26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

UWT Njombe washerehekea siku ya wanawake wakiwakumbuka watoto wanaoishi mazingira magumu, wazee

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Baadhi ya wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhenga Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamepatiwa sare za shule na mahitaji mengine muhimu ili waweze kuhudhuria masomo vizuri.

Misaada hiyo imetolewa kwa ushirikiano wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Njombe na UWT Wilaya ya Wanging’ombe katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa kiwilaya katika Kata ya Uhenga.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Scholastica Kevela, amesema wao ni walezi ndiyo maana wameguswa kuwanunulia mahitaji hayo muhimu ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Scholastica Kevela, akizungumza na mmoja wa wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhenga baada ya kuwapatia misaada mbalimbali.

“Tunatambua jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya elimu, na sisi tumeona tutumie siku hii muhimu kumuunga mkono kwa kuangalia makundi muhimu kama ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na wazee,” amesema Kevela.

Amesema pia jamii ina wajibu wa kuwatunza wazee na kuwataka vijana na wanawake wenye uwezo kuliangalia kundi hilo muhimu badala ya kuwaacha wakihangaika.

Baadhi ya wazee walioshiriki maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa kiwilaya katika Kata ya Uhenga Wilaya ya Wanging’ombe, Njombe.

Wanafunzi waliopatiwa misaada hiyo wameshukuru umoja huo na kuahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao na kuwasaidia wazazi wao baadaye.

Baadhi ya madiwani wa viti maalumu waliohudhuria hafla hiyo wamewahimiza wanawake kuzingatia lishe bora ili kuondoa tatizo la udumavu linaloikabili wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe.

Kwa upande wao wanawake wa Kata ya Uhenga wameishukuru Serikali kwa jitihada za kuwakwamua kiuchumi ambapo vikundi saba vimenufaika huku kimoja kikipata mradi wa ufugaji kuku 700 kutoka shirika la kuhifadhi mazingira na kurejesha uoto wa asili.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake 2024 inasema; Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles