Vigogo 13 uhujumu uchumi warudi uraiani

0
1082

Kulwa Mzee -Dar es salaam

VIGOGO 13 wa kesi za uhujumu uchumi wamefanikiwa kuruka kihunzi cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kukiri makosa na kuachiwa huru.

Miongoni mwa walioachiwa ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura.

Wambura ameachiwa huru kwa masharti baada ya kukiri kosa la kujipatia Sh milioni 100.9 kwa udanganyifu.

Makubaliano kati ya DPP na Wambura yalisomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai makubaliano yako tayari na Hakimu Mhina alisema kisheria yanatakiwa yasomwe ili mshtakiwa aseme kama ndivyo walichokubaliana.

Akisoma, Wankyo alidai mshtakiwa na DPP walikubaliana kuondoa mashtaka yote 16, likiwemo la kutakatisha fedha na kubakia na shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Wankyo alidai kuwa wamekubaliana kurejesha fedha alizojipatia Sh 100,998,124 kwa awamu tano ambazo ni Oktoba 7, mwaka huu Sh 20,249,531, Desemba kiasi hicho, Machi 2020 kiasi hicho, Juni 2020 kiasi hicho hicho, na Septemba 2020 kiasi hicho atakuwa anamalizia.

Wambura alisomewa shtaka moja la kujipatia Sh 100,998,124 akakiri na mahakama ikamtia hatiani kwa kosa hilo.

Hakimu Mhina alimfahamisha mshtakiwa haki ambazo atazikosa kwa makubaliano hayo kuwa ni ya kukata rufaa, kesi yake kusikilizwa, kukata rufaa makubaliano hayo na kwamba haki ya kukata rufaa itabaki katika adhabu.

“Mahakama inatoa amri ya kulipa fidia kama walivyokubaliana Sh 100,998,124 kwa awamu tano, adhabu yake asifanye kosa la jinai kwa miezi 12, mahakama inamwachia kwa masharti hayo,” alisema Hakimu Mhina.

Wambura aliachiwa huru, na furaha ilitawala kwa ndugu na jamaa waliofurika mahakamani hapo.

Alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Februari 11, mwaka huu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 17 yakiwemo ya kutakatisha zaidi ya Sh milioni 100.

Mashtaka hayo yaliondolewa na kubakia na shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu akidai kuwa fedha hizo ni sehemu ya malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 30,000 kwa Kampuni ya Jeck System Ltd huku akijua kuwa si kweli.

DK. TENGA NA WENZAKE

Wakili maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakurugenzi wenzake, nao wameachiwa huru baada ya kuingia makubaliano na DPP ya kulipa Dola za Marekani 3,748,751.19, ndani ya miezi sita, kuiachia Serikali nyumba iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam na mshtakiwa wa sita kulipa Sh milioni 30.

Wakurugenzi hao wa Kampuni ya Six Telecoms, Dk. Tenga, Hafidh Shamte, Peter Noni na Noel Chacha ambaye ni Ofisa Mkuu wa Fedha, wanatakiwa kulipa zaidi ya Sh bilioni 3 na Frank Mwalongo anatakiwa kulipa Sh milioni 30.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alisema makubaliano mengine ambayo mahakama inatakiwa kuzingatia ni kwamba washtakiwa wamelipa Dola za Marekani 150,000 na Dola 3,585,115 zilizobakia washtakiwa kuanzia wa kwanza hadi watano watalipa ndani ya miezi sita kuanzia jana.

Awali mahakama iliwatia hatiani na kuamuru warejeshe fedha kama walivyokubaliana na DPP.

Washtakiwa katika mashtaka mapya waliondolewa shtaka la kutakatisha fedha na kubakia na shtaka la kwanza linalowakabili washtakiwa wanne na Kampuni ya Six Telecoms.

Wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Desemba 2015 jijini Dar es Salaam kwa nia ya kupata fedha, walidanganya kwa kutoza kiwango cha chini ya Dola za Marekani 0.25 kwa dakika kwa mawasiliano ya simu za kimataifa.

Shtaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho kwa udanganyifu na kwa nia ya kukwepa malipo, walishindwa kulipa Dola za Marekani 3,282,741.12 kama kodi kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Nchimbi alidai shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote, ambao wanadaiwa kati ya Januari 2014 na Januari 2016 walishindwa kulipa ada ya uendeshaji Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Shtaka la nne linawakabili mshtakiwa wa kwanza hadi wanne ambao kwa pamoja wanadaiwa kuisababishia hasara TCRA Dola za Marekani 3,748,751.19.

VIGOGO NIDA

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watatu, wamegoma kuandika barua ya msamaha na kukiri makosa yao, huku wenzao wawili wakiwa wameandika na bado kukiri makosa mahakamani.

Washtakiwa katika kesi hiyo wanakabiliwa na mashtaka 100 yakiwemo ya kutakatisha fedha 25, kumdanganya mwajiri 43, kughushi 22, kusababisha hasara matano, kujipatia fedha mawili na moja kutumia madaraka vibaya.

Waliogoma kuandika barua ni Maimu, Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani, Meneja Biashara wa Nida, Avelin Momburi, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima na Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.

Walioandika barua ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege na Xavery Kayombo ambao walifikishwa mahakamani bila kuwepo washtakiwa wengine.

Upande wa Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Salum Ally, ulikwama kuwasomea upya washtakiwa mashtaka yao kwa sababu washtakiwa wengine hawakuwepo.

Mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi leo kuwasomea upya mashtaka ili washtakiwa wawili waliokubali kurejesha fedha wakiri makosa yao.

WAFANYAKAZI TIGO

Wafanyakazi watatu wa Kampuni ya simu za mkononi ya Tigo na wafanyabiashara wawili waliofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizile wakikabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kutakatisha fedha Sh milioni 20.3 nao wamekubali kurejesha.

Mashtaka mengine ni kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka katika akaunti za wateja, kuingilia mifumo ya kifedha ya Tigo pesa bila kibali na kupatikana na mavazi ya JWTZ.

Wafanyakazi wa Tigo ambao wanashtakiwa katika kesi hiyo ni Kokubelwa Karashani, mtoa hudumu kwa wateja, Godfrey Magoye, wakala na Khalfan Milao mtoa huduma kwa wateja. Wengine ni Mohamed Abdallah mfanyabiashara na Moses Kilosa.

Wakili wa Serikali Mkuu, Awamu Mbagwa, alidai washtakiwa hawajakamilisha kulipa fidia ya Sh milioni 20.3 lakini walishaanza kulipa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here