*Kuzunguka Mikoa yote nchini
Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, mwaka huu, Umoja wa Vijana (UVCCM) Taifa umezindua kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa.
Katika kampeni hiyo zaidi ya vijana 3,000 kutoka Chama Cha Mapinduzi walijitokeza katika maandamano yaliyoanzia Uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa hadi uwanja wa Mwembe Yanga, Temeke wakiwa na mabango mbalimbali yenye ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwahuku wakiwa wamevalia fulana za rangi mbalimbali zenye picha ya Rais Samia Suluhu Hassan,
Akizungumza Dar e Salaam Leo Alhamisi Juni 23, mara baada ya kuzindua kampeni hiyo, Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Kenan Kihongosi amesema kuwa kampeni hiyo itakuwa endelevu katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Kusini pamoja na Zanzibar.
Amesema umoja wa vijana una wajibu wa kuungana na Serikali, kueleza wananchi juu ya umuhimu wa sensa ya watu na makazi katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tumeona baadhi ya maeneo kuna changamoto, watu waliohesabiwa mwaka 2012 wengine hawakuhesabiwa, serikali inapotoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni kwa idadi ya watu walioandikishwa na kuhesabiwa, siku ya leo tuna watu watatoa elimu na kutunga nyimbo kwa ajili ya kuhamasisha sensa.
“Kampeni hii tumeizindua Dar es Salaam, tutakwenda maeneo mengine na tutaifanya kampeni hii kwa ukubwa, lengo ni kuunga mkoa juhudi za serikali ya awamu ya sita na utekelezaji wa Ilani ili kuhakikisha serikali inatimiza wajibu wake wa kutambua idadi ya watu,’’ amesema Kihongosi.
Kihongosi amesema katika kampeni hiyo watajumuika na wataalamu mbalimbali kutoka serikalini, ambao wataeleza faida watakazopata wananchi juu ya umuhimu wa kuhesabiwa.
Awali, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala amesema, takwimu za watu waliopo sasa ni ya mwaka 2012, hivyo wameamua kuunga juhudi za serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa, huku akiwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kuhesabiwa.
“Tukihesabiwa miundombnu itaboreshwa na hata tatizo la ajira kwa vijana litapata ukombozi, tunalalamika vijana hawana ajira lakini serikali ikitambua idadi yetu itajua namna gani itataua tatizo hili,’’amesema.
Katibu wa CCM tawi la Tandale Bundara Malima amesema ni muhimu wananchi kujitokeza kuhesabiwa kwani takwimu za Watanzania itairahisishia serikali kutenga bajeti kulingana na idadi ya watu waliopo.