26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo watano Vodacom kizimbani kwa uhujumu uchumi

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

VIGOGO watano wa Kampuni ya Simu ya mkononi, Vodacom Tanzania PLC akiwamo Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Hisham Hendi, wamefikishwa mahakamani kwa uhujumu uchumi ikiwamo kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni tano mali ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali  Simon Wankyo, akisaidiana na Wakili Jackline Nyantori, walidai kwa nyakati tofauti kwamba washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 10.

Mbali na Hisham, washatakiwa wengine ni Mkuu wa Kitengo cha Mapato, Joseph Nderitu, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Olaf Mumburi, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo, Joseph Muhere, Meneja Uhasibu, Ibrahimu Bonzo na Kampuni ya Vodacom Tanzania.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Biashara wa Inventure Mobile Tanzania LTD (Tala Tanzania) Ahmed Ngassa, Mtaalamu wa IT, Brian Lusiola na Kampuni ya Tala Tanzania.

Nyantor akisoma mashtaka, alidai shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa  Hisham, Nderitu, Mumburi, Muhere na Bonzo ambao wanadaiwa kati ya Januari mosi mwaka 2018 na Machi 11 mwaka huu katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam walijiingiza katika genge la uhalifu na kuisababishia TCRA hasara ya Sh 5,892,513,000.

Alidai mshtakiwa Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Tala Tanzania wanakabiliwa na mashtaka saba ya kuingiza vifaa vya mawasiliano vya  elekroniki kati ya Januari Mosi mwaka 2018 na Desemba 31 mwaka huo maeneo ya jengo la Tanzanite Park bila kibali cha TCRA.

Wanadaiwa kufunga vifaa hivyo bila kuwa na leseni na kati ya Aprili 17 mwaka 2018 na Machi 11 mwaka huu, washtakiwa kinyume cha sheria walipokea na kupiga simu za nje bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Wankyo alidai washtakiwa hao kwa nia ya kukwepa gharama za kulipia kwa kupokea na kupiga simu za kimataifa, walisimika mitambo ya mawasiliano kuzuia simu za nje zinaoingia na wanadaiwa kutumia vifaa ambavyo havijaidhinishwa na TCRA.

Shtaka la saba washtakiwa hao wanadaiwa kutumia namba 813 ya Vodacom Tanzania PLC bila kupata baraka za TCRA na shtaka la nane wanadaiwa kusababisha hasara kwa mamlaka hiyo ya Sh 642,276,000.

Nyantor alidai shtaka la tisa linawakabili washtakiwa Hisham, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Vodacom Tanzania PLC ambao kwa tarehe tofauti kati ya Aprili 17 mwaka 2018 na Machi 11 mwaka huu, kwa pamoja walitumia namba 813 ya Vodacom bila kibali cha TCRA.

Katika shtaka la 10  washtakiwa hao wanadaiwa kwa kufanya hivyo walisababisha hasara ya Sh 5,250,237,000 kwa TCRA.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, upelelezi haujakamilika na kesi iliahirishwa hadi Aprili 17 mwaka huu kwa kutajwa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mashtaka  (DPP), Biswalo Mganga alisema kesi hiyo si ya  siasa, washtakiwa ni wahalifu kama walivyokuwa wahalifu wengine.

“Washitakiwa walijiingiza katika genge la uhalifu, najua mengi yatazungumzwa lakini hayo yatakayozungumzwa mitaani hatutayajali.

“Najua watayaingiza katika siasa, mimi sitajali, uhalifu ni uhalifu, makampuni mengine yoyote yatakayofanya uhalifu hatutayafumbia macho,”alisema Mganga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles