25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Uzalendo huu Stars uendelezwe

Watanzania wameendelea kutembelea vifua mbele kutokana na matokeo mazuri ya timu yao ya Taifa, Taifa Stars ambayo imeendelea kuyapata katika michezo yake ya mashindano mbalimbali ya kimataifa.

 Hatua hiyo inatokana na ushindi wa mabao 2-1  ilioupata Taifa Stars, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika(Afcon 2021)dhidi ya timu ya Taifa ya Guinea ya Ikweta Ijumaa iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ulikuwa ushindi muhimu katika harakati za Taifa Stars kuisaka tiketi ya tatu ya Afcon, baada ya kufanikiwa kufanya hivyo mara mbili, mwaka 1980 zilipofanyika nchini Nigeria na mwaka huu zilipoandaliwa na Misri.

Hakika mwenendo huu wa sasa wa Stars unatia faraja  kwa miaka mingi Watanzania walikuwa wakitamani kushangilia mafanikio ya timu yao ya taifa kama wenzao wa mataifa mengine yanayofahamika kwa umahiri katika mchezo wa soka yakiwemo Misri, Cameroon, Nigeria na Ghana.

Umeanza kufikia wakati sasa, mashabiki wa soka hapa nchini wanaenda uwanjani kuishangilia Taifa Stars huku mioyo yao  ikiwa na utulivu wa kutosha ikiamini ushindi upo.

Hapo kabla hili lilikuwa gumu kwakua ilikuwa nadra sana bila kujali inacheza ugenini au nyumbani Watanzania kuishuhudia timu yao ya Taifa ikiwafurahisha kwa kuibuka na ushindi baada ya dakika 90.

Sisi MTANZANIA tunachukua fursa hii kuwapongeza wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa benchi la ufundi na wasimamizi wa mchezo wa soka  hapa nchini yaani Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), kwa hii picha nzuri inayoanza kuonekana katika mchezo huu unaopendwa na mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Ikumbukwe kwamba, Taifa Stars pia imefuzu kwa mara ya pili kushiriki fainali zijazo za Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, yaani Chan ambazo zitafanyika mwakani nchini Cameroon.

Pia mwenendo wake ni mzuri katika michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zijazo zitakazofanyika mwaka 2022 nchini Qatar.

Ni wazi matunda yanayoanza kuvunwa katika soka hapa nchini hayatokani na miujiza bali ni mipango thabiti iliyowekwa.

Kwenye mchezo dhidi ya Guinea ya Ikweta, wachezaji wa Stars walionesha maana halisi ya uzalendo kwa taifa.

Hali hiyo ilionekana kutokana na jinsi kila mmoja aliyepewa nafasi ya kiucheza mchezo huo alivyokuwa akipambana kuhakikisha Tanzania inapata ushindi nyumbani dhidi ya wageni.

Ndiyo maana haikuwa ajabu Guinea kutanguliwa kufunga bao la kuongoza kabla ya Stars kusawazisha na kufunga la ushindi.

Hivyo ndivyo inavyopaswa kulipigania taifa, kwani licha ya kuwa nyuma lakini wachezaji  wa Stars hawakuonekana kukata tamaa badala yake waliendelea kupambana wakiamini wanao uwezo wa kushinda.

Sasa Stars itakabiliana na Libya katika mchezo wa pili wa kusaka tiketi ya Afcon.

Katika mchezo huo Stars itakuwa ugenini.

Kama ilivyoonekana Ijumaa iliyopita pale Uwanja wa Taifa, silaha pekee itakapoiwezesha Stars kuishinda Libya ni kila mchezaji kujituma kwa dhati kuipigania Tanzania wakati huo huo kutekelezwa kwa ufasaha maelekezo ya benchi la ufundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles