23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Utumbuaji majipu wazuiwa kiaina

RAIS MAGUFULI (1)

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HUKU kukiwa na sintofahamu kuhusu staili ya kufukuza na kusimamisha kazi watumishi mbalimbali wa umma maarufu kama ‘kutumbua majipu’, Serikali imebadili utaratibu huo na kutoa maelekezo mapya kupitia halmashauri nchini.

Chanzo chetu cha habari kutoka halmashauri moja nchini kimesema Serikali imezipiga marufuku halmashauri zote  kuwachukulia hatua watumishi na kwamba  sheria, kanuni na taratibu zizingatiwe kabla ya kuchukuliwa uamuzi wowote.

Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani Novemba mwaka jana amekuwa akiwasimamisha kazi watumishi mbalimbali kwa uzembe na ufisadi huku viongozi wengine wa chini nao wakiiga staili hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka   halmashauri hiyo, hatua ya kupiga marufuku ‘utumbuaji’ huo   imetolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiwaelekeza  makatibu tawala wa mikoa kuhusu mwongozo wa  utendaji kazi.

Inaelezwa kuwa  watendaji wa halmashauri wanaonywa kuwa: “Ofisi ya Waziri Mkuu haitarajii kusikia au kupokea azimio la halmashauri kumkataa mtumishi wa umma.

“Baada ya mwongozo huu kusomwa kwenye mabaraza ya madiwani, ofisi hii (Tamisemi) haitarajii kusikia au kupokea azimio la halmashauri linalohusu kumkataa mtumishi wa umma badala yake halmashauri wachukue hatua kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na mwongozo.”

Mbali na hilo, watendaji hao wamekumbusha   kuwa Serikali imekuwa ikitoa miongozo ya aina hiyo, lakini imekuwa haitekelezwi kwa ukamilifu.

“Hatua hii inalenga katika kuhakikisha kunakuwapo na maadili, uadilifu na usimamizi wa dhati katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya shughuli za serikali.

“Hali halisi ya utekelezaji inaonyesha kwamba mwongozo huo haukutekelezwa kwa ukamilifu, hivyo Ofisi ya Rais, Tamisemi iliwaandikieni barua yenye Kumb.Na.CAB.112/497 ya Machi 13, 2013 ikiwakumbusha kuhusu mwongozo wa namna ya kuchukua hatua za  nidhamu kwa watumishi wanaofanya kazi katika mamlaka za serikali za mitaa,” kimesema chanzo chetu kikizungumzia maelekezo hayo na kwamba maelekezo hayo yanaendelea kusema:

“Pamoja na kuwapo mwongozo huu ambao ulisambazwa kwenye halmashauri zote Tanzania Bara, yamekuwapo  matukio ya baadhi ya mabaraza ya madiwani katika baadhi ya halmashauri kupitisha maazimio ya nidhamu.

“Vitendo vya kuwakataa watumishi ikiwa ni pamoja na wakurugenzi ni ukiukwaji sheria zinazosimamia utumishi wa umma kwa kuwa adhabu ya kumkataa mtumishi haipo katika utumishi wa umma Tanzania.

“Kwa barua hii tunaomba muwafikishie wakurugenzi wa halmashauri mwongozo huu wa mwaka 2006  wausome upya kwenye mabaraza ya halmashauri zote Tanzania Bara.

Chanzo chetu kilisema maelekezo hayo pia yalielekeza  kuwa mwenyekiti wa halmashauri atawasilisha maoni ya mkuu wa wilaya au mkoa kwenye baraza la madiwani na kuzitolea uamuzi na mapendekezo.

Kilisema maelekezo hayo yanaendelea kusema: “Mapendekezo ya Halmashauri yatapelekwa kwa mamlaka ya nidhamu ya mtumishi huyo kupitia kwa RC. Ieleweke kuwa halmashauri haitachukua hatua zozote za  nidhamu dhidi ya mtumishi yeyote wa kundi hili.

“Pale itakapoonekana kuwa ni lazima kuchukua hatua za  nidhamu dhidi ya mtumishi wa aina hii, basi mamlaka yake ya nidhamu itafanya uchunguzi wa awali na kuendelea na taratibu za  nidhamu kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma”.

Waraka huo pia ulieleza kuwa kwa mujibu wa kanuni 35(2)(a) ya kanuni za utumishi wa umma 2003, mamlaka ya nidhamu ya wakurugenzi wa majiji na watendaji wakuu wa tume ambao huteuliwa na rais ni Katibu Mkuu Kiongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles