30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

VIFAA VYA PLASTIKI VINASAMBAZA SARATANI, VIEPUKWE

JUMANNE wiki hii katika toleo la gazeti hili tuliripoti kuwa imebainika kwamba vifaa vya plastiki hutengeneza kemikali zaidi ya 200, hivyo kuwa chanzo cha aina 100 za ugonjwa wa saratani.

Vifaa hivyo vya plastiki ni pamoja na mifuko ya rambo, bakuli, vikombe na vifaa vya kuhifadhia chakula (makontena).

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Marafiki wa Watoto wenye Saratani Tanzania, Walter Miya,

matumizi ya plastiki yanazidi kuongezeka nchini, ugonjwa wa saratani nao umeongezeka, hasa kwa upande wa akina mama.

Kwamba ugonjwa wa saratani umekuwa ukiharibu ukuaji wa mfumo wa uzazi, hususani kwa watoto ambao bado kuzaliwa, mabadiliko ya kijenetiki na kushindwa kuona vizuri.

Kupitia utafiti uliofanywa, asilimia 60 za saratani zimesababishwa na matumizi ya vifaa vya plastiki.

Kwamba watu wengi wamekuwa wakitumia vifaa vya plastiki bila kujua madhara yake. Wanawake wengi wamekuwa wanachemsha maji na kuyahifadhi katika ndoo za plastiki yakiwa bado ya moto.

Baada ya muda ukija kuchunguza ile ndoo utakuta ina mabaka mabaka, maana yake imeshatoa kemikali nyingi na kuingia katika yale maji na athari haionekani mpaka ifike miaka 10 au 15; na si rahisi kugundua saratani hiyo imesababishwa na nini!

Mamantilie wengi pia hufunika sufuria za mchele au ndizi zinazochemshwa kwa kutumia mifuko ya plastiki au rambo ambazo hutoa kemikali na kuziingiza kwenye chakula.

Tunasema jamii inapaswa kupunguza matumizi ya plastiki kutokana na madhara yaliyomo katika vifaa hivyo.

Tunasema vilevile watu wachemshao maji wasubiri hadi yapoe ndipo wayamimine kwenye ndoo.

Tunapendekeza kuwapo kwa sera na sheria dhidi ya matumizi ya plastiki kutokana na kukithiri kwa vifaa hivyo ambavyo vimekuwa vikitengenezwa kila kukicha viwandani.

Tunadhani Serikali inapaswa tena kuwa makini na kila kitu inachoamua kukifanya ili kuwa Serikali inayoaminiwa na watu.

Mwaka jana mwishoni ilipiga marufuku uingizaji na usambazaji wa mifuko ya plastiki.

Kwamba Serikali ilikuwa inaendelea na mchakato wa kutafuta vifungashio mbadala badala ya kutumia mifuko hiyo ambayo imekuwa ikichangia uchafuzi wa mazingira nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (Muungano na Mazingira),  kwamba kuanzia Januari mwaka huu (2017) kusingekuwa na uingizaji, usambazaji   na utengenezaji wa mifuko ya plastiki  nchini.

Mifuko ya plastiki imekuwa kwa muda mrefu changamoto kubwa ya mazingira kutokana na kutolewa bure, hivyo kusababisha kuzagaa ovyo mitaani.

Kwamba nia ya Serikali ilikuwa kuweka zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki ndani ya sheria, na hii pia ilihusu matumizi ya mifuko ya plastiki kufungashia pombe, maarufu kwa jina la viroba.

Asilimia kubwa ya uchafu kwenye vyanzo vya maji hasa mito, maziwa na fukwe za bahari inatokana na mifuko ya plastiki.

Tunasema sasa ni mwezi Machi na hakuna kilichofanyika kuhusu Serikali ilichosema kuzuia.

Tunasisitiza kuwa hatua hii ya Serikali imechelewa kwani Serikali ya Zanzibar ilikwisha kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki na matokeo mazuri kuanza kuonekena.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles