25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

VIDONGE VYA UZAZI WA MPANGO VINAWEZA KUTIBU CHUNUSI

Vidonge vya uzazi wa mpango

NA JOACHIM MABULA,

VIDONGE vya uzazi wa mpango ni njia madhubuti ya kuzuia mimba vikitumiwa vizuri na kwa usahihi. Kila mwaka asilimia 8 ya wanawake hupata ujauzito wasioutegemea wakiwa kwenye njia hii ya uzazi wa mpango, mara nyingi ni kwa sababu wengi husahau kumeza vidonge.

Hata hivyo, vidonge vya uzazi wa mpango vikinywewa kila siku muda ule ule, mwanamke mmoja pekee kati ya 100 anaweza kupata mimba isiyotarajiwa ndani ya mwaka wa kwanza wa matumizi ya dawa za uzazi wa mpango. Kuna aina kuu mbili za vidonge vya uzazi wa mpango, zote zina homoni (vichocheo) zilizotengenezwa ziitwazo Estrojeni na Projesteroni.

Estrojeni ni homoni inayotengenezwa na uterasi/kizazi ambayo husaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi, kwa kuongoza ukuaji wa kuta za uterasi kwenye sehemu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi. Projesteroni ni homoni ya kopasi luteamu ya ovari ambayo huanzisha mabadiliko katika endometriumu kufuatia ovulesheni.

Kuna vidonge vina homoni zote mbili na vidonge vyenye homoni/kichocheo moja/kimoja tu ya Projesteroni. Vidonge vyenye kichocheo kimoja cha Projesteroni vinafanya kazi kwa kufanya ute mzito kwenye shingo ya mji wa mimba na kuzuia kupevuka kwa yai. Vidonge hivi huzuia mimba kwa kiwango cha asilimia 99 na ni salama.

Vidonge vyenye vichocheo viwili vya Estrojeni na Projesteroni vinafanya kazi kwa kuzuia kupevuka kwa yai, hufanya ukuta wa kizazi kuwa mwembamba na hufanya ute mzito kwenye shingo ya nyumba ya uzazi. Vidonge hivi huzuia mimba kwa kiwango cha asilimia 99 kama vitatumika kwa usahihi.

Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza pia kutumika kitiba mfano kuweka sawa mzunguko wa hedhi, kuzuia maumivu makali wakati wa hedhi, kutibu chunusi, kupunguza hatari ya magonjwa katika via vya uzazi. Dawa za uzazi wa mpango hazizuii magonjwa ya ngono.

ATHARI  ZA MATUMIZI YA VIDONGE VYA UZAZI WA MPANGO

Kutokwa na damu ukeni baada ya hedhi ya kawaida. Hali hii huwapata asilimia 50 ya wanawake wote wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango, hali hii hutokea zaidi ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza dawa hizi. Kiujumla, hali hii huisha kwa zaidi ya asilimia 90 ya wanawake wakianza kutumia pakti ya tatu ya dawa katika kipindi hiki cha kutokwa damu, kidonge cha uzazi wa mpango kina uwezo mkubwa endapo kitatumika kiusahihi. Inashauriwa kuwasiliana na mhudumu wa afya kama utatokwa damu kwa siku tano au zaidi wakati ukiwa unatumia dawa kwa siku tatu au zaidi.

Kichefuchefu: Kichefuchefu kidogo hutokea mwanzoni baada ya kuanza kumeza vidonge vya uzazi wa mpango. Hata hivyo, hali hii huisha baada ya siku chache. Ikiwa utapata kichefuchefu zaidi wasiliana na mhudumu wa afya.

Matiti kujaa na kuuma: Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza kusababisha matiti kujaa na kuwa na maumivu pindi yanapoguswa, dalili hii huanza kupungua ndani ya wiki za kwanza baada ya kutumia vidonge hivi. Hata hivyo, kukiwa na uvimbe au maumivu yasiyoisha tafuta msaada wa kitiba. Kupunguza matumizi ya kafeini na chumvi kunaweza kupunguza maumivu ya matiti, kama tu ilivyo kwa kuvaa brauzi isiyobana matiti.

Maumivu ya kichwa: Kwa kuwa kuumwa kichwa kunaweza kuwa dalili za magonjwa mengi, ikiwa maumivu mapya ya kichwa yataanza baada ya kumeza  vidonge vya uzazi wa mpango ni vyema kutoa taarifa kwa mhudumu wa afya.

Kuongezeka uzito: Ingawa tafiti zimeshindwa kuthibitisha ni jinsi gani vidonge vya uzazi wa mpango vinasababisha mabadiliko ya uzito, baadhi ya wanawake hupatwa na tatizo la maji kuganda kwenye matiti na maeneo ya nyonga.

Mabadiliko ya hisia: Kama una historia ya kushuka moyo (Depression) ni muhimu kumjulisha mhudumu wa afya ili kuweza kujadili ni jinsi gani utatumia dawa zako, pia ni muhimu kuwasiliana na mhudumu wa afya kama unapatwa na mabadiliko ya hisia wakati ukitumia vidonge vya uzazi wa mpango.

Kutokwa na uchafu ukeni: Baadhi ya wanawake hutokwa na uchafu ukeni, pia kuna uwezekano wa kupungua au kuzidi kwa ute wakati wa tendo la ndoa. Ni vyema kuzungumza na mhudumu wa afya juu ya dalili unazopata ili kuweza kugundua kama kuna maambukizi au la.

Kukosa hedhi: Kuna wakati bila kujali umetumia vidonge kwa usahihi unaweza kuruka au kukosa hedhi kabisa. Kuna vingi vinaweza kusababisha hali hii pia, pamoja na msongo wa mawazo (Stress), magonjwa, safari au wakati mwingine ni matatizo ya homoni. Ni vyema kupima mimba endapo utakosa siku zako ingawa unatumia vidonge vya uzazi wa mpango, ikiwa hali ya kukosa hedhi itaendelea ni jambo la busara kuzungumza na mtoa huduma.

Kupungua hamu ya tendo la ndoa: Vidonge vya uzazi wa mpango vinaweza kuathiri utendaji wa tendo la ndoa kutokana na homoni zilizomo ndani yake. Hata hivyo, kuna vitu vingine vinaweza sababisha tatizo hili kama kisukari, shinikizo kubwa la damu. Tatizo hili likizidi mtaarifu mhudumu wa afya.

Mabadiliko ya taswira kwa wale wanaovaa miwani ya macho: Ni vyema kumuona daktari wa macho ikiwa ni mtu unayevaa miwani na umeona mabadiliko katika taswira wakati unatumia vidonge vya uzazi wa mpango.

TAHADHARI KABLA NA BAADA YA KUTUMIA VIDONGE

Ikiwa kwa wakati mmoja utapata dalili kama maumivu ya tumbo, kifua (pumzi ya shida), kichwa kuuma, kuona maluelue, kuvimba na kuuma kwa miguu baada ya kumeza vidonge vya uzazi wa mpango, haraka wasiliana na mtoa huduma za afya au fika hospitali haraka.

Ikiwa utaharisha au kutapika tumia njia ya kondomu kipindi chote mpaka utakapopona na uongeze siku mbili zaidi. Baadhi ya dawa hupunguza nguvu na ufanisi wa vidonge kama dawa za kifua kikuu (Rifampicin) au dawa za kifafa hivyo ni vyema kumtaarifu mhudumu wa afya ili akuchagulie njia ya uzazi wa mpango itakayokufaa.

Vidonge vya uzazi wa mpango pia vinahusishwa na kupanda kwa shinikizo la damu, saratani ya ini na kuongeza hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. Vidonge vyenye homoni/vichocheo mbili/viwili huwa na hatari za matatizo ya moyo kama mshtuko wa moyo (heart attack), kiharusi (stroke) na mgando wa damu kwenye mishipa, yanayoweza kusababisha kifo. Kwa wanawake wenye historia ya mgando wa damu kwenye mishipa, mshtuko wa moyo au kiharusi, inashauriwa wasitumie vidonge vyenye homoni/vichocheo mbili/viwili na ni vyema kuzungumza na mtoa huduma juu ya njia mbadala za uzazi wa mpango.

Haishauriwi kutumia vidonge vya uzazi wa mpango ndani ya wiki tatu baada ya kujifungua, ikiwa unanyonyesha mtoto umri chini ya miezi sita, ikiwa umefanyiwa upasuaji mkubwa karibuni, ikiwa  mwanamke unavuta sigara mwenye umri zaidi ya miaka 35, una historia ya ugonjwa wa ini & manjano, moyo, tumbo la uzazi, saratani ya matiti, shinikizo la damu linalobadilika badilika kila wakati (140/90 au zaidi) au maumivu makali ya kichwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles