KOCHA wa Manchester United, Van Gaal, amedai kwamba kutolewa katika michuano ya Kombe la Europa kutazidi kuwasaidia kufanya vizuri katika Ligi Kuu nchini England.
Klabu hiyo ilitolewa katika Ligi ya Europa na majogoo wa Liverpool, ambapo Van Gaal akadai kuhamishia nguvu zake Ligi Kuu na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wake, Manchester City, juzi.
Bao hilo lilifungwa na mchezaji chipukizi Marcus Rashford, mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Etihad.
“Katika mchezo wa juzi, tulionesha kiwango cha hali ya juu, hasa katika kipindi cha kwanza na tulipata nafasi nyingi, lakini tulishindwa kuzitumia.
“Katika kipindi cha pili tuliongeza bidii, japokuwa wachezaji wangu walikuwa wamechoka kutokana na mchezo wa katikati ya wiki Kombe la Europa, lakini tulifanikiwa kushinda kutokana na juhudi zilizofanywa na wachezaji.
“Ushindi huo ulikuwa muhimu sana kwetu na wa lazima, hii imetokana na kutolewa katika michuano ya Europa, nguvu zote zimehamishiwa Ligi Kuu. Kwa hali hii ni wazi kwamba kuna nafasi kubwa ya kupigania Top Four,” alisema Van Gaal.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na alama 50 sawa na West Ham, ambao wanashika nafasi ya tano, wakitofautiana kwa mabao.
Hata hivyo, kuna uwezekano wa kuondoka baada ya kumalizika kwa Ligi msimu huu, huku ikidaiwa kwamba Kocha Jose Mourinho anatarajia kuchukua nafasi hiyo.