25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

Vigogo Kenya wakwama kufanya umafia

Inter-faith prayers ceremony for Westgate shopping mall victimsNa Mwandishi Wetu, Tanga

MRADI wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka mkoani Tanga hadi Hoima nchini Uganda, umechukua sura mpya baada ya Serikali ya Tanzania kushtukia umafia wa baadhi ya vigogo wa Serikali ya Kenya.

Kutokana na hali hiyo vigogo hao walijikuta wakikwama na kunyang’anywa hati za kusafiria walipokuwa wakijaribu kuingia kinyemela katika Bandari ya Tanga.

Maofisa hao waandamizi wa Kenya akiwamo Waziri wa Nishati, Charles Keter, walizuiwa huku ujumbe kutoka nchini Uganda, ulioongozwa na Waziri wa Nishati,  Irene Muloni, ukiruhusiwa kuendelea na ziara hiyo bila kusumbuliwa.

Maofisa waandamizi wa Kenya walianza safari yao Lamu, ambako walikagua mradi wa ujenzi wa bandari ya Lamu kabla ya kuelekea Bandari ya Tanga.

Safari hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni ya kutatua mvutano baina ya Kenya na Uganda kuhusu mpango wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ya Uganda kupitia Kenya au Tanzania.

Tukio hilo limevuta hisia na kuonesha kiu ya Kenya kuutaka mradi huo kwa udi na uvumba na namna inavyoleta mtihani kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mamlaka za Tanzania zilichukua nyaraka za kusafiria za Keter, Katibu Mkuu wa Petroli, Andrew Kamau na mwenzake wa Nishati, Joseph Njoroge na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Lamu, Sudan Kusini na Ethiopia (Lapsset), Sylvester Kasuku, wakati wakijaribu kuingia Bandari ya Tanga kwa mgongo wa ujumbe wa Uganda.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni moja ya mkakati kwa Tanzania kulipiza kisasi kwa kitendo cha Kenya kutowaalika Lamu wala katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, Nairobi, baina ya marais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Yoweri Museveni wa Uganda Jumatatu wiki hii.

Katika kikao hicho maofisa wa Uganda na wawakilishi wa kampuni za mafuta pekee ndiyo walioalikwa katika mkutano wa Nairobi ilihali ikifahamika Tanzania ina maslahi katika mradi huo.

Kutokana na tukio hilo, Kamau alithibitisha hati za kusafiria za maofisa wa Kenya zilichukuliwa wakati walipowasili Tanga kukagua bandari, ambayo imependekezwa kwa upande wa Tanzania kutumika kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda.

“Kimsingi tu mateka hapa. Wamekataa kuturudishia hati zetu za kusafiria kwa karibu saa moja. Pia wamekataa kuturuhusu kuingia katika bandari ya Tanga,” Kamau alisema alipohojiwa na gazeti la Daily Nation la nchini Kenya.

“Wameruhusu ujumbe wa Uganda tu kuingia bandarini,” alisema. Hati zetu za kusafiria zilirudishwa karibu saa moja baadaye,” alisema.

Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unalinda viongozi wenye hadhi ya kidiplomasia, wenye hati za kidiplomasia wanaowasili katika bandari ya kigeni kwa kawaida hupewa stahili fulani za kuingia maeneo hayo.

Lengo la kufanya hivyo ni kulinda wanadiplomasia wa kigeni dhidi ya vikwazo visivyo na sababu wakati wakitimiza shughuli zao.

Hata hivyo ni wajibu wa kuituma Wizara ya Mambo kupitia ubalozi ulio karibu, kuitaarifu nchi wenyeji kuhusu ziara ya ujumbe huo.

Katika tukio hilo kufahamika kama Kenya iliijulisha Tanzania kuhusu ziara hiyo.

Wakati wa mkutano wa Jumatatu, Kenya na Uganda zilishindwa kuafikiana kuhusu ujenzi wa bomba hilo kupitia ukanda wa Kaskazini, kutoka Hoima nchini Uganda kupitia Lokichar, hadi Lamu, wakati Rais Museveni alipoibua maswali kuhusu uwezekano wa mradi huo, bandari ya Lamu kuchelewa pamoja na wasiwasi wa kiusalama nchini Kenya.

Kampuni za mafuta zinazoendesha utafiti nchini Uganda zilikuwa zimeonya kuwa mipango ya Uganda kuanza kuvuna mafuta mwaka 2018 inaweza kuchelewa iwapo itaendelea na mpango wa kujenga bomba hilo nchini Kenya.

Kampuni hizo ni Total, Tullow Oil plc na China National Offshore Oil Company (CNOOC).

Hata hivyo, Tullow Oil plc imekana kuwa na mkono katika utafiti huo.

Tullow imeeleza wazi kuhusu mtazamo wao wa njia za kaskazini na kusini kupitia Kenya kuwezekana kiufundi, ambapo kwa mujibu wa taarifa yake kupitisha bomba la mafuta katika njia ya Kaskazini kuna manufaa zaidi kifedha kwa mafuta ghafi ya Kenya na Uganda.

Baada ya mkutano wa Jumatatu, ujumbe wa Uganda ukiongozwa na Muloni, na timu ya Kenya ikiongozwa na Keter zilipewa kazi ya kufanya mikutano ili kuja na msimamo wa pamoja kuhusu bomba la mafuta na kuripoti kwa marais wakati wa mkutano utakaofanyika Kampala nchini Uganda wiki mbili zijazo.

Baada ya kufanya vikao virefu siku ya Jumanne, timu hizo mbili zilielekea Lamu kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari.

Wakiwa Lamu, maofisa walitembelea magati matatu ya kwanza ya bandari yanayotarajiwa kujengwa.

Baadaye walifanya mkutano wa ndani na wadau wa mradi wa Lamu, Lapsset, Mtendaji wa Ardhi wa Kaunti ya Lamu na watalamu wa sekta ya mafuta baadaye msafara huo walielekea Tanga Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, alinukuliwa na gazeti la Nation kwamba wizara yake ilimuagiza balozi wa Kenya mjini Dar es Salaam, Chirau Mwakwere, kutatua suala hilo na Serikali ya Tanzania.

“Balozi wetu anawasiliana nao na anajaribu kutatua tatizo hili. Nitakutaarifu baadaye kuhusu yaliyojiri,” alisema kwa njia ya simu.

Hata hivyo Balozi Mwakwere, alisema hafahamu suala lolote.

“Sifahamu unachozungumza. Iwapo nitajua ningekuwa na taarifa. Lakini subiri nifuatilie,”  alisema Balozi Mwakwere .

Kauli ya RC Shigella

Kutokana na tukio hilo MTANZANIA ilimtafuta Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo ambapo alisema hawakuwa na taarifa za ujio wa wageni kutoka Kenya.

“Mgeni anapokuja ni lazima ujue anatoka wapi na anakwenda wapi, sasa anaingia ndani hana maaelezo ya kina utampeleka wapi? Sisi kama mkoa tuliwaambia hatuna taarifa za ujio wao,” alisema RC Shigella.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,682FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles