27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Uzembe, mwendokasi ulivyokatiza maisha ya watumishi wa umma 34

Na ANDREW MSECHU

JUZI Askari Polisi watatu walifariki dunia na wawili kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kwenye Kijiji cha Kilimahewa Barabara ya Kilwa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa kipolisi Rufiji.

Msemaji wa Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), David Misime, alisema askari hao waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili PT.3822 aina ya Toyota Cruiser mali ya jeshi hilo ambapo walikuwa wakitokea Ikwiriri kwenda Kijiji Cha Mwalusembe.

Alisema gari hilo lilipasuka gurudumu la nyuma upande wa kulia na kupinduka na kusabababisha vifo vya askari vifo na majeruhi.

Ajali hiyo inafanya watumishi wa umma waliopoteza maisha katika ajali ndani ya mwaka mmoja na nusu kufika 34.

Kwa mujibu wa polisi ajali nyingine zilizotokea na kusababisha vifo ni ile iliyohusisha gari la wafanyakazi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), iliyotokea Juni 25 na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi watatu.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Izazi Kata ya Izazi Tarafa ya Isimani Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma Mkoani Iringa, ikihusisha gari lenye namba  za usajili STL 3807 Toyota Hilux mali ya Tarura Mkoa wa Songwe.

Gari hilo lilikuwa likitoka Iringa kwenda Dodoma likagongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T146BAZ aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa linatokea Dodoma kwenda Iringa.

Ofisa Mnadhimu wa Trafiki Makao Makuu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdi Isango, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi na uzembe wa dereva wa fuso aliyeshindwa kulimudu gari lake na kuhama upande wa pili na kugongana na gari la Tarura.

ACP Isango alisema kwa kiasi kikubwa, ajali nyingi zinazohusisha  magari ya umma, chanzo kikuu kinaonekana ni mwendokasi wa madereva.

 “Madereva wengi hasa wanaoendesha magari ya Serikali wana dhana kuwa kwa sababu wao ni watumishi wa Serikali hawaguswi na sheria,” alisema.

Alisema japokuwa polisi wa Usalama Barabarani wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu na kudhibiti mwendokasi na uzembe, matatizo ya ajali hizo zimeendelea kujirudia kila wakati, suala linalohitaji utayari wa viongozi na watumishi wa Serikali kuwajibika.

ACP Isango alisema taarifa zao zinaonesha idadi ya vifo vya ajali zinazohusisha magari ya  umma vinaongezeka kila wakati.

Alisema ajali nyingine iliyohusisha gari la umma, ni ya gari lililokuwa limebeba wataalamu wa Wizara ya Ardhi,  iliyotokea Ifakara mkoani Morogoro.

Alisema ajali hiyo ilitokea Mto Kikwila katikati ya mji wa Kiberege na Ifakara wilayani Kilombero mkoani Morogoro Februari 23.

Katika ajali hiyo, anasema vifo vilikuwa tisa na majeruhi wanne, huku chanzo pia kikitajwa ni uzembe wa dereva.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop lenye namba za usajili STK 9444 mali ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori, ambalo liliacha njia na kutumbukia mtoni.

ACP Isango alisema chanzo cha ajali kilikuwa mwendokasi wa gari hilo uliosababisha dereva kushindwa kulimudu na kuacha njia, kisha kutumbukia mtoni.

Ajali nyingine ni iliyohusisha watumishi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Kijiji cha Mbande Kata ya Sejeli huko Kongwa, Dodoma Novemba 3, 2018 kwenye barabara ya Morogoro Dodoma.

Alisema katika tukio hilo gari lenye namba za usajili STL 6250 Toyota Land Cruiser mali ya Ofisi ya CAG iliigonga kwa nyuma lori lenye namba T161CBB/T152CBB aina ya DAF, kisha kwenda kugongana uso kwa uso na gari lenye namba SU 41173 mali ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PSSSF).

Alisema ajali hiyo ambayo chanzo chake ni mwendokasi wa gari lenye namba STL 6250 Toyota Land Cruiser mali ya Ofisi ya CAG, ilisababisha vifo saba na majeruhi watatu.

“Ajali nyingine ni hii iliyohusisha wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo huko Manyoni, Singida. Ajali hii iliyotokea Oktoba 21 mwaka jana kwenye eneo la Njirii Manyoni barabara kuu ya Manyoni – Singida Wilaya Manyoni ilisababisha vifo vitano na majeruhi mmoja.

“Ajali hii ilihusisha gari lenye namba za usajili STK 8925 Mitsubishi Pajero liligongana uso kwa uso na lori la mafuta lenye namba za usajili RL-1177 na kisha kuacha njia na kupinduka, chanzo kikiwa ni mwendokasi wa gari na ku-overtake (kupita magari mengine)  bila ya kuchukua tahadhari,” alisema.

ACP Isango alitaja ajali nyingine iliyochangia kuongeza vifo na majeruhi kuwa ni ile iliyomhusisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala iliyotokea huko Babati, Manyara Agosti 4, 2018.

Alisema chanzo cha ajali hiyo  iliyohusisha gari lenye namba za usajili STL 5718 Land Cruiser V8 lililoacha njia na kupinduka na kusababisha kifo kimoja na majeruhi watatu, ni mwendokasi wa gari uliomfanya dereva ashindwe kulimudu alipojaribu kukwepa twiga.

“Lakini pia tunaona kuna ajali iliyotokea Julai 30, 2018 iliyomhusisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara huko Geita. Hii ilihusisha gari namba STK 9565 Toyota Land cruiser mali ya Wizara ya Viwanda ambalo liliwagonga watembea kwa miguu wawili na kisha kuacha barabara kupinduka.

“Ajali hii ambayo pia chanzo chake kilikuwa mwendokasi uliosababisha dereva kushindwa kulimudu gari na kupinduka ilisababisha kifo kimoja na Majeruhi sita,” alisema.

Aliaeleza kuwa katika ajali nyingine ilihusisha watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilitokea Julai 14, 2018 huko Singida ikihusisha gari yenye namba za usajili DFPA 0148 Toyota Hilux mali ya halmahauri hiyo, ambalo liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo viwili na majeruhi watano.

Alisema chanzo cha kilikuwa ni kupasuka kwa tairi la mbele upande wa kushoto kulikosababisha gari hilo kuacha njia na kupinduka.

ACP Isango alisema katika ajali nyingine ilihusisha wataalamu wa Uwekezaji (TIC) waliokuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara Mei 21, 2018 huko Msoga, Chalinze, gari yenye namba STK.5923 aina Toyota Land Cruiser mali ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lligongana na gari namba T. 620AQV/ T.407DBY aina ya Scania.

“Ajali hii hii ilisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi mmoja, lakini chanzo chake pia ni mwendokasi na uzembe wa dereva wa gari namba STK 5923 mali ya wizara,” alisema.

ACP Isango alisema ajali nyingine iliyosababishwa na mwendokasi na dereva kushindwa kulidhibiti gari alipojaribu kumkwepa mtembea kwa miguu aliyekuwa akivuka barabara ilitokea Machi 29, 2018 huko Gwata, barabara ya Dar es Salaam – Morogoro.

Alisema ajali hiyo ilihusisha gari yenye namba za usajili Z374HA aina ya Toyota Prado iliyokuwa ikiendeshwa na mbunge wa Jimbo la Mfenesini Zanzibar, Masoud Ally, aliyekuwa akitokea Dodoma kuelekea Dar es Salaam, iliyoacha njia na kupinduka, hivyo kusababisha Majeruhi watano waliokuwa wakisafiri kwa gari hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles