30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Vigogo tisa CCM mbaroni kwa rushwa

JANETH MUSHI-ARUSHA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(TAKUKURU) Mkoa wa Arusha, inawashikilia watu tisa, wakiwemo viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM kwa tuhuma mbalimbali za rushwa.

Miongoni mwa wanaoshikiliwa, ni pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), watumishi na wafanyabiashara mbalimbali.

Waliokamatwa ni Mjumbe wa Baraza la Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Arusha, Sifael Pallangyo, Katibu wa Malezi Wilaya ya Longido na Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Arusha, Upendo Ndoros, Katibu wa Wazazi Wilaya ya Longido na Mjumbe wa Baraza la Wazazi Mkoa wa Arusha, Laraposho Laizer.

Wengine ni Katibu wa wazazi Kata ya Kikatiti, Meru, Godwait Mungure, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Tukusi wilayani Monduli, Mboiyo Mollel, Mwenyekiti wa Kamati ya pembejeo Kijiji cha Loita Kata ya Nkoanrua, Kanankira Nnyary, wafanyabiashara wa Kata ya Olturmet, Gervas Mollel na Joseph Mollel.

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, James Ruge, amesema tukio la kwanza lilitokea  Juni 26, mwaka huu.

Amesema walipokea taarifa kutoka kwa raia mwema, kuwa Lilian Ntiro ambaye anatarajia kugombea ubunge wa viti maalumu (Wazazi) Mkoa wa Arusha alikuwa akifanya siasa ambazo hazikuwa sahihi.

Amesema mtuhumiwa anadaiwa kumpatia Pallangyo fedha kwa ajili ya kwenda kuwahonga wajumbe wa Baraza la Wazazi Wilaya ya Longido kama kishawishi cha kumpigia kura katika kura za maoni zinazotarajia kufanyika hivi karibuni.

Amesema baada ya taarifa hiyo, taasisi hiyo kwa kushirikiana na ofisi yake  Wilaya ya Longido,  waliandaa mtego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kila mmoja akiwa na kiasi tofauti cha fedha zilizokuwa zimeandaliwa kugawiwa kwa wajumbe wa baraza hilo.

“Pallangyo alikutwa na shilingi milioni 14, Upendo  shilingi 552,000 pamoja na simu aina ya Irtel smart ambapo kulikuwa na mawasilianao na watuhumiwa wenzake, Laraposho alikuwa na shilingi 117,000, simu aina ya Samsung Galaxy  ambapo kulikuwa na mawasiliano na watuhumiwa wenzake.

“Mungure alikuwa na simu ndogo ikiwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Pallangyo,” amesema.

Amesema uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea ambapo watuhumiwa wote wako mahabusu tangu Juni 26, mwaka huu, huku wakitarajiwa kupewa dhamana  jana.

Amesema taasisi yake inaendelea kumshikilia mtia nia (Lilian)  kwa mahojiano.

WAJIPATIA MILIONI 15/-  

Pia taasisi hiyo, inawashikilia Gervas Mollel na Joseph Mollel ambao ni wafanyabiashara wa Olturmet kwa kujipatia Sh milioni 15 kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mfanyabiashara mwenzao, Advera Kyarunzi mkazi wa Mto wa Mbu wilayani Monduli.

Amesema awali ilielezwa wafanyabiashara hao, wote walikuwa wakishirikiana kusafirisha mbegu za vitunguu kutoka Tanzania kwenda Uganda, ambapo Septemba 2018 baada ya kupakia mzigo ukiwemo wa Advera uliokuwa wa Sh milioni 15, walikubaliana Advera, Gervas Andrea na Haruna Kitundu, watangulie kwa basi kwenda mpaka Murongo ambako wangekutana na Mollel ambaye alikuwa  dereva wa gari aina ya Fuso yenye namba T 449 ATT.

“Gervas alisema anaumwa tumbo, atampatia Advera kijana mwingine wa kuvuka naye mpakani, Advera alipojaribu kuwasiliana na Christopher ikawa hapatikani kwenye simu na hakuweza kumuona tena wala kupata mzigo, aliendelea kufuatilia fedha zake bila mafanikio, watuhumiwa tunaendelea kuwahoji,” amesema.

PEMBEJEO ZA RUZUKU

Katika tukio la tatu,amesema taasisi hiyo imewakamata Mboiyo Mollel, Mikidadi Mollel na Kanankira kwa kosa la kughushi vocha za pembejeo za kilimo za ruzuku ambazo walitakiwa kuzigawa Kijiji cha Tukusi wilayani Monduli, mwaka 2016.

Amesema watuhumiwa walipaswa kugawa mbegu za mahindi, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia kwa wakulima,wao waligawa mbegu tu na baadaye katika vocha wakaonyesha wamegawa vitu vyote wakati siyo kweli, ambapo uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,854FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles