30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Vifo majeruhi ajali lori la mafuta vyafikia 97

Aveline Kitomary, Bosco Mwinuka, Neema Sigaliye Na Faustine Madilisha (TUDARCO) -Dar es salaam

MAJERUHI wawili kati ya 20 wa ajali ya lori la mafuta lililoanguka na kuwaka moto mkoani Morogoro, waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamefariki dunia.

Vifo hivyo vimefanya jumla watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo hadi sasa kufikia 97.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Muhimbili, Aminieli Aligaesha, alisema idadi ya majeruhi waliobaki hospitali hapo ni 18 na wote wako katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).  

Aligaesha alisema majeruhi waliofariki dunia ni Rosijo Mollel (35) na Neema Chakachaka (30), hivyo idadi ya majeruhi waliofariki wakiwa hospitalini hapo kufika 29.

“Majeruhi wawili wamefariki dunia, kuna Rosijo Mollel ana miaka 35 ambaye aliletwa juzi kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro, huyu alifariki jana mchana saa nane na Neema Chakachaka alifariki saa 11:30 alfajiri ya leo (jana), huyu alilazwa ICU iliyopo jengo la wazazi.

“Kati ya majeruhi 47 walioletwa hapa, wamebaki 18 na wote wako ICU. Waliopo ICU ya Mwaisela wapo 14, mtoto mmoja yupo ICU ya watoto na wengine watatu wako ICU ya HDU Mwaisela, mpaka sasa majeruhi waliopoteza maisha wakiwa hapa hospitali wamefikia 29,” alisema Aligaesha.

Alisema Hospitali ya Muhimbili inaendelea kutoa huduma kwa majeruhi waliobaki ili waweze kurejea katika hali nzuri.

“Bado tunaendelea kupambana, madaktari wetu na wale wa JWTZ wanaendelea kuwapatia matibabu majeruhi hawa ili waweze kurejea katika hali nzuri,” alisema Aligaesha.

Wakati huohuo, uchangiaji damu hospitalini hapo umepungua baada ya mwitikio wa watu jana kuwa mdogo.

Akizungumza na MTANZANIA jana Daktari wa Kitengo cha Utoaji Damu, Dk. Judith Kayombo, alisema uchangiaji damu kitaifa ulimalizika juzi na kwamba kwa sasa huduma hiyo inaendelea kwa watu kuchangia damu kwa ndugu zao.

“Zoezi la uchangiaji damu kwa taifa  lilimalizika Jumapili, kwa sasa tunaendelea na uchagiaji damu kwa wale wenye wagonjwa wanaohitaji damu na wachangiaji wa kujitolea, ndiyo maana mwitikio ni mdogo,” alisema Kayombo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles