NA BADI MCHOMOLO
UMRI haudanganyi! Ndio unaweza kusema hivyo kwa bingwa namba moja wa zamani wa mchezo wa tenisi duniani, Venus Williams.
Huyo ni mchezaji ambaye aliwahi kufanya makubwa kwenye mchezo huo, Februari 25, 2002 alitajwa kuwa ni bora duniani kwa upande wa wanawake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 37, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 22, ushindani mkubwa alikuwa anaupata kutoka kwa mdogo wake Serena Williams.
Wakati huo Serena alikuwa na umri wa miaka 20, hao ni wachezaji ambao walikuwa wanasumbua kwenye mchezo huo kwa upande wa wanawake, waliweza kuteka hisia za mashabiki hasa pale walipokuwa wanakutana wawili hao fainali.
Venus hakuweza kudumu sana kwenye nambo moja ya ubora wake, alikaa kwa miezi minne kabla ya mdogo wake Serena kuja kuchukua nafasi huyo Julai 8 mwaka huo huo.
Leo hii bado wawili hao wanasumbua kwenye mchezo huo, mwaka jana Serena aliibuka bingwa wa michuano ya Wimbledon na kushika nafasi ya kwanza kwa ubora duniani kwa wanawake.
Hata hivyo baada ya taji hilo alitangaza kupumzika kwenye mchezo huo kutokana na kujiandaa kupata mtoto kwa kuwa ni mjamzito, hivyo alishindwa kushiriki baadhi ya michuano na hatimaye kuangukia nafasi ya 15 kwa ubora.
Venus yeye kwa sasa anashika nafasi ya 9, lakini uhakika wa kurudi nafasi ya kwanza kama ilivyo mwaka 2002 ni kazi kubwa kutokana na ushindani.
Alikuwa na nafasi ya kushika nafasi ya juu zaidi endapo angefanikiwa kutwaa namba moja kwenye michuano ya Wimbledon ambayo imemalizika wiki moja iliopita, huku bingwa kwa wanawake akichukua Garbine Muguruza raia wa nchini Hispania, mwenye umri wa miaka 23, wakati kwa wanaume akichukua Roger Federer.
Venus kufika fainali ni nafasi kubwa kwake kwa sasa kutokana na ushindani, lakini ingekuwa na faida kubwa endapo angefanikiwa kutwaa taji hilo la Wimbledon.
Alishindwa kuonesha ubora wake mbele ya mpinzani wake ambaye amemuacha miaka 14, hapo ndipo unaweza kuamini kuwa umri wa Venus unamtupa mkono.
Kutokana na umri alionao na ushindani anaoupata itampa wakati mgumu wa kupata nafasi ya kufika fainali kwenye michuano mikubwa na kurudi kwenye nafasi yake ya kwanza.
Ni wakati wake sasa wa kuangalia maisha baada ya tenisi, japokuwa sio jambo rahisi sana kulikubali kwa sasa lakini lazima iwe hivyo ili kulinda heshima yake.
Hasipofanya hivyo wachezaji wengi ambao wanafanya vizuri kwa sasa kama vile Johanna Konta, Angelique Kerber, Garbine Muguruza na wengine wengi, watamsumbua.
Ni wakati wake sasa wa kustaafu ili aweze kulinda heshima ya mchezo huo, bado uwezo anao lakini sio wa kushindana na damu changa.
Hata Venus mwenyewe alimwelezea mdogo wake Serena kwamba ushindani ni mkubwa na kuna wimbi kubwa na wachezaji ambao wana uwezo wa hali ya juu.
“Unaendeleaje Serena, nilikumisi sana, lakini kama ulivyoona, nilijaribu kupambana kwa hali na mali lakini sikuweza kutimiza malengo yangu.
“Ushindani ni mkubwa sana kwa sasa na hata kufika fainali nilijitahidi sana, wachezaji wengi wana umri mdogo na uwezo wao ni mkubwa sana,” Venus alimwambia Serena