25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo walivyotafuna Bandari

1>> Maofisa wafunguka waeleza jinsi ‘Wakubwa’ walivyotumia kampuni za mifukobi, vimemo kupitisha makontena

>> Faili la majina yao latua mikononi mwa Waziri Mkuu, malori yapungua barabarani

Na Waandishi Wetu

VIGOGO na watu wakubwa wenye ushawishi serikalini wakishirikiana na baadhi ya wafanyabiashara wametajwa katika orodha aliyokabidhiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kama wahusika wakuu wa kupitisha kinyemela makontena takribani 2,780 na kukwepa kodi inayokadiriwa kuzidi Sh bilioni 600.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, ofisa mmoja wa ngazi za juu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) ameliambia gazeti hili kuwa ripoti hiyo imeeleza pia jinsi ‘wakubwa’ hao walivyofanikisha kupitisha makontena hayo kwa kutumia kampuni zao za mifukoni na vimemo.

Alisema tayari majina ya vigogo hao yamekabidhiwa kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ambaye tangu ateuliwe kuwa Waziri Mkuu amefanya ziara ya kushitukiza mara mbili Mamlaka ya Bandari (TPA) na kuibua ufisadi huo.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, vigogo hao wengine walikuwa wakituma ‘vimemo’ kwa wakubwa wa bandari ili wawapitishie makontena hayo, mengine yakiwa ni ya kwao, ndugu zao na wapendwa wao.

Ofisa huyo alisema kutokana na nyadhifa za wakubwa hao, ilikuwa ni mawili, ama ukatae ufukuzwe kazi au upitishe uendelee kubaki kazini na kuneemeka.

Alisema kutokana na mtihani huo, wengi wao walilazimika kupitisha makontena hayo kwa lazima ili maisha yaweze kuendelea.

“Tunafanya kazi kwa kasi inayotakiwa, lakini wenzetu, hasa vigogo wakishatoa mizigo sisi ndio tunaopata tabu.

“Lakini wahusika kabisa wenyewe wanajulikana na majina yao yapo na kampuni wanazomiliki zipo na wengine wanatumia makampuni ya mifukoni, Waziri Mkuu tumempa majina yote na kila kitu…lakini tunaohangaishwa ni sisi watu wa chini,” alisema ofisa huyo.

Gazeti hili lilimtafuta kwa njia ya simu Kaimu Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Janeth Luzangi, ambaye alikiri ripoti ya majina ya vigogo hao kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu.

Kwa mujibu wa Luzangi, ripoti hiyo iliwasilishwa juzi ofisini kwa Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mamlaka mbili zinazofanya kazi kwa pamoja, Mamlaka ya Bandari (TPA) na ile ya Mapato (TRA) umebaini kuwako kwa hali ya sintofahamu, huku wafanyakazi wakisema wanafanya kazi kwa staili ya mguu mmoja ndani mwingine nje.

Kwa upande wa Bandari ya Dar es Salaam, baadhi ya wafanyakazi wameonekana wakihaha kuandaa ripoti zinazohusu mwenendo wa upakuaji na utolewaji wa makontena bandarini hapo.

Mmoja wa wafanyakazi wa bandari aliyezungumza na gazeti hili alisema kwa sasa hali ni ya mchakamchaka, huku viongozi pamoja na baadhi ya wafanyakazi wakiwa wametingwa kuandaa ripoti hizo na ufuatiliaji ukiongezeka.

Pamoja na hilo, ofisa mwingine aliliambia gazeti hili kuwa miongoni mwa makontena 2,431 ambayo yamebainika kuwa hayakulipiwa kodi, yapo mengine yaliyouzwa kwa njia ya mnada, huku TRA ikielezwa kuwa ndio wahusika wa hilo.

“Huku sasa ni kazi tu! Watu wanapiga kazi kweli sasa hivi… viongozi wanahaha kuandaa ripoti ya makontena 2,431 ambayo yalitolewa hapa bandarini bila kulipia kodi, hata hivyo miongoni mwa makontena hayo yapo yaliyouzwa kwa njia ya mnada,” alisema ofisa huyo aliyezungumza na MTANZANIA Jumamosi bila kutaja idadi ya makontena yaliyopigwa mnada, akisema ripoti inaandaliwa.

Akizungumzia hilo, Luzangi alisema TPA haihusiki na kupiga mnada makontena, kwamba wenye dhamana ya kufanya hivyo ni TRA.

MTANZANIA Jumamosi limepata taarifa zinazoonyesha kuwa aina nyingine ya wizi iliyokuwa ikitumiwa na vigogo hao ni kudanganya kwamba baadhi ya makontena yanasafirishwa kwenda nje ya nchi.

Hata hivyo, makontena hayo yalikuwa yakibaki na bidhaa zake kuuzwa hapa hapa nchini na hivyo kukwepa kodi.

Taarifa hizi ambazo nyingine ni zile zilizowahi kuripotiwa na vyombo vya habari huko nyuma zimepata nguvu tena baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa kwa mara ya pili kufanya ziara ya kushtukiza TPA, ambapo mara ya kwanza alibaini upotevu wa makontena 349 na mara ya pili 2,431.

Katika ziara yake ya juzi, Waziri Mkuu alisema taarifa za ukaguzi zilizopo zinaonyesha kuanzia Machi hadi Septemba mwaka 2014, makontena hayo yalipita bila kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni Jefang, DICD, PMM na Azam.

Alimuagiza Meneja wa Bandari, Hebel Mhanga, kuhakikisha ndani ya kipindi cha wiki moja anabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka ‘billing system’, badala yake uwekwe mfumo wa malipo wa kielektroniki uitwao e-payment.

Miongoni mwa mifumo aliyoiangalia ni ya upokeaji na utoaji mizigo pamoja na utozaji wa malipo na aliikagua baada ya kupewa taarifa kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.

Majaliwa aliangalia mifumo hiyo wakati akikagua idara mbalimbali za Mamlaka ya Bandari na kuona ukaguzi wa mizigo unavyofanyika kwa kutumia mashine maalumu.

Hata hivyo, Majaliwa alikosoa uamuzi wa bandari kuwasimamisha watumishi 10 kutokana na uzembe wa kukubali kupitisha kinyemela makontena hayo 2,431.

Alisema waliosimamishwa ni watu wadogo, huku wakubwa wakiwa wameachwa. Akisisitiza hilo, alisema hawawezi kukubali kuendelea kuikosesha mapato serikali kwa namna hiyo.

Akiwa kwenye chumba cha scanner mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers, lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Bandari upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ben Usaje, ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha scanner, alisema inapobainika taarifa kama hiyo, inapaswa itumwe kwa wenye bandari kavu ili wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena kuhakikisha mali zilizomo ndizo zilizoandikishwa kwenye manifest.

Katika hatua nyingine, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa tangu serikali ya awamu ya tano ibaini madudu ya ukwepaji wa kodi ya makontena bandarini, msongamano wa malori ya mizigo katika barabara za Mandela na Morogoro umepungua.

Kupungua huko kwa idadi ya makontena bandarani kumejenga hisia kwamba huenda makontena mengi yaliyokuwa yakipitishwa ni yale ya ‘dili’.

Kupitia uchunguzi huo, baadhi ya wakazi wanaotumia barabara hizo wanadai hali hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa foleni ya magari barabarani, ambapo kwa wastani wanatumia dakika 20 hadi nusu saa kufika Mbezi badala ya saa mbili hadi tatu walizokuwa wakitumia awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles