JUDITH PETER NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga, watashuka dimbani leo kusaka pointi muhimu kwenye viwanja tofauti ikiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) mzunguko wa pili unaoelekea ukingoni.
Yanga ambao Jumapili iliyopita waliichakaza FC Platinum ya Zimbabwe kwa mabao 5-1 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, watakuwa wenyeji wa Kagera Sugar kwenye uwanja huo.
Simba nao wamesafiri hadi mkoani Tanga kuifuata Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ambapo wanatarajia kucheza mechi yao ya kiporo iliyosogezwa mbele na bodi ya ligi inayosimamia michuano hiyo.
Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia pointi 31, itakuwa vitani kuwania pointi ambazo zitairejesha kileleni kuongoza ligi hiyo baada ya kushushwa na Azam FC iliyofikisha pointi 33, kwa kuifunga Ndanda FC bao 1-0 juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake wanaokabiliwa na adhabu ya kadi tatu za njano, Kelvin Yondani, Danny Mrwanda na Said Juma pamoja na kiungo, Haruna Niyonzima anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa katika mechi dhidi ya Simba.
Mbrazil Andrey Coutinho, ambaye aliikosa mechi ya watani wa jadi kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti aliyopata kwenye mechi ya Mbeya City, pia hatacheza dhidi ya Kagera pamoja na beki, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye ni majeruhi.
Yanga itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum ya Zimbabwe kwenye mechi ya kimataifa, lakini pia machungu ya kufungwa bao 1-0 na watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu uliofanyika Machi 8, mwaka huu.
Kwa upande wa kikosi cha Simba kinachonolewa na kocha Mserbia, Goran Kopunovic, sasa kimeimarika zaidi baada ya kushinda mechi tatu mfululizo na kufikisha pointi 29 na kuendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, ikiwa ni tofauti ya pointi mbili nyuma ya Yanga.
Simba ilitoa kipigo cha mabao 5-0 kwa Tanzania Prisons, ikawafunga mahasimu wao, Yanga bao 1-0 na Mtibwa Sugar bao 1-0, matokeo ambayo yanazidi kumpa Goran kiburi cha kuendeleza kasi hiyo ili kuongeza matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Kwa mara ya mwisho msimu uliopita Simba ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani na kuweka rekodi ya kushindwa kutamba kwenye uwanja huo kwa misimu miwili tangu kupanda kwa timu hiyo.
Akizungumzia mechi yao, kocha mkuu wa Kagera Sugar Mganda, Jackson Mayanja, alisifia uwezo wa wachezaji wake wa kucheza soka la kiufundi na kupiga pasi zinazoeleweka, ambazo zinaweza kuwachanganya Yanga kama ilivyokuwa katika mchezo wa awali.
“Mchezo wa awali tuliwafunga Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, hivyo waamuzi wa pambano hili wanatakiwa kuchezesha kwa umakini bila upendeleo ili wapenzi wa soka waweze kupata burudani,” alisema.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Stand United ambayo ilipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa vibonde, Tanzania Prisons Jumamosi iliyopita, watakaribishwa na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.