha zilibakia Sh milioni 249,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here