NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
VIGOGO sita wa Kampuni ya Viettel Tanzania, akiwemo Mkurugenzi wa Halotel, Son Nguyen (46), wanaokabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya zaidi ya Sh bilioni 78 wameandika barua kukiri makosa yao.
Taarifa ya washtakiwa hao kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) ziliwasilishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kupitia Mahakama Mtandao.
Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai kesi ilikuja kwa kutajwa, upelelezi haujakamilika na waliomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Wakili wa utetezi, Majura Magafu akisaidiana na Iddi Msangi, alisema Aprili 21, mwaka huu wateja wao waliandika barua kwa DPP kukiri makosa.
Wakili Magafu alidai barua hiyo imepokewa, majadiliano yameanza na wamekamilisha kwa kiasi kikubwa, kinachosubiriwa ni hati ya kuipa mamlaka Mahakama ya Kisutu kuendelea na shauri hilo kutoka kwa DPP.
Alisema DPP yuko Dodoma hivyo akirudi wataendelea kufuatilia.
Hata hivyo, Magafu alipendekeza kesi itajwe Ijumaa, lakini Wakili Wankyo alisema kwa kuwa bado mazungumzo yanaendelea kesi ipangwe kutajwa ndani ya siku 14, lakini wakikamilisha kabla washtakiwa wataletwa.
Hakimu Simba alikubali na kusema kwamba mazungumzo yakikamilika wiki hii washtakiwa wataletwa ikiwa bado kesi itatajwa Mei 18.
Mbali na Son washtakiwa wengine ni Nguyen Minh (40) na Vu Tiep ambao wote ni mameneja wa Halotel, Ha Than (39) ambaye ni mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) Halotel, Mkurugenzi wa fedha wa kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel.
Awali waliposomewa mashtaka Machi 27 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, ilidaiwa washtakiwa hao kati ya Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida.
Inadaiwa kati ya Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi kwa pamoja walitumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.
Pia inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo hayo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.
Katika mashtaka ya nne, inadaiwa washtakiwa hao walikwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Viettel Tanzania na Vietnam kinyume na sheria.
Inadaiwa Juni 8, 2017 na Machi 26, 2020 maeneo hayo kwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA walisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 75.
Pia wanadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh bilioni 3.03.
Katika mashtaka ya saba washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.
Kampuni ya Viettel Tanzania inadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu ilitakatisha Sh bilioni 3.03 na mashtaka ya tisa na 10, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha Sh bilioni 75 wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu.