Na Mwandishi Wetu
-PEMBA
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umerusha kombora kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na kusema kuwa kiongozi huyo na chama chake sasa wamejikita kwenye siasa chafu za kupandikiza chuki na uchochezi wenye malengo hatarishi kwa Taifa.
Kutokana na hali hiyo umoja huo umesema kuwa ushindani wa hoja kwa hoja umeachwa na badala yake wamehamia kukaanga mbuyu kwa kuigombanisha Serikali ili ichukuwe na wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana Kisiwani Pemba na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, wakati wa kuhitimisha ziara yake kisiwani hapa.
Alisema katika masuala ya utawala jambo la kuingia mikataba au kuvunjwa ni mambo yanayojitokeza hivyo haiwezi kuwa ndiyo hoja ya msingi kwa mwanasiasa na chama chake kupoteza muda na kuzungumzia jambo ambalo lipo mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Licha ya hali hiyo alisema hata Waziri Mkuu Mstaafu ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye aliwahi kuvunja Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam na madiwani wakapoteza nafasi zao.
Alisema bila shaka alitimiza wajibu huo kwa kutazama masilahi mapana ya maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam na ufanisi wake kwa ujumla.
“Mungu ampe upeo Tundu Lisu hajui masuala ya utawala katika medani za kidola kwa vile ni mwanasiasa mwanagenzi asiye na uzoefu wa kutosha na ni mtu wa kukurupuka. Kama hoja yake ni kudaiwa, Serikali zote duniani, taasisi za kibenki, mashirika ya kimataifa pia hudaiwa , hakuna asiyedaiwa,” alisema Shaka.
Alisema waziri mwenye dhamana au kiongozi yoyote mwandamizi wa serikali hawezi kuamka nyumbani wake akavunja mkataba iwapo mambo hayaendi kama ilivyokusudiwa bila kupata idhini ya Baraza la Mawaziri kama anaavyofikiri Lissu na wenzake.
“Lissu anafanya uchochezi wa kisiasa ili kujitafutia umaarufu kwa masuala ambayo hayamsaidii yeye wala Chadema wanadhani wanapambana na mtu. Mbona hakuhoji Sumaye na Lowasa jinsi walivyoshiriki kuvunja mikataba. Asitegemee kupata sifa kwa kujionyesha kwake si mzalendo halisi kwa taifa,” alisema