29.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo vya mama wajawazito bado changamoto

*Mkutano wa ICPD25 kufanyika Zanzibar Novemba 9 hadi 11

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Pamoja na juhudi mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali katika kuhakikisha kwamba vifo vya wajawazito vinapungua, lakini bado changamoto kubwa imeonekana katika vituo vya afya ambapo asilimia 90 ya vifo vimekuwa vikitokea huko.

Meneja wa Programu ya Afya ya Uzazi-Mama na Mtoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi(UNFPA Tanzania), Felista Mbwana.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam Novemba 4, 2022 na Meneja wa Programu ya Afya ya Uzazi-Mama na Mtoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi(UNFPA Tanzania), Felista Mbwana, wakati akielezea mkutano wa Idadi ya Watu Duniani na Maendeleo (ICPD25) unaotarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar Novemba 9 hadi 11, mwaka huu.

Amesema kwa Tanzania hali ya vifo vya mama na watoto wachanga bado iko juu, kwani wanawake 556 kati ya vizazi 100,000 wanakufa kila mwaka uzazi kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika.

“Hii ni sawa na kusema kwamba wanawake 30 kwa siku wanapoteza maisha kila siku sababu ya uzazi, lakini pia kwa takwimu ambazo zimetolewa na Wizara ya Afya, zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wanafariki dunia wakiwa katika vituo vya afya au hospitali hali ambayo inaacha maswali juu ya ubora wa huduma zetu za afya.

“Kwani zamani wanawake walikuwa wanapoteza maisha kwa kutokufika katika vituo vya afya au hospitali, lakini leo hii wanakufa wakiwa katika mikono ya wataalamu wa afya ambalo siyo jambo jema hata kidogo,” amesema Mbwana.

Amesema wao kama Umoja wa Mataifa hasa UNFPA ajenda yao ni kuona kwamba hakuna mwananmke anayepoteza maisha wakati na baada ya kujifungua huku akiainisha mambo matatu wanayoyatazamakuwa mwarobani.

“Kwanza kabisa tunahakikisha kuwa hakuna mwanamke anayepoteza maisha sababu ya uzazi ili kufanikisha hilo tunatakiwa kuhakikisha kuwa mtu anayehitaji huduma ya uzazi wa mpango anaweza akapata anapohitaji ambapo inaweza kuzuia vifo kwa asilimia 40, kwani tunaona bado matumizi ya uzazi wa mpango nchini yako chini hasa kwa vijana balehe.

“Jambo la pili ni upatikanaji wa huduma za dharura kwa usahihi ambapo linaweza kuokoa maisha ya mama na mtoto wake na jambo la tatu ni kuwa na wataalamu waliosoma ambao wanahamasa ya kufanya kazi husika kwani pia wataweza kusaidia kupunguza vifo,” amesema Mbwana.

Ramadhani Hangwa ambaye ni Mchambuzi wa Masuala ya Idadi ya Watu na Maendeleo UNFPA.

Upande wake Ramadhani Hangwa ambaye ni Mchambuzi wa Masuala ya Idadi ya Watu na Maendeleo UNFPA, akizungumzia mkutano huo wa Idadi ya Watu Duniani amesema kuwa unalenga kujadili na kupitia mapendekezo mbalimbali yaliyoazimiwa katika mkutano wa mwisho wa Tathimini ambao ulifanyika jijini Nairobi nchini Kenya mwaka 2019 ukihusisha mataifa 173 Tanzania ikiwemo.

“Lengo la mkutano ule ambao ulifanyika ikiwa ni baada ya miaka 25 tangu kufanyika kwa mkutano wa kwanza mjini Cairo, Misri mwaka 1994 na zipi changamoto, sasa katika tathimini ile ikaonekana kwamba kuna mambo ambayo bado ni changamoto ikiwamo udhibiti wa vifo vya kina mama vinavyotokana na uzazi, mabinti kupata mimba katika umri mdogo, kuendelea kushamili kwa vitendo vya kikatili Kusini mwa Jangwa la Sahara na upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi.

“Baada ya mkutano huo nchi mbalimbali zilitoa maazimio juu ya kile watakachokifanya, hivyo ikaanzishwa Kamisheni ya kupokea taarifa za mara kwa mara za utekelezaji ambayo Rais mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete alichaguliwa kuwa Mwenyekiti Mwenza.

“Hivyo kwa mara hii Tanzania imepata bahati ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu utakaofanyika visiwani Zanzibar kuanzia Novemba 9 hadi 11, kwa ajili ya pokea taarifa hiyo ya Kamisheni ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa Nairobi mwaka 2019,”amesema Hangwa.

Awali, akifungua mkutano na Waandishi wa Habari, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA Tanzania, Mack Bryan Schreiner mbali na kuhimiza umuhimu wa vyombo vya habari kuupa kipaumbele mkutano huo, pia alisema mkutano wa Nairobi ulipata uungwaji mkono ili kufikia matokeo matatu ya mageuzi, ndani ya miaka 10.

“Hizi ni: Sifuri ya vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika, sifuri ya hitaji lisilofikiwa la upangaji uzazi na sifurifu ukatili wa kijinsia na mila hatarishi (FGM na ndoa za utotoni), tunatambua kwamba serikali ya Tanzania ilipitisha Mpango wa Utendaji wa ICPD, na ikatoa ahadi katika ICPD25.

“Tunasisitiza kwamba UNFPA inalenga kuunga mkono serikali ya Tanzania ili kuharakisha maendeleo kuelekea ahadi hizi za ICPD25. Aidha, katika kuunga mkono mchakato wa ICPD, nina furaha kueleza kuwa katika wiki ijayo tutakaribisha wageni maalum na wa ngazi ya juu kwenye mkutano utakaofanyika Zanzibar.

“Wageni mbalimbali watakuwepo kwa ajili ya kupeleka ahadi za kimataifa kuhusu afya ya uzazi wakiwamo wajumbe wa Tume ya Ngazi ya Juu ya Mkutano wa Kilele wa Nairobi wa Ufuatiliaji wa ICPD25. Tume ya Ngazi ya Juu ina jukumu la kufuatilia, kuripoti na kutoa mapendekezo kuhusu maendeleo ya ahadi za ICPD25.

“Hivyo, katika mkutano huu watawasilisha ripoti ya pili ya mwaka ya ufuatiliaji wa ahadi za mkutano wa Nairobi ambapo Wenyeviti wenza wa Tume ya Ngazi ya Juu ni Dk. Kikwete, Michaëlle Jean, Gavana Mkuu wa zamani na Kamanda Mkuu wa Canada,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles