NYOTA wa timu ya Taifa ya Chile, Arturo Vidal, amekanusha madai kwamba anataka kujiunga na klabu ya Chelsea mwishoni mwa msimu huu.
Kiungo huyo wa klabu ya Bayern Munich, ilidaiwa kwamba ana lengo la kutaka kujiunga na klabu za nchini England baada ya kumalizika kwa msimu huu, hasa timu ya Chelsea, lakini mchezaji huyo amedai ana furaha na maisha ya Bavaria.
“Nina furaha kubwa kuwa mchezaji wa Bayern Munich, ni klabu kubwa duniani, hivyo sioni sababu ya kutafuta klabu nyingine, labda uongozi ukiwa hauna mpango wa kunipa mkataba mpya baada ya kumalizana nao.
“Kuna habari ambazo zinadai kwamba natarajia kujiunga na klabu za England baada ya msimu huu, napenda kuweka wazi kwamba hakuna ukweli huo, nitaendelea kuwa mchezaji wa Bayern hadi mkataba wangu utakapomalizika 2019.
“Nilikuwa karibu na kocha Antonio Conte, ambaye anatarajia kujiunga na Chelsea baada ya kumalizika msimu huu, lakini siwezi kumfuata kule ambako anakwenda kwa kuwa maisha ni sehemu yoyote na hapa nilipo najua kwamba ni sehemu sahihi kwangu,” alisema Vidal.
Mchezaji huyo aliisaidia klabu yake kushinda bao 1-0 dhidi ya Benfica katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku bao hilo akilifunga yeye na kuipa nafasi ya kujiamini katika mchezo ujao wa marudiano.