28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

VIGOGO WANAOSHIKILIA HATIMA YA WENGER EMIRATES

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


NI wazi kuwa mashabiki wa timu ya Arsenal wamekata shauri kuhusu kocha wao, Arsene Wenger na wanachokisubiri sasa ni kuona viongozi wa klabu hiyo wanachukua hatua kali  ya kumfukuza kocha huyo baada ya kushindwa kuisaidia timu hiyo kunyakuwa makombe kwa muda mrefu.

Hatima ya Wenger kuendelea kuifundisha timu hiyo kwa sasa ipo shakani hasa baada ya kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Bayern Munich katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hatua ya 16 bora uliochezwa Uwanja wa Allianz Arena.

Hata hivyo, Wenger amewaeleza mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu ujao utakuwa wa mafanikio kwake, bila ya kueleza iwapo ataendelea kuifundisha timu hiyo au ataondoka mkataba wake utakapomalizika hivi karibuni.

Wenger (67) ambaye ameifundisha Arsenal kwa miaka 21, mkataba wake unatarajia kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Hata hivyo, bado hatima yake haijafahamika katika klabu hiyo kutokana na mwenendo wa timu hiyo kwa sasa kuwa mbaya zaidi.

Lakini Wenger amesisitiza kwamba hatajiuzulu bila kuthibitisha kama atakuwapo katika klabu hiyo au nyingine msimu ujao.

“Bila kujali kilichotokea, nitafanya vizuri msimu ujao nikiwa hapa Arsenal au klabu nyingine.

 “Nimekuwa hapa kwa miaka 20, katika maisha ni muhimu kufanya jambo jema nafahamu nipo katika kazi inayokusanya maoni ya wengi hivyo natakiwa kukubaliana nayo,” anasema Wenger.

Wenger alisema hataki kujadili kuhusu hatima yake katika klabu hiyo kwa kuona jambo hilo si muhimu zaidi ya klabu hiyo.

“Tunatakiwa kujikita katika matatizo ya kweli yanayotukabili ndani ya klabu hasa aina ya uchezaji wetu, lakini si hatima yangu,” anasema Wenger.

Lakini wapo vigogo katika klabu hiyo ambao uamuzi wao unaweza kuwa wa faraja au huzuni kwa Wenger kutokana na umuhimu na nguvu waliyonayo ndani ya klabu hiyo.

Miongoni mwao ni Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Stan Kroenke (69), raia wa Marekani ambaye anaongoza kumiliki asilimia 67 za hisa katika klabu hiyo.

Tajiri huyo ana nguvu kubwa ya  ushawishi ndani ya Arsenal hasa linapokuja suala la kumfukuza Wenger na kuajiri kocha mwingine.

Kwa mujibu wa jariba la Forbes, Kroenke ana utajiri wa dola bilioni saba unaotokana na shughuli mbalimbali zinazomwingizia kipato.

 “Nahisi kuwa na nguvu ya kutosha na nafikiri Wenger amekuwa akifanya kazi yake kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwetu, hajawahi kutuangusha, tunafurahi kuwa naye pia tunafurahishwa na namna ya timu inavyocheza katika michuano inayoshiriki,” aliwahi kusema Kroenke wakati akihojiwa na mtandao wa Daily Telegraph mwaka 2013.

Kigogo mwingine ni mtoto wa Kroenke ambaye anaitwa Josh Kroenke (36), mara ya kwanza kuwa katika bodi ya klabu hiyo ni mwaka 2013.

Lakini Mrusi, Alisher Usmanov (63) ni kigogo mwingine ambaye tangu mwaka jana amefanikiwa kumiliki hisa za asilimia 30 baada ya kuongeza kutoka kwa Farhad Moshiri na kuwa wa pili katika umiliki wa hisa ndani ya klabu hiyo.

Moshiri aliuza hisa zake ili aweze kununua hisa nyingi katika klabu ya Everton ambayo kwa sasa ndio mmiliki.

Mwaka 2016, jarida la Forbes liliwahi kumtaja kuwa miongoni mwa matajiri 58 wenye ushawishi na nguvu kubwa duniani akiwa na utajili wa dola milioni 15.

Mkurugenzi Mkuu wa klabu hiyo, Ivan Gazidis (52), ni raia wa Ugiriki na Afrika Kusini ambaye amekuwa katika cheo hicho tangu mwaka 2009.

Oktoba mwaka jana aliingiza fedha ya ziada kiasi cha euro milioni 1 kwa mwaka licha ya klabu hiyo kushindwa kunyakuwa kombe lolote.

Kigogo mwingine ni Mwenyekiti wa klabu hiyo, Chips Keswick, (77), ambaye anafanya kazi benki ya Hambros, DeBeers na Benki ya England iliyopo jijini London. 

Keswick, amekuwa kiongozi wa klabu hiyo tangu mwaka 2013 akirithi mikoba ya Peter Hill-Wood.

Keswick mara kadhaa humpongeza Wenger kutokana na kuimarisha klabu hiyo hadi kuwa ya ushindani barani Ulaya.

Mtendaji mwingine ni Lord Harris (74), kwa sasa amefikisha miaka 12 tangu awe miongoni mwa wajumbe wa bodi ya klabu hiyo.

Katika mahojiano yake na mtandao wa Sportsmail mwaka jana, Lord Harris, alisisitiza kuwa klabu ya Arsenal ina kila sababu ya kushindana kuwa kileleni mwa klabu kubwa Ulaya.

 “Tatizo la fedha lilikuwapo wakati tunahamia Uwanja wa Emirates lakini kwa sasa hali ni shwari, tunaweza kuingia sokoni na kununua mchezaji yeyote duniani, tuna kiasi cha pauni milioni 200 benki kwa ajili ya usajili wa wachezaji.

“Unaweza kusema kuwa Arsenal hatuna fedha na Wenger akawa hana wasiwasi au unaweza kumpa pauni milioni 100 ili kusajili lakini anaweza asitumie fedha hizo,” anasema Harris.

Mtendaji mwingine ni Ken Friar (82), ambaye amefanya kazi na klabu hiyo kwa zaidi ya miaka 60 akiwa katika nyadhifa mbalimbali na amekuwa miongoni mwa walioshauri kujengwa Uwanja wa Emirates wakati huo wakitumia Uwanja wa Highbury.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles