*Kufikia tani 756,000 ifikapo 2025
Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Bodi ya Sukari imesema uzalishaji wa sukari nchini umeongezeka kutoka tani 110,000 mwaka 2004 hadi 380,000 kufikia Juni 30, mwaka huu.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Oktoba 25,2022 na Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Profesa Kenneth Bangesi wakati kueleza utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo na mwelekeo kwa mwaka wa fedha 2022/2023
Mkurugenzi huyo amesema uagizaji huo wa sukari ulikuwa unagharimu zaidi ya Sh bilioni 300.
Amesema jitihada zinazofanyika za upanuzi na uanzishaji wa viwanda vya uzalishaji wa sukari, vitawezesha kufikia tani 756,000 ifikapo mwaka 2025 na hivyo kuondokana na uagizaji wa sukari kawaida.
Prof. Bangesi amesema kuwa mahitaji ya sukari ya kawaida nchini hadi kufikia Juni 30, 2022 mwaka huu ni tani 645,000 ambapo kati ya hizo tani 440,000 ni za kawaida na tani 205,000 ni za viwandani.
Amesema hadi sasa uzalishaji wa sukari ya viwandani haujaanza nchini na kwamba ulichelewa kutokana na soko la mahitaji ya sukari ya kawaida kuwa kubwa sana nchini.
Amesema hali ya uzalishaji iliyopo hivi sasa, kwa mwaka jana walizalisha tani 379,000 na hivyo iliacha pengo la tani 60,000 ambayo ilitakiwa kuagizwa kuziba pengo hilo la sukari nchini,”amesema.
Amesema kwa takwimu hiyo upungufu kwa sukari ya kawaida ni tani 60,000 wakati kwa sukari ya viwandani ni tani 205,000.