28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Vazi linaloweza kukuzuia kuingia mahakamani

img_0562

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

KILA mwananchi anayehitaji kupata haki yake anaruhusiwa kufika mahakamani kuisaka haki hiyo.

Mahakamani ni mahali ambako kila mmoja anaruhusiwa kufika na kupata huduma anayoihitaji hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuzuia mtu kufika eneo hilo.

Haki hiyo ya kufika mahakamani inatumika vibaya pale ambapo wanaofika eneo hilo wanakuwa katika mtazamo usioheshimu eneo hilo.

Watu wamekuwa wakifika mahakamani wakiwa wamevaa suruali zinazoanzia chini ya makali, maarufu mlegezo kwa wanaume, wanawake wanavaa nguo fupi kupita kiasi na wengine zinazobana na kuonyesha mwili.

Uongozi wa mahakama umeliona hilo na kuweka matangazo ya maelekezo kwamba nguo za aina hiyo haziruhusiwi hivyo ukijiona umevaa hutaruhusiwa kufika eneo hilo.

Walinzi getini wamekuwa wakizuia wanaofika wakiwa wamevalia nguo za kubana na wengine fupi, wenye khanga kwenye mikoba wanaamua kufunga ili waingie mahakamani.

Inawezekana wananchi hawajui mavazi yanayoruhusiwa kuvaa katika eneo hilo, lakini hata wale wanaofika mara kwa mara mahakamani wamekuwa wakionekana wakivaa nguo fupi na wengine za kubana.

Tunajua kwamba mahabusu waliopo gerezani kuna mahitaji ya lazima ambayo hawapati kutokana na utaratibu uliowekwa.

Hili halihitaji elimu, wanawake waliovalia nguo fupi ama za kubana na kuonyesha maumbile wanaweza kukaa vipi mahakamani kusikiliza kesi.

Mazingira hayo ya uvaaji ni korofi yanasumbua mahakama, uvaaji huo hi hatarishi kuvaliwa katika eneo la mahakama kwani linaweza kusababisha usikivu kupotea.

Tangazo lililowekwa na mahakama liheshimiwe, walinzi watimize wajibu kwa kuhakikisha wanaoshindwa kuvaa mavazi ya staha hawaruhusiwi kuingia mahakamani.

Walinzi wakizingatia maelekezo hayo itasaidia kulinda heshima ya mahakama, pia kwa wale wanaofahamu haya wasiwe wavivu kutoa elimu kwa wasiofahamu.

Utaratibu huo unamuhusu mtu yeyote mwenye shughuli mahakamani hapo wakiwamo mashahidi, wasikilizaji wa kesi na wanahohitaji huduma mbalimbali.

Aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kinondoni, Kwey Rusemwa aliwahi kusema mavazi hayo yanashusha heshima hivyo mtu anayefika mahakamani lazima avae mavazi ambayo si kero kwa mwingine.

Alitahadharisha anayefika mahakamani kuwa na khanga ili akibainika vazi alilovaa halistahili, aweze kujisitiri kwa kufunga khanga hiyo na kuingia mahakamani kupata huduma.

Haki ya kufika mahakamani ni ya kila mmoja lakini kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, ukiukwaji wa taratibu hizo kutasababisha kuikosa haki hiyo.

Ni wajibu wa kila mmoja kuilinda haki yake kwa kufuata utaratibu uliowekwa, utaratibu huo haumbani mtu bali unamjenga kujiheshimu.

Kuelekezwa kuvaa vazi la staha si kukubana bali kulinda heshima yako pamoja na eneo husika, mavazi yasiyo na staha yanajulikana mahali yanakostahili kuvaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles