VIGOGO SITA NJOMBE WANASA ANGA YA MAJALIWA

0
473


Na Mwandishi Wetu, Njombe

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema ana taarifa za watendaji wakuu wa Wilaya ya Makete wakiwamo Mkurugenzi wa Halmashauri, Francis Namsumbo, Mweka Hazina, Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi, Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani, Michael Shija, kuhusika na upotevu wa Sh milioni 71 zikiwamo Sh milioni 41 za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi jioni alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa Njombe wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani hapa.

Alisema watumishi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo mbalimbali ili kuficha ubadhirifu huo.

“Mkuu wa mkoa hakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuhusu matukio haya,” alisema.

Pia alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, kuhakikisha mtumishi mmoja wa Wanging’ombe, Edwin Kigoda, anachukuliwa hatua stahiki kwa ubadhirifu wa Sh milioni 37.9 zilizotolewa kuwajengea uwezo walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Mbali na watumishi hao, pia alimtaka Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa Ardhi wa Mji wa Njombe, Addo Kabange, anayetuhumiwa kuuza viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.

Pia alimwagiza Sendeka kuchukua hatua kali kwa waliohusika na upotevu wa zaidi ya Sh bilioni moja za vyama vya ushirika.

Majaliwa alisema kati ya fedha hizo, Sh milioni 532.736 zilipotea katika Saccos ya Kurugenzi Njombe na Sh milioni 900 zilizopotea katika Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe Saccos.

 “Maofisa ushirika nchini mmeendelea kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha ushirika. Katika eneo hili ninahitaji mkuu wa mkoa ufuatilie suala hili na kuwachukulia hatua wahusika wote,” alisema Majaliwa.

Pia aliwaagiza wakuu wote wa wilaya kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika mkoani Njombe.

 “Tunataka ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika ulioambatana na harakati za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia wana ushirika wasio waaminifu,” alisema.

Aliwasisitiza watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu, kutojihusisha na rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma na Serikali itachukua hatua kali dhidi ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao kujinufaisha.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu umiliki wa Kiwanda cha Chai cha Lupembe na kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.

Alisema alipotembelea kiwanda hicho alifarijika kukuta kimeanza kufanya kazi baada ya kusimama kwa takriban miaka minane kutokana na mgogoro uliopo baina ya mwekezaji na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.

Alisisitiza kwamba Serikali haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi, hivyo aliahidi kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta njia ya kutatua mgogoro uliopo.

Majaliwa alisema baada ya kusomewa taarifa ya kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika, alibaini kuwapo kwa mgogoro unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa amani na usalama.

Pia alielekeza shughuli za ulimaji na uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika kiwanda hicho iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la wakulima na ajira za watumishi wa kiwanda hicho.

Alisema kwa kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia, aliuelekeza uongozi kuhakikisha wanaweka wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika katika bodi ya kiwanda hicho.

 Katika hatua nyingine, Majaliwa alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga na alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi, bali ni mpango wa Serikali wa kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa Watanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here