27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo Vodacom wanusurika kwenda jela

Na KULWA MZEEDAR ES SALAAM

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC na Inventure Mobile Tanzania/Tala Tanzania zimehukumiwa kulipa jumla ya Sh 5,892,513,000 ambayo ni hasara waliyoisababisha kwa kusimika mitambo, kupiga na kupokea simu za nje bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ilisoma hukumu hiyo jana baada ya vigogo watano wa Vodacom, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Hisham Hendi na wenzake wanne kukiri mashtaka tisa ya uhujumu uchumi yaliyokuwa yakiwakabili.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Simon Wankyo na Jackline Nyantori waliwasomea upya washtakiwa mashtaka tisa wakati shtaka moja la kujiingiza katika genge la uhalifu walilosomewa Aprili tatu mwaka huu likiondolewa.

Washtakiwa walikiri makosa hayo.

Wakili Nyantori alisema kitendo cha kutumia namba 813 kupiga na kupokea simu za nje bila leseni na bila kujulikana, ilikuwa inahatarisha usalama hivyo wapewe adhabu kali.

Washtakiwa waliomba wapunguziwe adhabu kwa sababu ni wakosaji wa mara ya kwanza na wana familia zinazowategemea.

Akitoa adhabu, Hakimu Shaidi alisema kwa shtaka la kwanza hadi la sita, washtakiwa Ahmed Ngassa, Brian Lusiola na Kampuni ya Tala wanakuhumiwa kulipa faini ya Sh milioni tano kwa kila kosa na kwa kila mshtakiwa, endapo watashindwa wataenda jela mwaka mmoja.

“Shtaka la saba washtakiwa hao wanatakiwa kulipa Sh 642,276,000 kwa Serikali ambayo ni hasara waliyoisababisha kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania baada ya kusimika mitambo na kuitumia kwa kupiga na kupokea simu za kimataifa bila leseni.

“Shtaka la nane, Hisham, Joseph Nderuti, Olaf Mumburi, Joseph Bonzo na Vodacom Tanzania kwa kutumia namba 813 isiyosajiliwa kukwepa malipo, wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni tano na wakishindwa kulipa wataenda jela miezi 12,” alisema.

Mahakama hiyo pia imeihukumu Vodacom kulipa Sh 5,250,237,000 kwa Serikali ambayo ni hasara waliyosababisha kwa kutumia namba ambayo haikusajiliwa na wakishindwa kulipa hasara walizosababisha watarudishwa mahakamani kupangiwa adhabu. Washtakiwa wote wamelipa faini.

Awali Wankyo aliwataja vigogo wa Vodacom kuwa ni Hisham, Mkuu wa Kitengo cha Mapato, Joseph Nderitu, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria, Olaf Mumburi, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo, Joseph Muhere, Meneja Uhasibu, Ibrahimu Bonzo na Kampuni ya Vodacom Tanzania.

Washtakiwa wengine ni Meneja Biashara wa Inventure Mobile Tanzania Ltd (Tala Tanzania) Ahmed Ngassa, Mtaalamu wa IT, Brian Lusiola na Kampuni ya Tala Tanzania.

Alidai washtakiwa Ngassa, Lusiola na Kampuni ya Tala Tanzania wanakabiliwa na mashtaka saba ya kuingiza vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki kati ya Januari Mosi mwaka 2018 na Desemba 31 mwaka huo maeneo ya jengo la Tanzanite Park bila kibali cha TCRA.

Wanadaiwa kufunga vifaa hivyo bila kuwa na leseni na kati ya Aprili 17, 2018 na Machi 11 mwaka huu washtakiwa kinyume cha sheria walipokea na kupiga simu za nje bila kuwa na leseni kutoka TCRA.

Wankyo alidai washtakiwa hao kwa nia ya kukwepa gharama za kulipia kwa kupokea na kupiga simu za kimataifa, walisimika mitambo ya mawasiliano kuzuia simu za nje zinaoingia na wanadaiwa kutumia vifaa ambavyo havijaidhinishwa na TCRA.

Shtaka la sita na saba washtakiwa hao wanadaiwa kutumia namba 813 ya Vodacom Tanzania PLC bila kupata baraka za TCRA na shtaka la nane wanadaiwa kusababisha hasara kwa mamlaka hiyo ya Sh 642,276,000.

Nyantori alidai shtaka la nane linawakabili washtakiwa Hisham, Nderitu, Mumburi, Muhere, Bonzo na Vodacom Tanzania PLC ambapo kwa tarehe tofauti kati ya Aprili 17, 2018 na Machi 11 mwaka huu kwa pamoja walitumia namba 813 ya Vodacom bila kibali cha TCRA.

Katika shtaka la tisa washtakiwa hao wanadaiwa kwa kufanya hivyo walisababisha hasara ya Sh 5,250,237,000 kwa TCRA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles