Uzito mkubwa, shinikizo la damu bado tishio

0
800

NA VERONICA ROMWALD
– DAR ES SALAAM-
UZITO mkubwa na shinikizo la juu la damu ni matatizo ambayo yanaonekana ni tishio na yanazidi kuwatesa wananchi wengi,
huku wengine wakiwa hawajijui.

Kati ya watu 1,375 waliofika katika maonyesho ya Sabasaba na kupimwa afya zao asilimia 39.2 walikutwa na uzito mkubwa.

Hayo yalielezwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Pedro Pallangyo alipozungumza na MTANZANIA jana.

Alisema asilimia 31 ya watu hao 1,375 walikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.

“Wananchi hao walifika katika banda letu kule Sabasaba na walikuwa tayari kupima afya zao, wengi walikuwa hawajijui kama wana matatizo
hayo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, wagonjwa 39 walilazimika kupatiwa rufaa kufika katika taasisi hiyo kufanyiwa uchunguzi zaidi.

“Kati ya wagonjwa hao 39 ambao tuliwapa rufaa, wagonjwa 31 walikutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu na wagonjwa saba waligundulika kuwa na moyo mkubwa na mmoja alikutwa na tatizo kwenye milango ya moyo wake (valve),” alisema.

Dk. Pallangyo ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha utafiti na mafunzo wa taasisi hiyo, alisema wagonjwa hao tayari wamepatiwa matibabu stahiki.

Alitaja dalili za mtu mwenye tatizo la shinikizo la damu kuwa ni kuhisi maumivu makali ya kifua hasa upande wa kushoto.

“Kwa kawaida mtu akifanya shughuli yoyote ile mwili huhitaji kiwango fulani cha damu na mahitaji hayo hutofautiana kulingana na shughuli anayoifanya.

“Lakini kwa mtu mwenye shinikizo la damu, hata akifanya shughuli ndogo huhisi uchovu wa mwili jambo ambalo si la kawaida,” alisema.

Alisema zipo sababu nyingi zinazochangia mtu kupata tatizo la shinikizo la juu la damu, ikiwamo ulaji mbovu, kutokufanya mazoezi,
uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi.

“Lakini kuna magonjwa kama vile kisukari, ambayo huweza kusababisha mtu kupata tatizo.

“Lakini sababu nyingi zinaepukika hivyo naishauri jamii kubadilika,” alishauri daktari huyo ambaye pia ni mshindi wa
tuzo la Watafiti Vijana wa Afrika kwa Mwaka 2017.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here