25 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Uwepo wa kaya hewa Tasaf ni hujuma kubwa kwa Taifa

Mwandishi WetuYohana Paul

MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ulianza rasmi nchini mwaka 2000 chini ya udhamini wa Benki ya Dunia (WB), kwa lengo la kupunguza tatizo la umasikini huku walengwa wakiwa ni wananchi wanaotoka katika kaya zisizojiweza na zinazotazamwa kuishi katika umasikini uliotukuka.

Tangu kuanzishwa kwake, mradi unatajwa kuchangia kubadili kwa kiwango kikubwa maisha ya wanufaika na kuwajengea uwezo wa kuanzisha vitega uchumi na hivyo kuwafanya wasiwe wategemezi tena badala yake wameweza kujitegemea kiuchumi na kukidhi mahitaji yao ya msingi ya kila siku kama malazi, mavazi na makazi.

Mpango huo ambao sasa unaingia kipindi cha pili cha awamu ya tatu hadi kufikia mwaka 2023, unakadiriwa kuwa utatumia kiasi cha Sh trillion 4.1 kwa ajili ya utoaji ruzuku kwa wanufaika sambamba na utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii ili kusaidia wananchi masikini kupata huduma hizo bila gharama kubwa na kwa ukaribu zaidi.

Licha ya kuwa matarajio ya kuanzishwa kwa mpango huo ni kuona wanufaika kwa maana ya walengwa halali ndio wanafikiwa na mradi huo, ili kutimiza lengo la Benki ya Dunia na serikali kwa ujumla lakini imeonekana baadhi ya watendaji waliokabidhiwa kusimamia mpango huo wamefanya undanganyifu kama si ubadhirifu kiasi cha kusababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya kaya masikini hewa na hata wanufaika wake kuwa si walengwa.

Hali hiyo imethibitishwa na Rais Dk. John Magufuli wakati akifungua kipindi cha pili cha awamu hiyo ya tatu cha mpango huo ambapo aliweka wazi uwepo wa idadi kubwa ya kaya masikini hewa, ambazo zipo katika mfumo wa kupokea ruzuku ya Tasaf huku wanufaika wake wakiwa hawapo ama waliopo hawana vigezo vya kupewa ruzuku hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu alizozitoa Rais Magufuli, katika uhakiki wa kaya masikini uliofanywa kuanzia Novemba 2015 hadi Juni mwaka 2017 zilibainika kaya hewa 73,5621 ambapo 22, 034 zilithibitika kuwa wanakaya wake si masikini, kaya 18, 700 zilikuwa na mwana kaya mmoja au wote wameshafariki, kaya 18,700 hazikujitokeza mara mbili kuchukua ruzuku.

Nyingine ni kaya 9,903 zilizohamia vijiji, mitaa na shehia ambapo mpango huo haujaanza kutekelezwa na kaya 5134 wanakaya wake walibainika kuwa walikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa kamati ya usimamizi jamii, halmashauri za vijiji na mitaa pia viongozi na watendaji.

Kwa takwimu hizo ni wazi kuwa watendaji waliopewa mamlaka wamehusika moja kwa moja na madudu hayo ambayo binafsi nayatazama kama hujuma kubwa kwa taifa ambalo serikali yake inapambana kufikia uchumi wa kati na kupunguza changamoto ya umasikini kwa watu wake.

Uwepo wa idadi hiyo kubwa ya kaya masikini hewa inatoa taswira kwamba watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezwaji wa mpango huo, wengi wao wamekuwa wakilenga kujinufaisha ama kuwanufaisha watu wao wa karibu kwa fedha za Tasaf chini ya kivuli cha Kaya masikini bila kujua kitendo hicho kinawakosesha haki yao walengwa.

Sakata hili la kaya masikini hewa linanikumbusha ule mchakato wa kutumbua wafanyakazi hewa uliosimamiwa na Rais Magufuli kwa kuwa yote kwa pamoja imechangia kuwanufaisha watu wasio na sifa huku wenye sifa wakikosa haki yao.

Sote tunafahamu serikali imekuwa ikitumia pia fedha hizo kutekeleza miradi yenye lengo la kuchochea maendeleo ya uchumi hususani miundombinu ya usafiri, nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini, kwa kuwa asilimia kubwa ya wananchi maskini wanaishi vijijini lakini linapokuja suala la kaya hewa masikini kwa kiasi kikubwa linakuwa linachangia si tu kuwazibia riziki walengwa bali pia kukwamisha ukamilishwaji wa miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Kwa hakika kuwepo kwa kaya hewa takribani 73,000 ni jambo ambalo naamini kila mtanzania mwenye kiu ya maendeleo na taifa lake hajafurahishwa nalo na binafsi kama mtanzania na mwananchi wa kawaida nalitazama kama hujuma kubwa kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.

Ni imani yangu mamlaka zinazohusika zitafanya kazi yake ili kumsaidia Rais kufanikisha adhma ya kuondoa kabisa kaya hizo masikini hewa ili wanaoendelea kunufaika na fedha hizo za Tasaf basi wawe ni wale tu wenye sifa ambao kwa namna moja au nyingine wamekidhi vigezo na wanastahilli kupata ruzuku ya kaya masikini kwa kufanya hivyo tutachangia kuongeza kasi ya kupunguza tatizo la umasikini kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,540FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles