28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo roli la mafuta, watoto vilivyoacha taharuki 2019

Na AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

ULIANZA mithili ya nyota ya asubuhi ambayo hung’aa na kila mtu anapoiona hufurahi na kupata matumaini mapya kama inavyofahamika kuwa ‘nyota njema huonekana asubuhi’.

Zilipigwa ngoma na kelele za shangwe katika mitaa mbalimbali duniani huku kila mtu akimshukuru Mungu kuuona mwaka mwingine ambao wengi wao walitabiri utakuwa wa mafanikio kwao.

Viongozi mbalimbali wa dini nao walisimama madhabahuni na kuwaongoza waumini wao ibada ya kumshukuru Mungu kwa kuwafiki- sha salama mwaka mpya.

Licha ya hayo yote lakini sasa tunasema hakuna chenye mwanzo kisichokuwa na mwisho, hivi ndivyo inavyoonekana kwa mwaka huu wa 2019 ambao unaelekea ukingoni baada ya safari ndefu ya miezi 12.

Mwaka 2019 si haba kutokana na vitu vingi vya maendeleo vilivyofanyika hasa kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ambayo imejitahidi kujenga miundombinu na kuimarisha uchumi wa nchi.

Si safari rahisi kwani licha ya mafanikio pia kuna matukio am- bayo yameweza kutikisa jamii kwa kuleta hisia tofauti.

Yapo matukio yaliyoonesha furaha baina ya watu na yapo ambayo yalileta huzuni katika jamii.

Waswahili husema mbio za sakafuni huishia ukingoni swali ni kwamba je, mbio hizo zilishia pazuri au pabaya? majibu anayo kila mmoja kwa jinsi anavyoumaliza mwaka.

Makala haya yanaangazia matukio mbalimbali ya kijamii yaliyotokea mwaka huu.

MAUAJI YA WATOTO NJOMBE

Tuliianza Januari kwa safari ya matumaini mapya lakini katika mwezi huo yalitokea matukio ambayo yalileta simazi kwa jamii na aibu kwa Taifa.

Matukio hayo ni ya mauaji ya watoto yaliyoanza Novemba mwaka jana na kuja kutikisa Januari mwaka huu baada ya mauaji kuendelea kuongezeka.

Katika matukio hayo ya mauaji ambayo yalikuwa yakihusishwa na imani za kishirikina jumla ya watoto 10 walitekwa na kuuawa kisha kunyofolewa viungo vikiwamo sehemu za siri na masikio.

Kutokana na vitendo hivyo hofu ilitanda katika Mkoa wa Njombe kutokana na wazazi kuhofia maisha ya watoto wao huku wakiacha shughuli zingine na kuwapeleka watoto shule na kwenda kuwachukua.

Katika Kijiji cha Ikundo watoto watatu wa familia moja Oliva Nziku (11), Gasper Nziku (8) na Giliadi Nziku (5), waliuawa na miili yao kutelekezwa msituni.

Kutokana na mauaji hayo mtu mmoja aliuawa na wawili kujeruhiwa na wananchi katika Kijiji cha Magunguli Kata ya Kibaoni baada ya kuhisiwa kuwa ni miongoni mwa wanaojihusisha na utekaji wa

watoto, watu hao walikuwa wageni. Serikali ililaani vitendo hivyo vya aibu na kuahidi kukomesha mauaji hayo kwa kuwasaka washukiwa mbalimbali.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) kwa pamoja waliungana na Serikali kulaani na kukemea mauaji hayo.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa nusu mwaka 2018, kumekuwa na ongezeko la ukatili dhidi ya watoto ambapo jumla ya matukio 6,376 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa.

Ripoti hiyo pia inatanabaisha kwamba katika kipindi cha Januari hadi Juni 2018 watu 17 waliuawa kwa sababu ya imani za kishirikina ambapo hadi kufikia Juni 2018 jumla ya watu 106 waliuawa.

WAFANYAKAZI WA AZAM

Julai 8 mwaka huu ambapo tasnia ya habari ilipata pigo baada ya kuondokewa na waandishi wa habari watano na madereva wawili kutoka Azam Media.

Ilikuwa simanzi nzito kwa waandishi wa habari na Watanzania wote kwa ujumla kwa namna walivyoguswa na msiba huo.

Ajali hiyo ilitokea Shelui mkoani Singida na kuhusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso. Wafanyakazi hao wa Azam TV walikuwa njiani kwenda kurusha matangazo mubashara ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato.

Wafanyakazi wa Azam TV waliofariki kwenye ajali hiyo ni Salim Mhando (muongozaji wa matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi.

Wengine wawili waliofariki ni dereva wa gari ambalo Azam TV Walilikodi pamoja na msaidizi wake.

Katika ajali hiyo wafanyakazi watatu wa Azam TV walijeruhiwa ambao ni ambao ni Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde.

VIFO LORI LA MAFUTA

Tukio hili lilileta simazi si tu kwa Tanzania bali dunia nzima.

Asubuhi ya Agosti 10 lori lililobeba mafuta lilipata ajali eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kusababisha mafuta kumiminika.

Baadhi ya watu walisogelea eneo hilo la ajali wakijaribu kucho- ta mafuta yaliyokuwa yakimiminika wengi wao wakisadikika kuwa ni madereva bodaboda.

Muda mfupi baadaye gari hilo lililipuka na kuwaka moto ambao pia uliwapata watu waliokuwa wanachota mafuta hayo.

Jumla ya watu 104 walipoteza maisha katika ajali hiyo na ambapo zaidi ya 60 walipoteza maisha papo hapo huku wengine 70 wakijeruhiwa vibaya.

Majeruhi wenye hali mbaya ambao walikuwa 46 walipelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hata hivyo idadi ya vifo iliendelea kuongezeka na walibaki majeruhi 11 huku watatu wakiruhusiwa kutoka hospitali.

Ajali hiyo ni msiba mkubwa wa taifa kwa mwaka huu kutokana na madhara yaliyotokea na vifo vingi.

Serikali ilitangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa na bendera zote zilipeperushwe nusu mlingoti kwa siku tatu.

Agosti 11 Rais Magufuli aliwatembelea majeruhi waliokuwa wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbi na kuahidi Serikali kugharamia matibabu yao.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliongoza umati wa wananchi mkoani Morogoro katika mazishi ya waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo.

Mazishi hayo yalifanyika katika eneo la makaburi la Kola Hill mkoani Morogoro.

WATU MASHUHURI

Mwaka huu pia Taifa lilipoteza watu mashuhuri na waliokuwa wakiwasaidia vijana na jamii kwa njia mbalimbali.

Februari 26 aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalilishaji Clouds Media Group, Ruge Mutahaba (49), alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu Afrika Kusini.

Habari hizo zilikuwa simanzi kubwa masikoni mwa Watanzania hasa vijana kwa sababu bado walikuwa wanahitaji malezi yake hasa katika kukuza vipaji.

Wakati mwili wake unapitishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwenda Mikocheni wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam walitembea kwa miguu wakiusindikiza huku wengine wakilia kwa uchungu.

Kutokana na Ruge kuibua vipaji vingi hasa vya uimbaji wasanii walitunga wimbo wa kumuenzi na kumuombea katika safari yake ya mwisho waliouita ‘Asante Baba’.

Wasanii walioimba ni pamoja na Barnaba, Lina, Pipi, Ditto, Amini wengi wao waliokuwa Tanzania House of Talent (THT) iliyoanzish- wa na Ruge. Ruge alizikwa kijijini kwao Bukoba.

Kifo kingine kilichoshtusha jamii ni cha mfanyabiashara maarufu Dk. Reginald Mengi (75) ambaye alifariki Mei 2 akiwa katika nchi za Falme za Kiarabu.

Kifo chake kilikuwa pigo si tu kwa familia yake bali hata kwa Watanzania hasa vikundi vya kinamama, wenye ulemavu kutokana na kuwasaidia.

Katika tasnia ya habari Dk. Mengi alikuwa msaada mkubwa kutokana na kuajiri wanahabari wengi katika vyombo vyake vya habari yaani magazeti, redio na televisheni.

Rais Magufuli alisema; “Nimehuzunishwa na habari za kifo cha mengi, siku zote nitamkumbuka kwa mchango wake wa maendeleo ya nchi yetu na mtazamo wake alioundika katika kitabu chake, ‘I can, I will, I must”.

Mbali ya vyombo vya habari Mengi pia ana kampuni ya maji ya kunywa na alikuwa akijihusisha na biashara ya uchimbani madini ya urani, shaba na makaa.

Mwaka 2014 aliwekwa nafasi ya 50 miongoni mwa watu matajiri kabisa barani Afrika akikadariwa kumiliki utajiri wa takribani Dola milioni 560.

Taarifa nyingine ya kifo ni ile ya Desemba 8 ambapo mfanyabia- sha mkubwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Infotech Investment Group, Ali Mafuruki, alifariki dunia Afrika Kusini wakati akipatiwa matibabu.

Kupita ukurasa wake wa Twiter Rais Magufuli alisema; “Nimehu- zunishwa na taarifa za kifo cha rafiki yangu Ali Mufuruki (Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni CEOrt).

“Nitamkumbuka kwa uzalendo na mchango wake katika kukuza sekta ya biashara na ushauri kwa Serikali. Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un.

Mufuruki ambaye alikuwa akisumbuliwa na homa ya mapafu alifariki akiwa na miaka 60 na alizikwa katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

BIMA YA AFYA


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Anne Makinda, akikata utepe wakati wa uzinduzi wa vifurushi vipya vya bima ya afya. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard Konga na kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, Tryphone Rutazamba na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba.

Novemba 28 mwaka huu Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) ulizindua vifurushi vipya vya aina tatu vya Najali afya, Timiza Afya na Wekeza Afya.

Vifurushi hivyo ni mpango wa kuwarahisishia wananchi kupata huduma za matibabu kwa haraka bila usumbufu.

Katika vifurushi hivyo mtu wa kuanzia umri wa miaka 36 hadi
59 atachangia Sh 240,000 kwa kifurushi cha Najali, Sh 444,000 kwa kifurushi cha Wekeza na Sh 612,000 kwa kifurushi cha Timiza. Kwa mchangiaji wa miaka 60 na kuendelea atachangia Sh 360,000 kwa Najali, Sh 660,000 kwa Wekeza na Sh 984,000 kwa Timiza.

Hata hivyo wananchi waliomba kupunguziwa gharama na baadhi ya vizuizi vilivyowekwa hasa kwa magonjwa yenye gaharama kubwa kama saratani, moyo figo na mengineyo.

Akijibu hoja za Wananchi Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema hata yeye aliona kuna haja ya vifurushi hivyo kuendelea kuboreshwa na kuwekwa magonjwa hayo yenye gharama kubwa.

Waziri Ummy aliutaka mfuko huo wa bima kuendelea kusikiliza maoni ya wananchi na kuboresha vifurushi hivyo.

Pia alisema gharama za vifurushi hivyo zitapungua wakati sheria ya matumizi ya lazima ya bima ya afya itakapopitishwa na Bunge mwanzoni mwa Februari mwakani.

KUFUFULIWA TRENI YA ABIRIA

Katika kipindi cha mwisho wa mwaka watu wengi hasa wa mikoa ya Kaskazini hupenda kwenda kusherehekea sikukuu majumbani mwao.

Hatua hiyo imekuwa ikileta adha ya usafiri kutokana na idadi ya abiria kuwa kubwa huku kukiwa hakuna magari ya kutosha.

Treni ambayo ilisimama kwa miaka 25 ilianza upya safari zake Desema 7 kwa kubeba abiria kutoka Dar es Salaam hadi Moshi.

Kuwepo wa treni hiyo katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka kumekuwa mkombozi mkubwa baada ya kupunguza msongamano katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo.

Gharama za usafiri kupitia treni hiyo pia zimekuwa za chini kulin- gana na madaraja ambayo abiria atachagua.

Kwa mfano kutoka Dar es Salaam hadi Korogwe kwa daraja la tatu nauli ni Sh 10,700, daraja la pili kukaa (Sh 15,300) na kwa daraja la tatu kulala (Sh 25,400).

Kwa upande wa safari za kutoka Dar es Salaam hadi Moshi daraja la tatu ni Sh 16,500, daraja la pili (Sh 23,500) na daraja la tatu kulala (Sh 39,100).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles