29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO WATANO KNCU KIZIMBANI

Na SAFINA SARWATT -MOSHI


WALIOKUWA viongozi wa Kiwanda cha kukoboa kahawa mjini Moshi cha Tanganyika Coffee Curing Company Limited (TCCCo), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro wakikabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi.

Watuhumiwa hao watano walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Pamela Mazengo.

Hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda hicho, Meynard Swai, aliyekuwa Meneja Mkuu, Andrew Kleruu, Mwenyekiti wao, Aloyce Kitau, Makamu wake, Hatibu Mwanga na Meneja Mkuu wa sasa wa KNCU, Honest Temba.

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama hiyo, Jackline Nyantory, aliwasomea mashtaka washtakiwa wawili, Swai na Kleruu, kwamba katika tarehe tofauti kati ya Januari mwaka 2014 na Desemba mwaka 2015, walitumia madaraka yao vibaya na kununua mtambo mbovu wa kukobolea kahawa kutoka Kampuni ya Brazafric Limited ya Nairobi nchini Kenya.

Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka huyo, washtakiwa hao walisababisha hasara ya Sh bilioni 1.6 kiwandani hapo.

Alidai  mashtaka ya watuhumiwa hao ni ya uhujumu uchumi na   hawawezi kuruhusiwa kupata dhamana.

Hakimu Mazengo alikubaliana na upande wa mashtaka na kuamuru washtakiwa wapelekwe rumande hadi Julai 24, mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena.

Wakati huo huo, washtakiwa watatu waliobaki  walisomewa mashtaka yao na Mwendesha Mashtaka wa Mahakama, Abdallah Chavula mbele ya hakimu huyo.

Chavula alidai katika nyakati tofauti, kati ya Julai mwaka 2014 na Novemba mwaka 2017, washtakiwa hao walikula njama na kutumia vibaya madaraka yao na kuilipa kampuni moja ya Ocean Link Shipping Service Limited Sh bilioni 2.9 isivyo halali.

Kama alivyosema mwendesha mashtaka mwenzake, Chavula naye alidai mashtaka ya uhujumu uchumi yanayowakabili washtakiwa hayana dhamana, hivyo wanastahili kuendelea kuwa mahabusu hadi shauri lao litakapomalizika.

Hakimu Mazengo alikubaliana na upande wa mashtaka na kuamuru washtakiwa wapelekwe rumande hadi Julai 24, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles