31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo waanza kujisalimisha kwa DPP

Kulwa Mzee, Dar es salaam

WAKATI leo ikiwa ni siku mwisho aliyoitoa Rais Dk. John Magufuli kwa watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha  kuomba msamaha na kurejesha fedha hizo, tayari orodha ya vigogo kadhaa imekwisha mwandikia Mkurugenzi wa Mashataka nchini (DPP) Biswalo Mganga.

Wakati Mganga akikiri kuwapo kwa maombi mengi yaliyokwishawasilishwa kutoka pande zote za nchi, Wakili maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakugenzi wenzake  wa Kampuni ya Six Telecoms,  ni miongoni mwa waliowasilisha barua kwa DPP.

Mbali na hao raia Sri Lanka AbdulAzeez Amaan naye amefuata utaratibu huo huo  baada ya kukiri kosa la kusafirisha madini yaliyokuwa na thamani zaidi ya Milioni 36 kinyume na sheria.

Hayo yalibainika jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi inayohusu washtakiwa hao  ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

AKINA RINGO TENGA

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori alidai Septemba 24 kesi ilipokuja kwa ajili ya kutajwa upande wa utetezi walisema wana hoja za kushauriana na wateja wao.

Wakili wa utetezi, Bryson Shayo alidai ni kweli waliwasilisha maombi hayo na kwamba tayari wateja wao walishaandika barua kwa DPP.

“Barua imeandikwa kwa kuzingatia maagizo ya Rais Magufuli aliyotoa Septemba 22 mwaka huu, wateja wetu waliandika barua Septemba 26 yenye maombi mbalimbali kuhusiana na shauri hilo.

“Tunaomba ahirisho la siku 14 ili tupate majibu kuhusiana na barua iliyoandikwa,”alidai.

Hakimu Simba alikubali maombi hayo na aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 11 mwaka huu.

Washtakiwa wengine katika  kesi hiyo ambao ni wakurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms, Peter Noni, Hafidh Shamte, na Noel Chacha ambaye ambaye ni Afisa Mkuu wa Fedha.

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani Novemba 20 mwaka 2017 wakishtakiwa kwa uhujumu uchumi na kutakatisha fedha zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu.

Shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote wanne na Kampuni ya Six Telecoms ambapo wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam kwa nia ya kupata fedha walidanganya kwa kutoza kiwango cha chini ya Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa mawasiliano ya simu za kimataifa.

Shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho kwa udanganyifu na kwa nia ya kukwepa malipo walishindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kama kodi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Alidai shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote, wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016 walishindwa kulipa ada ya uendeshaji Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Shtaka la nne linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne ambao kwa pamoja wanadaiwa kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha Dola za Marekani 3,282,741.12 huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la udanganyifu,”alidai Nyantori.

Alidai shtaka la tano linaikabili Kampuni ya Six Telecoms ambayo inadaiwa katika kipindi hicho ilitakatisha kiasi hicho cha fedha.

Shtaka la sita linawakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa katika kipindi hicho walisababisha hasara ya zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu kwa TCRA.

Awali Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai upelelezi ulishakamilika wanaandaa nyaraka muhimu kabla ya kuihamishia kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

RAIA WA SRI LANKA

Wakati huo huo, Mahakama hiyo imemtia hatiani  raia Sri Lanka AbdulAzeez Amaan (26) baada ya kukiri kosa la kusafirisha madini yaliyokuwa na thamani zaidi ya Milioni 36 kinyume na sheria.

Mshtakiwa huyo ambaye  ni mwanafunzi alikiri jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Simba.

Akitoa adhabu baada ya kumtia hatiani, Hakimu Simba alisema mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni 10.

Pia mahakama imeamuru madini yataifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Wakili wa Serikali, Nyantori kabla ya hukumu hiyo aliomba mshtakiwa apewe adhabu kali kwa sababu usafirishaji wa madini hupunguza pato la taifa hivyo aliomba madini yataifishwe.

Juzi Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon akimsomea mshtakiwa mashtaka yanayomkabili alidai Septemba 21 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere uliyopo Ilala Dar es Salaam mshtakiwa alikutwa akisafirisha madini aina ya Scapolite yenye uzito wa gramu 996.50.

Madini aina ya Sperssartite gramu 487, Tanzanite gramu 44, Quarts gramu 126, Citrine gramu 174, blue agate gramu 101.80, Toumarine gramu 16, Aquamarine gramu 14.30 na Supphire gramu 5.04 yote kwa pamoja yakiwa na jumla ya Sh. Milioni 36.5 bila ya kuwa na kibali.

Wakili wa mshtakiwa, Shabani Mlembe alidai tayari mteja wake alishaandika barua kwa DPP ya kukiri kosa hilo hivyo waliomba tarehe ya karibu ambayo ni jana  ili kufanya utaratibu unaotakiwa kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles