29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO CCM WAANZA KUKIMBIA UCHAGUZI

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


WAKATI hekaheka za uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zikianza kupamba moto, vigogo wake wameanza kukimbia, huku wengine wakibadili gia angani kutowania nafasi ndani ya chama hicho na jumuiya zake.

Baadhi ya vigogo wa ngazi ya taifa, wameanza kutafakari uamuzi uliotangazwa na chama hicho kupitia Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Magufuli, kutaka mtu mmoja awe na nafasi moja na si vinginevyo.

Agizo hilo alilitoa Desemba 13, mwaka jana wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Dk. Magufuli alisema wakati wa mtu kuvaa kofia nyingi ndani ya chama ufike mwisho na kuwa sasa ni wakati wa nafasi moja ya uongozi kushikwa na mtu mmoja.

Alisema hilo litasaidia kutoa nafasi kwa watu wengine pia kukitumikia chama.

Hali hiyo ya baadhi ya viongozi wa juu wa CCM kuamua kutogombea tena uongozi ndani ya chama hicho, inatajwa kuwa huenda ni hofu ya majina yao kukatwa na Kamati Kuu (CC) kama utekelezaji wa agizo la mwenyekiti wao.

Taarifa zilizoifikia MTANZANIA kutoka kwa maofisa wa juu wa CCM, zinasema kuwa licha ya kanuni za chama hicho tawala kuwa kimya na viongozi wenye nafasi zaidi ya moja kuzuiwa kugombea au kukatwa kwa majina yao, jambo hilo linaweza kuibua hofu na manung’uniko.

“Unajua wapo hadi wabunge ambao nao wamegombea nafasi mbalimbali za kitaifa, lakini kutokana na mabadiliko ya CCM mpya, kuna kila dalili ya kukatwa kwa majina yao. Na hili fagio litagusa hadi ndani ya jumuiya za chama ambako kwa sasa tochi limekuwa likiwamulika sambamba na wale waliopandikizwa,” kilisema chanzo chetu.

 

BULEMBO AJING’OA

Jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Abdallah Bulembo, alitangaza kujitoa katika kinyang’anyiro kutetea nafasi yake.

Hatua hiyo imekuja baada ya ile ya awali aliyoitoa miezi michache iliyopita, kuwa hatogombea tena nafasi hiyo, kabla baadaye kuchukua fomu baada ya kupata shiniko kutoka kwa makatibu wa mikoa na wazee wa jumuiya hiyo.

Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari Dar es Salaam, Bulembo alisema tangu mwanzo aliamua kutogombea, lakini baadaye aliombwa na makatibu wa mikoa wa jumuiya hiyo na wazee, ndipo akachukua fomu.

“Mwanzoni nilipotangaza kutogombea, makatibu wangu wa mikoa walitaka nichukue fomu, lakini tangu nimechukua sijawahi kuomba ushauri, hivyo msimamo wangu wa kutogombea uko pale pale.

“Hivyo leo (jana) ninapeleka barua kwa Katibu Mkuu wa chama (Abdulrahman Kinana) ya kumweleza dhamira yangu hii,” alisema.

Bulembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema alichukua fomu kwa kuwa haikuwa dhambi, kanuni za chama zinaruhusu na kwamba upo uwezekano wa kuwa na nafasi mbili za uongozi.

“Kumekuwa na upotoshaji kwamba ukiwa mbunge au waziri hauwezi kugombea nafasi nyingine, sasa hapa nina kitabu cha kanuni za mwaka 2005, 2010, 2012 na 2017, zinasema kiongozi au mbunge, waziri anaweza kugombea ila Kamati Kuu ya chama itaamua inavyofaa, kama bado anahitajika atapitishwa, lakini mimi sitagombea tena.

“Hivyo chama chetu tunafanya kazi kwa vikao na vikao vikiamua ndiyo matokeo,” alisema Bulembo ambaye pia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais.

Kauli hiyo ya Bulembo inapingana na ile ya Dk. Magufuli aliyoitoa wakati anaingia madarakani, kuwa hakuna ruhusa mtu kuwa na nafasi mbili CCM.

Mbali na Magufuli, Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole, naye mara kadhaa amekuwa akisema kuwa ndani ya chama hicho ni mtu mmoja nafasi moja.

Katika mkutano huo, Bulembo alisema anaamini wagombea 48 waliopatikana, yupo mmoja ambaye atafaa kuongoza jumuiya hiyo.

Alisema uchaguzi katika ngazi ya taifa utafanyika kuanzia Novemba 20 hadi 23, huku akiwatahadharisha wagombea ambao wameanza kampeni mapema, watakuwa wameshajikata.

Alipoulizwa pamoja na kwamba anang’atuka ameiachaje jumuiya, alisema: “Nitaondoka na kuacha historia kuliko mtu yeyote yule… nilikuta akaunti ya jumuiya ina sifuri, lakini nitaacha fedha na siwezi kutaja hapa, hili nitalisema mbele ya mwenyekiti wa chama (Dk. Magufuli) siku nakabidhi kijiti.”

 

KINANA

Katika moja ya ziara zake za kuimarisha chama nchini, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alikuwa akisisitiza kwa kuwataka viongozi wa chama hicho kutoongoza wanachama na wananchi kwa kutumia mawazo yao.

Kauli hiyo amekuwa akiirudia kila wakati.

Alisema kuwa CCM haiko madarakani kutafuta ubwana mkubwa, ila ina jukumu la kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa mujibu wa sheria.

“Pindi mnapohojiwa, tambueni kuwa ni wajibu wetu kutoa majibu sahihi katika hili na kama mtafanya kinyume na haya, ni wazi mtakuwa mnakiweka chama katika mazingira ya kutoaminiwa.

“Na kama kuna kiongozi ambaye anaona kuwa ameelemewa na uzito wa uongozi, atumie busara na kupima ili aweze kukaa pembeni,” alisema Kinana akiwa katika ziara yake Machi, 2013 mkoani Morogoro.

Mwisho

 

 

 

Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles