Na Mwandishi Wetu, Pemba
Vijana kisiwani Pemba wanatarajiwa kunufaika na aajira kutokana na uwekezaji unaotarajiwa kujfanyika kwenye sekta ya samaki.
Hayo yameelezwa leo Januari 6, na Mwenyekiti wa Chama cha ACT –Wazalendo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kwenye ziara yake kisiwani Pemba.
Amesema tayari yupo muwekezaji ambae ataleta boti za kisasa za uvuvi kwalengo la kufanya uvuvi wa kisasa sambamba na kujenga kiwanda cha kusindika samaki, jambo ambalo litazalisha nafasi kadhaa za ajira kwa Wananchi wa kisiwa cha Pemba.
Aidha, ametoa ufafanuzi juu ya wale wananchi wanaokoseshwa ajira kwa sababu za kiitikadi za kisiasa kwa kusema;
“Nikweli kulikuwa na changamoto katika baadhi ya taasisi za kiserikali katika kuajiri, lakini kwasasa serikali itaanzisha mfumo rasmi wa kimtandao kwa kuomba ajira na sio kama zamani, jambo ambalo litapunguza ukiritimba wa kiubaguzi wa kisiasa.
“Pia niwatake wananchio ambao hamko kwenye vikundi vya Saccos zilizopo, kuanzisha vikundi vyenu na kuhakikisha vinasajiliwa na kuanza shughuli za kijasiriamali ili kujikimu kimaisha,” amesema Maalim.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa za viongozi wote wa taasisi za umma ambao hawawatendei haki Wananchi ama wanaofanya kwa upendeleo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Maalim Seif pia ameendelea kusisitiza kwa Wanachama na viongozi wa Mkoa wa Mkoani Pemba kichama kuhakikisha wanafanya shughuli za Chama kwa lengo la kuimarisha Chama hicho.
Maalim Seif ameahidi kuendelea na ziara yake ya Kisiasa na kiserikali katika Kisiwa cha Unguja ili kuleta umoja na mshikamano katika Nchi ya Zanzibar na kuimarisha Chama.
Baada ya kikao hicho Maalim Seif alikwenda kumpa mkono wa pole mbunge mstaafu wa Viti maalum wa Chama cha Wananchi (CUF), Halima na familia yake kwa kufiwa na mama yao katika kijiji cha Kichunjuu Mkoa wa Kusini Pemba. Kiongozi huyo amekamislisha rasmi ziara yake kisiwani Pemba.