27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Vigogo CCM Arusha watimkia Chadema

IMG_20150809_114435NA ELIYA MBONEA, ARUSHA

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Mkoa huo, Isack Joseph, wamekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha  Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ole Nangole na Joseph walifikia uamuzi huo jijini hapa jana na kusema kwa nyakati tofauti wamelazimika kuchukua uamuzi huo kwa kuwa utaratibu wa kumpata mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulikiukwa.

Kwa mujibu wa wana CCM hao, wakati wa mchakato huo baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho walikuwa na wagombea wao mifukoni waliotaka wagombee nafasi hiyo.

Kwa upande wake, Ole Nangole aliyejiondoa CCM akiwa kwenye kipindi cha awamu ya pili cha uenyekiti wake, alisema alijiunga CCM mwaka 1977 ambapo alifanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali zikiwamo mwenyekiti wa CCM wilaya kwa miaka kumi.

“Ndugu zangu waandishi wa habari nimewaita leo kuwaambia jambo moja kwamba ninahama CCM kuanzia sasa. Najiuzulu nafasi yangu ya mwenyekiti niliyoitumikia kwa miaka saba na ninajiunga na Chadema kuanzia sasa.

“Nashindwa kuwa na moyo wa chuma wa kuendelea kuwa ndani ya CCM kwa sababu CCM niliyoifahamu tangu enzi za TANU siyo hii ya sasa.

“Kuondoka kwangu kumechangiwa na kikundi cha viongozi wachache kuiongoza CCM kwa mabavu, nguvu na kwa kutumia fedha walizokwapua serikalini.

“Miaka yote tangu nilipojiunga CCM mwaka 1977, sikuwahi kukiona chama hiki kikiendesha mambo yake bila kufuata kanuni na taratibu za vikao kama kilivyofanya wakati wa vikao vya kupitisha mgombea urais mjini Dodoma hivi karibuni.

“Mkutano mkuu wa CCM uliongozwa kwa kukiuka haki na misingi kwa wanachama kwani hata nyinyi mtakumbuka kulikuwa na mchakato wa urais na wagombea 40 walijitokeza akiwamo Edward Lowassa.

“Kwa mapenzi yake Lowassa alivyokitumikia chama na Taifa, wananchi tuliamini mchakato ule kama jina lake lisingekatwa angekuwa mmoja wa wagombea ambao wangefika mbali ndani ya chama.

“Lakini jina lake lilikatwa bila sababu japokuwa sababu tulizijua tangu alipotoka kwenye uwaziri mkuu kwa vile kuliendelea kusambazwa maneno na hujuma za kisiasa dhidi yake kupitia kwa viongozi wa chama na Serikali wakiwamo vijana wadogo waliopewa fedha na madaraka ili wamchafue,” alisema Ole Nangole.

Kwa upande wake, Joseph alimnyooshea kidole Katibu wa CCM, Abdulrahman Kinana na kumtaka achunge ulimi wake pindi anapowaita Watanzania makapi ndani ya nchi yao.

Joseph ambaye ni Diwani wa Kata ya Monduli Mjini aliyemaliza muda wake na kupita bila kupingwa ndani ya CCM, alisema hakuna Mtanzania aliye makapi kwani wote wana haki ya kidemokrasia ya kuhama vyama kwa jinsi watakavyoona inafaa.

“Watasema mengi na tumeondoka watatuita makapi. Naomba niwaambie, sisi siyo makapi, wakitaka tuzungumze suala la makapi hao wanaosema hivyo wao ndio makapi halisi.

“Sisi Watanzania si makapi kwani tukichambuana kwa suala la makapi na kuangalia wewe umetokea wapi, tutakwenda kusiko. Kwanza aliyesema hiyo kauli yeye ni Msomali. Hivyo tukisema nani ni makapi yeye ndiye makapi halisi anayeishi Tanzania kwani asili yake ni Somalia,” alisema Joseph.

Joseph alitoa kauli hiyo zikiwa ni siku chache baada ya Kinana kunukuliwa na vyombo vya habari akisema wanachama wa CCM wanaohamia Chadema ni makapi.

Akizungumzia kuhusu kuhama kwake, alisema ametafakari kwa muda kilichotokea mjini Dodoma na kisha kuamua kuiridhisha roho na nafsi yake, kwamba kilichofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM kilikuwa ni uhuni wa kisiasa.

“Mheshimiwa Lowassa alisema demokrasia imebakwa ndani ya CCM. Mimi nasema kanuni na taratibu za CCM zimehodhiwa na kikundi cha watu wachache.

“Ukiona wachache wanahodhi madaraka ya chama, huna sababu ya kurudi nyuma na kuangalia chama ni cha watu wachache au ni cha wanachama.

“Hivyo basi, nimetafakari kwa muda mrefu, nimeridhika kwamba uamuzi ninaouchukua kuondoka CCM na kujiunga na Chadema ni sahihi,” alisema Joseph.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles