22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

VETA Arusha kuboresha mafunzo ya utalii

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo cha VETA cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii kilichopo Njiro jijini Arusha kimejipanga kuboresha mafunzo ya kuongoza watalii hasa katika eneo la vivutio vipya ili wageni wanaokuja Tanzania waweza kukaa muda mrefu.

Akizungumza na Mtanzania Digital kwenye maonyesho ya Sabasaba, Mwalimu wa mafunzo ya kuongoza watalii katika chuo hicho Ludovic Saronga, amesema chuo hicho ni pekee katika VETA kinachotoa mafunzo hayo ambayo yamesaidia vijana wengi kuajiriwa na wengine kujiajiri.

“Kwenye maonyesho haya ya Sabasaba tumekuja na kitu kipya kwa sababu kihistoria Tanzania tulikuwa tukiuza utalii wa wanyamapori, milima na fukwe. Wageni wengi wamekuwa wakikaa kati ya siku nane mpaka 12 wanaondoka na kurudi makwao lakini haina maana kwamba fedha zimeisha…wanazo ni ‘activities’ hatuna za kuwafanya wakae zaidi.

“Kwahiyo tunahitaji kuongeza vivutio zaidi ili watalii wanaokuja Tanzania waweze kukaa muda mrefu, jinsi wanavyokaa muda mrefu ndivyo jinsi tunavyokusanya fedha kutoka kwao,” amesema Saronga.

Amesema utalii wa utamaduni ni aina mpya ya vivutio na kwamba wageni wataweza kwenda katika kaya mbalimbali kuangalia nyumba wanazotumia, namna wanavyofuga, wanavyolima na jinsi wanavyoandaa vyakula.

“Mfano kwenye chakula wataona mama anakamata bata anachinjwa anaandaliwa, kama ni mboga za majani zinachumwa anaziona, kama ni ndizi mkungu unakatwa anauona kwahiyo mgeni anakula vitu halisi kabisa.

“Hii itawafanya badala ya kuondoka watakuwa na siku nyingine moja au mbili hata tatu kutembelea kaya, aina hii ya biashara itawafanya vijana wa eneo husika kuongoza watalii kwahiyo tutakuwa tumetengeneza ajira vijijini na kupunguza wimbi la wanaokuja mjini kutafuta kazi kwa sababu tumewafungulia soko la ajira kulekule,” amesema.

Pia amesema wameweka mikakati ya kuwasaidia vijana wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye uziwi ili wasibaki nyuma na kuwa tegemezi.

“Tumekuwa tukiwapa nafasi ya kupata ujuzi kwa sababu hili kundi ni kama limeachwa nyuma, tumegundua kwamba vijana hawa wako wengi tutaweka mikakati ili wasibaki nyuma waje VETA tuwape ujuzi tunataka nao wachangie uchumi wasiwe tegemezi,” amesema Saronga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,283FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles